Dar es Salaam. Safu ya ushambuliaji ya Simba
imeimarika baada ya kumsajili mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Elias
Maguli pamoja na kuwasili kwa kiungo Mrundi Pierre Kwizera (23) jana
mchana.
Maguli amesaini mkataba wa miaka miwili jana
mchana na sasa anatengeneza kombinesheni na Mrundi Amisi Tambwe katika
safu ya ushambuliaji.
Maguli msimu uliopita alifunga mabao 14 na
kukamata nafasi ya pili katika orodha ya wapachika mabao nyuma ya
Tambwe aliyefunga mabao 19.
Maguli alisema, anajisikia furaha kujiunga na Simba, kwa vile ni miongoni mwa timu kubwa na kongwe hapa nchini.
“Nimesaini mkataba wa miaka miwili leo ya
kuichezea Simba na bila kuficha nina furaha kujiunga na timu hii kwani
ni timu kubwa hapa nchini.
“Najua kuna changamoto kuichezea timu kubwa kama Simba lazima nipo tayari kukabiliana nazo na kuzishinda,” alisema Maguli.
Aliongeza: “Nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kutoa mchango utakaosaidia timu kupata mafanikio.”
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire
alilithibitishia gazeti hili kwamba klabu yake imemalizana na Simba na
kumruhusu Maguli kuanza maisha mapya.
“Natangaza rasmi kwamba Maguli sasa ni mali ya
Simba baada ya taratibu zote kufuatwa kwetu hatuna kingine cha kusema
zaidi ya kumtakiwa kila la kheri.”
Kwizera aahidi mataji Simba
Kiungo Mrundi, Pierre Kwizera (23) ametua nchini
jana saa nane mchana akitokea Ivory Coast katika klabu ya Afad na
kuwaahidi mashabiki wa Simba kuwa amekuja kuleta ubingwa.
Kiungo huyo alisema, “Nimekuja kuwapa ubingwa
Simba na kazi yangu kubwa ni kuhakikisha ushindi unapatikana na timu
kupata mafanikio.
“Mimi ni kiungo mkabaji, lakini nakuja na kitu cha tofauti
ambacho ni kuwa nina uwezo wa kucheza mipira mirefu na pia kufunga kwa
faulo. Kwa sasa ninachooomba ni ushirikiano ili niweze kuzoea mazingira.
Nataka kucheza Simba kwa mafanikio na kwa kuangalia mafanikio ya timu
zaidi,” alisema Kwizera.
Ujio wa kiungo huyo kwenye kikosi cha Simba,
unakamilisha nafasi za wachezaji wa kigeni kwenye klabu hiyo ambayo
inatakiwa kuwa tano.
Wachezaji wengine wa kimataifa waliopo Simba ni
Amisi Tambwe (Burundi), Paul Kiongera (Kenya), Donald Musoti (Kenya )
na Joseph Owino (Uganda).
Post a Comment