wasaniii Tanzania
Tasnia ya sanaa imekua, ukiachana na sanaa kama kivutio, kuna
jingine kubwa na la msingi la sanaa kutengeneza ajira nyingi hasa kwa
vijana na hapo hapo mtazamo wa sanaa umegeuka kuwa biashara.
Hili ni jambo la kushukuru sana kwa sababu sanaa
inachangia kodi serikalini, hivyo kuwa moja ya vyanzo vinavyochangia
maendeleo ya nchi, lakini wakati huohuo inaisaidia Serikali kupunguza
tatizo la ajira kwa vijana.
Kusema ukweli kuna haja ya Serikali kuiangalia
tasnia ya sanaa kwa jicho la pili ili kuiwezesha kupiga hatua, kwani
imeshaonesha dhahiri jinsi ambavyo inaweza kushiriki kikamilifu katika
kuchangia maendeleo ya nchi.
Sasa katika kuliangalia hilo kwa umakini kuna
matatizo tayari yameshaanza kujitokeza miongoni mwa washika dau wa
sanaa, na kama ulikuwa huwajui washika dau hao ni wasanii wenyewe na
vyombo vya habari.
Unajua baada ya sanaa kukamilika, inahitaji mkono
wa chombo cha habari ili iweze kutambulika kwa jamii. Hii ndiyo sababu
washika dau hawa wawili wamekuwa mhimili mkubwa wa maendeleo ya sanaa
nchini, kwa jinsi wanavyotegemeana katika kuendeleza.
Tatizo lililopo sasa, ni wadau hawa kuanza
kuchukua upande katika mivutano inayoendelea nchini huku wadau wakiona
dhahiri, jambo ambalo kwa majukumu waliyonayo, siyo sahihi.
Msanii ili awe mahiri, anatakiwa kuwa na mashabiki
wengi na mara nyingi mashabiki hao huwa na imani tofauti za kidini na
kisiasa na hutofautiana misimamo. Lakini wote hawa wanakuja kukutana
kwenye sanaa baada ya kukubaliana na kazi za huyu msanii.
Hapo ndipo imani za kidini, kisiasa na nyinginezo
huwekwa pembeni, watu wakakaa meza moja, kucheza muziki, ama kuangalia
mavazi na wakati mwingine hata kuangalia sinema pamoja, huku wakiamini
kwamba huyu msanii ni kwa ajili ya jamii nzima.
Lakini inapofikia mahali msanii huyu akaonyesha
dhahiri imani yake katika siasa, ama dini na kuweka misimamo ya kuchukua
upande fulani ndipo sanaa yake inapoanza kuingia doa kwani mashabiki
ambao hayuko nao kwenye imani moja, lazima watagoma kukubaliana naye.
hapa ndipo wengi wanapoanza kupoteza mashabik na
kuanza kuhisi pengine wanahujumiwa kumbe moto wameukoka wenyewe, kuukoka
wanahisi utawaunguza.
Kila mwenye imani yake ataondoka na kurudi kule ambako anahisi kunamfaa, hali kadhalika na wanahabari wanayo changamoto hii.
Katika uandishi na utangazaji siyo vyema
tukaonyesha dhahiri kwamba tumesimama kwa huyu, nasi pia tunasikilizwa
na kusomwa na watu wa kila aina katika jamii.
Hata siku moja kuripoti kwetu hakutakiwi kusimama kwenye kutetea
upande fulani. Tusimame kwenye kuipeleka taarifa kama ilivyo na
kuichambua bila kulalia upande mmoja, mwishowe uamuzi tuwaachie
wanajamii wenyewe waamue.
Ndugu zetu wanahabari iwapo mmejisahau,
tunawakumbusha kwamba haya ni mambo ambayo mlifundishwa wakati mko
vyuoni, kuhusiana na kusimama katikati ya jamii na kuripoti kilicho sawa
na siyo kuweka misimamo yenu kwenye majukwaa mliyopewa.
Tunawatakia Jumamosi njema.
Post a Comment