Wachezaji wa timu ya Yanga wakiwa mazoezini wakiwemo pia raia wawili kutoka nchini Brazil. Picha na Doris Maliyaga
Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Marcio Maximo amewatetea nyota
wake wawili kutoka Brazil, Andrey Coutinho, Santos Santana ‘Jaja’ kwa
kusema ni wachezaji wazuri, na kama mnataka taarifa zao nendeni kwenye
mtandao wa You Tube, mtaziona.
Kauli ya Maximo imekuja wakati wadau wa soka
hususani mashabiki watani zao wa jadi Simba kubeza kuwa hakuna mchezaji
mzuri kutoka Brazil akaja kucheza soka Tanzania ambayo soka bado
linajikongoja.
Maximo alisema “Brazil kuna timu nyingi sana, na
sio kila timu iliyopo kule ni kubwa, kuna nyingine zipo kama Coastal
Union, naitolea mfano Coastal kwa vile naifahamu, na kule mpira
unachezwa kwenye majimbo tofauti tofauti, kwa hiyo wasibeze ujio wao
huku wakadhani ni wachezaji wabovu. “Wabrazili wengi wanaenda kucheza
soka Angola, Angola wanaenda Brazil hata wachezaji wa Tanzania
wanatakiwa kutoka kwenda kucheza soka Brazil, kama ambavyo Wakenya na
Waganda wanakuja kucheza soka hapa Tanzania hivyo hivyo wachezaji wa
hapa walitakiwa kwenda kule, lugha ya mpira inayoongelewa ni moja
duniani hakuna tofauti.”
Pia, Maximo amewatema rasmi kwenye kikosi chake wachezaji Reliant Lusajo na Abuu Ubwa ambao awali aliwarudisha kundini.
Alisema kuwa aliamua kuwaita ili angalie uwezo wao
kwa vile aliwafahamu viwango vyao miaka minne iliyopita, alitegemea
vingekuwa vimepanda, lakini vimeporomoka.
“Nimeamua kuwaacha ili wakajipange upya, nisije
nikawashikilia alafu baadae wakakosa timu za kuchezea, nimewachia waende
kusaka timu wapandishe viwango vyao, Thabit Abdul amenivutia kiwango
chake, kuna wachezaji chipukizi niliowaacha naona wanaendelea vizuri
kama Omega Seme, nilitegemea Ubwa na Lusajo nao wangekuwa kwenye kiwango
hicho, lakini bahati mbaya.” alisema kwa masikitiko Maximo.
Post a Comment