Msimu wa soka katika ligi ya
uingereza unaanza rasmi jumamosi huku kilabu ya Manchester City ikianza
kulitetea taji lake,Manchester United nayo ikianza msimu mpya na kocha
Luis Van Gaal,liverpool ikianza maisha bila mfungaji wao matata Luis
Suarez pamoja na chanagmoto chungu nzima katika kinyanganyiro cha taji
hilo.Swali ni Je, Kocha Jose Mourinho atakiongoza kikosi kipya cha
Chelsea kushinda taji la mwaka huu?Je Arsenal imeimarisha kikosi chake
ilivyo ili kuweza kupigania taji la ligi hiyo.Maswali hayo yatapata jibu
katika kipindi cha miezi tisa inayokuja.
'Liverpool'

Katika usajili wake Meneja wa Liverpool Brendan Rogers amemsajili mlinzi Dejan Lovren
Baada ya kuishia kunawa katika mechi
tatu za mwisho msimu uliopita,Liverpool hadi sasa imekwishasajili
wachezaji wanane wapya ikiwa ni kujiandaa kwa msimu mpya ambapo pia
itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya huku wakiwa na
kikosi kipana kilichosheheni nyota kadhaa mahiri katika usakataji
kabumbu.
Katika usajili wake Meneja wa Liverpool Brendan
Rogers amewasajili mlinzi Dejan Lovren, Kiungo Adam Lalana,na
mshambuliaji Rickie Lambert.
Wote hao kutoka Southampton,huku akiwasajili
kiungo Emre Can,na mshambuliaji wa pembeni Lazar Markovic na sasa
ameimarisha tena idara ya ulinzi kwa kumleta Beki wa Pembeni Alberto
Moreno kutoka Sevilla ya Uhispania ili kuimarisha mapengo yaliyojitokeza
msimu uliopita.
Ingawa inaaminika kuwa Pengo la Luis Suarez
litakuwa gumu kuzibika hasa kutokana na kiwango alichokionyesha msimu
uliopita pale alipoweza kutupia kambani bao 30
'Arsenal'

Arsenal imemsajili winga machachari wa Chile Alexis Sanchez
Nayo Arsenal baada ya ukame wa miaka mingi
hatimaye ndani ya miezi mitatu imekwishaanza kuzoa mataji mawili baada
ya kutwaa kombe la FA majuzi iliopowachapa Mabingwa watetezi Man City
bao 3-0 katika mechi ya ngao ya jamii kufungua pazia la msimu huu
unaoanza.
Bila shaka mashabiki wa Arsenal watakuwa
wanasubiri kwa hamu kuona iwapo timu hiyo itaendeleza moto huo pamoja na
kumpoteza mlinzi wake Thomas Vermaelen aliyejiunga na Barcelona na
Bacary Sagna aliyetimkia Man City ,lakini wamemsajili winger machachari
wa Chile Alexis Sanchez,Mathieu Debuchy wa Ufaransa,na mlinzi Calum
Chambers ili kuimarisha kikosi cha timu hiyo almaaruf the Gunners.
'Manchester united'

Kocha mpya Van Gaal anatarajiwa na wengi kurejesha moto wa kabumbu katika klabu ya Man u
Kwa upande wake Manchester United baada ya
kutepeta msimu uliopita imeanza kwa kupata kocha mpya mwenye rekodi ya
mafanikio Mholanzi Luis Van Gaal,huku pia ikimsajili Kiungo Ander
Herrera na Mlinzi kinda wa pembeni Luke Shaw ambao wanataraji
kushirikiana na wakongwe waliosalia kwenye timu hiyo.
Ingawa bado usajili unaweza kufanyika katika
wiki tatu zijazo kabla ya kufungwa dirisha la usajili huku akiwa tayari
ameshashinda mechi mbili za kujiandaa na msimu kwa kuilaza Liverpool na
Valencia matokeo ambayo yamewapa matumaini makubwa mashabiki wa Timu
hiyo maarufu kama mashetani wekundu.
'Chelsea'

Didier Drogba atachezea Chelesea licha ya wnegi kusema kuw aumri wake umesonga mno
Naye Kocha Jose Mourinho akiwa na kikosi
kilichozidi kuongezewa ubora kwa kuwasajili Diego Costa na Cesc
Fabregas,anataraji kuwa na kikosi kamili msimu huu ambapo pia
amemrejesha mkongwe Didier Drogba licha ya kuwa umri wake umesonga
mbele.
'Manchester City'
Nao mabingwa watetezi Manchester City wakiwa
wameimarisha idara ya ulinzi kwa kuwasajili Mlinzi ghali Eliaquim
Mangala kutoka Porto na Bacary Sagna kutoka Arsenal msimu huu
watakabiliana na changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa wanatetea Ubingwa
wao,huku wakiwa wamemuazima Kwa muda Kiungo wa zamani wa Chelsea Frank
Lampard
'Timu nyinginezo'
Ingawa Timu kubwa kubwa ndizo zinatajwa
sana,lakini Everton,Tottenham Hotspurs, na Swansea nazo huenda zikatoa
changamoto katika mbio za kuwania Ubingwa huo wa Ligi kuu England.
Aidha mashabiki wa soka watakuwa wakifuatilia
kuona Southampton itakabiliana vipi na timu pinzani hasa baada ya
kuondokewa na nyota wake watano bila shaka ambao wameuzwa katika timu
kubwa na Liverpool,Man United na Arsenal.
Huu ni msimu mpya utakaokamilika mwezi May
mwakani ambapo Idhaa ya Kiswahili ya BBC kupitia Ulimwengu wa soka
itakuwa hewani kila Jumamosi na Jumapili kukuletea moja kwa moja mechi
hizo kupitia Radio washirika.