Sera ya uzazi wa mpango ya China, maarufu kama sera ya mtoto mmoja, ni
sera inayofahamika sana duniani kwanza kutokana na ufanisi wake katika
kudhibiti ongezeko la idadi ya watu, na pili kutokana na kupata upinzani
mkali kutoka kwa baadhi ya taasisi za kidini nje ya China. Lakini
pamoja na sera hiyo kufahamika kutokana na sababu hizo mbili, bado watu
walio nje ya China wana uelewa mdogo sana kuhusu undani wa sera hii, na
hawajui inatekelezwa vipi, ina manufaa gani na changamoto gani, na nini
tunaweza kujifunza kutokana na sera hii.
Sera ya uzazi wa mpango ya China ilianza kutekelezwa miaka 70 karne
iliyopita, ili kudhibiti ongezeko la kasi la idadi ya watu. Kimsingi
sera hii inawataka kila wanandoa wachina wawe na mtoto mmoja. Nimeamua
kutumia neno “kimsingi” kwa kuwa si wanandoa wote wanaotakiwa au
wanaolazimishwa kuwa na mtoto mmoja kama baadhi ya watu wanavyoambiwa na
kuamini.
Sera hii kwanza inawalenga watu wa kabila kubwa zaidi la China, yaani
wa-Han, ambao wanachukua zaidi ya 95 ya idadi ya watu wote wa China.
Watu wa makabila mengine ambayo nchini China yanaitwa makabila madogo
madogo wanaweza kutekeleza sera hiyo kwa hiari, na baadhi yao hata
wanapewa ruzuku kutokana na kufuata sera hiyo kwa hiari. Hata hao wa-han
si wote wanaotakiwa kutekeleza sera hiyo kama sera inavyoelezwa, kuna
wakati baadhi hawabanwi sana na sera hiyo.
Kwa mfano, wa-han wachina wanaoishi vijijini wanaotegemea shughuli za
kilimo, sera hii haiwabani sana kwa kuwa wanahitaji nguvu zaidi, kwa
hiyo wanaweza kuwa na mtoto zaidi ya mmoja. Wa-han wa mijini ambao wote
ni mtoto pekee kwenye familia zao, wakioana wanaruhusiwa kuwa na watoto
wawili. Wa-han wanaobanwa na sera hii wakienda kinyume wanatozwa faini.
Kwa hiyo ukiangalia vizuri unaweza kuona kuwa, kwa wachina wa kabila la
wa-han sera hii ni kama sheria, lakini kwa wachina wa makabila mengine
ni sera ambayo utekelezaji wake ni hiari.
Hebu kwanza tutupie macho hali nchini China katika miaka ya 1970 wakati
ilipoamua kutekeleza sera ya uzazi wa mpango. Jamhuri ya watu wa China
ilianzishwa mwaka 1949 baada ya mapigano na vita vilivyodumu kwa karibu
miaka 100 nchini China. Mwaka 1949 idadi ya wachina ilikuwa milioni 550,
na kwa wastani watu waliokuwa wanaishi miaka 35. Lakini hadi kufikia
mwaka 1980, idadi ya watu wa China iliongezeka na kufikia bilioni 1 na
umri wa wastani wa maisha ya mchina pia uliongezeka na kufikia miaka 68.
Kutokana na makadirio yaliyofanyika mwaka 1980, idadi ya watu wa China
ingeweza kufikia bilioni 1.4 hadi ifikapo mwaka 2000.
Ukiangalia sababu nyingi zilizowafanya wachina waanze kutekeleza sera
hii, unaweza kuona kuwa kuna mazingira mengi yanayofanana na hali ya
sasa ya Tanzania. Idadi kubwa ya watu ni shinikizo kubwa sana kwa
maliasili na raslimali za jamii kama vile ardhi, maji, chakula, shule,
hospitali na miundo mbinu mingine. Mwanzoni mwa miaka ya sabini
changamoto hizo zilikuwa ni mzigo mkubwa sana kwa wachina, na ni
changamoto hizo hizo ambazo kwa sasa sisi watanzania tunalalamika nazo
kila kukicha. Lakini changamoto hizo hazipo kwa Tanzania peke yake, bali
pia zipo katika maeneo mengine duniani, ambako maliasili zinaendelea
kupungua.
Nchini China watu walijua kuwa kama wakiendelea kuzaliana kwa wingi,
basi ingekuwa ndoto au ingechukua muda mrefu kuwa na ongezeko la uchumi,
na hata kama kungekuwa na ongezeko lolote la uchumi, ongezeko hilo
lingefutwa na ongezeko la idadi ya watu. Kwa sasa hapa Tanzania tunasema
kasi ya uchumi wa nchi yetu inaongezeka kwa asilimia zaidi ya 5 na 6
hivi. Hii kwa kweli ni habari nzuri, lakini ongezeko hilo halionekani
kwenye maisha ya mtanzania wa kawaida, inawezekana kuwa ongezeko hilo
linafutwa na ongezeko la idadi ya watu.
Hata tukiangalia familia moja moja, ni wazi kuwa ukiwa na watoto wengi
kuliko uwezo wako wa kuwamudu, kwanza kama mzazi utatumia muda mwingi
kujaribu kuwatunza watoto wako, na pili unaweza kukosa muda wa kutosha
kutumia akili zako na nguvu zako kufanya mambo mengine yanayoweza
kukunufaisha wewe na kulinufaisha taifa.
Mbali na maelezo yanayotolewa na serikali ya China kuhusiana na manufaa
ya kiuchumi yanayotokana na utekelezaji wa sera hii, ukiwauliza wachina
wa kawaida hasa wa mijini, wanakwambia kuwa hata kama isingekuwa sera
ya serikali, wengi wao wanalazimika kutekeleza sera hiyo kutokana na
mazingira ya sasa ya kiuchumi. Si rahisi kumudu kununua nyumba ya
kuwatunza watoto watano, si rahisi kununua chakula cha kuwalisha watoto
wengi namna hiyo, na zaidi ni vigumu sana kumudu gharama za elimu,
matibabu na huduma nyingine kwa ajili ya watoto. Kwa ufupi ni kwamba,
kuwa na idadi kubwa ya watoto, kwa mazingira ya nchi kama China, hasa
mijini, ni kujiletea matatizo makubwa.
Hata hivyo sera yoyote lazima iendane na hali halisi. Katika miaka ya
hivi karibuni, kutokana na ongezeko la uchumi na kuinuka kwa kiwango cha
maisha, wachina hasa wakazi wa mijini katika maeneo yaliyoendelea
kiuchumi, wanandoa vijana wanaonesha nia ya kuahirisha umri wa kuzaa
mtoto, na baadhi yao kuamua kutooana au kutozaa.
Kwa upande mwingine wazee wanaishi kwa muda mrefu zaidi, hali ambayo
inafanya kuwe na wazee wengi katika jamii ya China. Ndiyo maana pamoja
na kuendelea na juhudi za kudhibiti ongezeko la kasi la idadi ya watu,
serikali ya China imeanza kufikiria na kuchukua hatua ya kurekebisha
sera yake ya uzazi wa mpango. Hatua moja ni kwamba, wanandoa ambao wao
ni mtoto pekee kwenye familia, wanaruhusiwa kuwa na watoto wawili. Na
serikali pia ilichagua baadhi ya maeneo kufanya jaribio la watoto
wawili, lakini watu wengi waishio maeneo hayo hawapendi kuzaa mtoto
zaidi ya mmoja, tofauti na ilivyodhaniwa. Kuna wachina wengi tu ambao
wanaamua kuoana na kutozaa, labda kutokana na utamaduni wa sisi waafrika
jambo hili halifikiriki.
Pamoja na kuwa sera hii imeshambuliwa na jumuiya za haki za binadamu
duniani na taasisi za kidini, hasa kutokana na kuongezeka kwa vitendo
vya utoaji mimba hasa inapojulikana kuwa ni mtoto wa kike, na kutokana
na kinachotajwa kuwa ni kuzuia uhuru wa mtu kuamua idadi ya watoto
anaotaka, lakini tukiangalia lengo la kimsingi la uwepo wa sera
hii—kulinganisha matokeo ya uzalishaji wa mtu mmoja moja na thamani ya
uzalishaji wa mali na maendeleo ya uchumi na jamii kwa ujumla, tunaweza
kusema sera hii kimsingi imekuwa na manufaa kwa mtu mmoja mmoja, familia
na nchi kwa ujumla.
Inakadiriwa kuwa sera hii imepunguza ongezeko la idadi ya watu kwa watu
milioni 400, maana yake ni kuwa maliasili na rasilimali ambazo
zingetumika kwa ajili ya watu hao milioni 400, sasa zinatumika kuboresha
maisha ya watu waliopo sasa. Afya ya kina mama wanaojifungua na huduma
wanazopata wakati wa kujifungua vyote vimeboreshwa, na kutokana na
kutokuwa wajawazito mara kwa mara, kina mama wanashiriki zaidi kwenye
shughuli za uchumi, na hata watoto wanakuwa na afya zaidi, mazingira
mazuri zaidi ya elimu na hata kuwa na mustakbali mzuri zaidi.
Tanzania tumewahi kuwa na kampeni kubwa iliyokuwa inatoa mafunzo mazuri
sana kuhusu afya ya uzazi na hata manufaa yake kwa mlengwa,
ikishirikisha taasisi zisizo za kiserikali. Pamoja umuhimu wake, kampeni
hiyo ilikosolewa na baadhi ya taasisi za kidini, lakini ilionesha
mwelekeo mzuri. Sijui kwa sasa Chama Cha Uzazi wa Mpango na Malezi bora
UMATI kilichokuwa kinahimiza kampeni hiyo kinachukuliwa vipi, kina
mwelekeo gani na kina uwezo gani wa kuhimiza upangaji wa sera za taifa
kwenye mambo ya uzazi na kusimamia utekelezaji wake. Kama Chama hiki
kikipewa msukomo zaidi wa kufanya kazi na kuwafikia watanzania wengi,
kuna uwezekano kuwa chama hiki kitakuwa ni jibu la tatizo la ongezeko la
idadi ya watu Tanzania. Kwa kuwa chama hiki kinajua vizuri mazingira ya
watanzania kiuchumi, kidini na hata mienendo ya uzazi ya watanzania.
Hapa Tanzania changamoto ya idadi ya watu, haitazamwi kwa umakini
unaostahili. Pamoja na kuwa kuna baadhi ya watu wanazungumza suala hilo,
inaonekana kuwa lipo vinywani tu. Bado baadhi yetu tunaamua tu kuzaa
kwa kuwa tumefikisha umri fulani, sio kwa kuwa kweli tunahitaji kuwa na
watoto, uwezo wa kukabiliana na majukumu ya kuwa na mtoto au sisi
wenyewe kuwa wazazi, au tunaiga mkumbo na kuchagua kuwa na idadi ya
watoto tunaopenda kuwa nao bila kuzingatia kama tuna uwezo wa kuwatunza
na kuwawezesha waishi maisha bora, na baadhi tunachukulia fahari na
kuona ni jambo la kawaida kuwa na watoto nje ya ndoa, kuwatelekeza na
kuwafanya wengine wawe watoto wa mitaani. Ni kawaida kuona mtu ana
watoto watano, lakini kimsingi hana hata uwezo wa kiuchumi wa kumudu
kumtunza mtoto mmoja, lakini ukiuliza ni kwanini ana watoto wengi,
huwezi kupata jibu la maana, zaidi ya kusema Mungu atawaangalia.
Sera ya mtoto mmoja ya China ina dosari zake, na wachina wenyewe
wanajua dosari hizo, na kwa sasa kuna mjadala unaoendelea kuhusu
kuifanyia mabadiliko sera hiyo ili iendane na mazingira ya sasa. Siwezi
kusema kuwa sera hiyo inafaa kwa Tanzania au la, kwa kuwa kuna mambo
mengi yanaoendana na sera hiyo ambayo yako kinyume kabisa na maadili,
utamaduni na mazingira ya Tanzania. Lakini pia kuna mambo mengi yaliyomo
kwenye sera hiyo, ikiwa ni pamoja na mantiki ya sera yenyewe,
yanayoweza kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania na watanzania.
Ni bora kuwepo na sera ya maana inayotekelezwa na kulalamikwa, kuliko
kutokuwa kabisa na sera au kuwa sera midomoni na kwenye makaratasi tu,
na kuacha ongezeko la idadi ya watu liendelee kuwa bomu linalokaribia
kulipuka.
Tunachotakiwa kukumbuka ni kuwa, sera inayohusu idadi ya watu ni sera
muhimu kwa taifa inayopaswa kupangwa kwa uangalifu sana tangu mwanzo,
kwani athari au manufaa yake hayaonekani mara moja, lakini hakika sera
ya namna hiyo inaweza kuwa na manufaa kwa taifa pamoja na mwananchi
mmoja mmoja baada ya miaka 10 hadi 20, wakati watu wa kizazi kimoja
watakapokuwa wamekua, kuingia kwenye soko la ajira na kutaka maisha
bora.