Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Daudi Ballali
Dar na Marekani. Wakati kukiwa na uthibitisho kwamba Gavana wa
zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali alifariki dunia na
kuzikwa miaka sita iliyopita, kitendawili kilichobaki ni sababu za
ugonjwa na baadaye kifo chake.
Wanafamilia wote waliozungumza na mwandishi wa
gazeti hili tangu uchunguzi huu ulipoanza Julai 2012, hakuna aliyekuwa
tayari kueleza sababu za kifo chake na wote waliohojiwa wanasema
anayefahamu matokeo ya vipimo vya madaktari ni mkewe, Mama Anna Muganda.
Wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kuwa na taarifa
za sababu za kifo cha Gavana huyo kilichotokewa Mei 16, 2008 nyumbani
kwake Washington DC ni mtalaka wake, Malva Ballali na watoto wake;
Octavio Ballali na Rahel Ballali.
Kwa muda mrefu gazeti hili lilijitahidi kutumia
njia mbalimbali kumtafuta Mama Muganda, lakini jitihada hizo
hazikufanikiwa na taarifa kutoka kwa ndugu zake wa karibu zinasema
hayuko tayari kwa namna yoyote kuzungumzia suala hilo.
Kwa jinsi hali ilivyo siyo tu kwamba imekuwa
vigumu kwa Mama Muganda kuzungumzia suala hilo, ila hata upatikanaji
wake kwa kukutana naye ana kwa ana au kupata mawasiliano yake yawe ya
baruapepe au namba za simu yalishindikana.
Wakati mwandishi wa gazeti hili alipokwenda
Marekani, aliambiwa kwamba mwanamama huyo aliyekuwa mshauri wa kwanza wa
masuala ya uchumi enzi za uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, alikuwa
nchini Tanzania kumuuguza dada yake ambaye baadaye alifariki dunia na
kuzikwa Mugumu, Serengeti mkoani Mara.
Baada ya kurejea Dar es Salaam kutoka Mara, kati
ya Julai 8 na juzi, gazeti hili lilimtafuta kupitia kwa ndugu zake,
lakini jitihada hizo ziligonga mwamba na baadaye liliambiwa kwamba
ameondoka Julai 16 usiku kuelekea Marekani. Habari zinasema Mama Muganda
akiwa mshauri wa Mkapa, ndiye aliyemshauri kiongozi huyo kumchukua
Ballali kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kuongoza
BoT.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu serikalini
alisema kama Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa ilipata
mafanikio yoyote kiuchumi, basi mafanikio hayo hayawezi kutenganishwa na
Ballali na mkewe Mama Muganda waliokuwa washauri na watekelezaji wa
maboresho ya sekta hiyo.
“Kinachozungumzwa leo hii ni tuhuma tu dhidi ya
Ballali kwa sababu pengine hayupo, lakini ukweli ni kwamba kukua kwa
uchumi wakati wa uongozi wa Mkapa kunatokana na ushauri wa yule mama
(Muganda) na utekelezaji na usimamizi wa sera za kiuchumi uliofanywa na
BoT chini ya Gavana ambaye ni Ballali,” alisema ofisa huyo ambaye
aliomba jina lake lihifadhiwe.
Kutokana na hali hiyo, Mama Muganda amekuwa kimya
kutokanana kile kinachoelezwa na ndugu zake kwamba ni ukimya wa viongozi
wa Serikali wakati wa ugonjwa wa mumewe na kunyamazia tuhuma alizopewa
Ballali wakati akiumwa na baada ya kifo chake.
Mtalaka na watoto
Hali ya kutotaka kwa namna yoyote kuzungumzia
chanzo cha kifo cha Ballali, pia imeonekana kwa Malva ambaye ni mke wa
kwanza wa Gavana huyo na mtoto wake, Octavio.
Kwa nyakati tofauti wakati gazeti hili likitafuta mawasiliano
nao, walisema hawakuwa na cha kusema kwa hiyo wasingependa simu, wala
baruapepe zao zitolewe kwa mwandishi wa Mwananchi.
Katika harakati za kutaka kuzungumza na familia
hiyo, gazeti hili lilimtumia ujumbe Malva ambaye ni mzaliwa wa Argentina
kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, lakini hadi jana hakuwa amejibu
ujumbe huo, licha ya kuwa anwani yake ilionekana kufanya kazi.
Baadhi ya ndugu walioko Tanzania kwa upande wao
walisema hawafahamu chanzo cha kifo chake na kwamba taarifa walizopewa
zilihusu ugonjwa na baadaye kifo.
“Kwamba kilichomuua ni nini, kwakweli sijawahi
kufahamu pengine mke wake anafahamu, mimi sijawahi kuambiwa na hata
ndugu zetu wengine hawajui kilichomuua,” alisema Margaret Mpango ambaye
ni dada mdogo wa Ballali.
Kauli yake inafanana na ile ya Paschal Ballali
ambaye pia ni mdogo wa marehemu ambaye alisema: “Kwa kweli hatujawahi
kuambiwa kwamba tatizo lilikuwa nini, tulipewa taarifa kwamba anaumwa na
mara amezidiwa na baadaye taarifa za kifo.”
Wiki iliyopita Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu
alisema wakati akienda Marekani Agosti 2007, Ballali alikuwa mgonjwa,
lakini akasisitiza kwamba wanaoweza kueleza tatizo lake ni familia.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue katika
mazungumzo yake na gazeti hili wiki jana alisema Ballali alikuwa
mgonjwa, lakini naye akasema familia yake pekee ndiyo inayoweza kutoa
taarifa kuhusu ugonjwa wake.
Inaendelea kesho...
Post a Comment