Dodoma. Ligi Daraja la Kwanza ya netiboli inafikia ukingoni huku
timu za Uhamiaji na JKT Mbweni zikishinda mechi zake walizocheza jana
na juzi jioni na Polisi Kigoma na Polisi Shinyanga wakionekana kuvurunda
kwenye ligi hiyo kutokana na kupoteza tena michezo yake.
Katika mchezo uliochezwa juzi, Uhamiaji iliwafunga
Polisi Kigoma kwa mabao 46-9, JKT Mbweni ikashinda 36-13 dhidi ya
Polisi Dodoma na kila mmoja kujiwekea matumaini ya kutwaa ubingwa wa
michunao hiyo.
Mechi nyingine, TTPL iliwachapa vibonde wa ligi
hiyo, Polisi Shinyanga kwa magoli 38-9, Polisi Morogoro ikatoa kipigo
kwa ndugu zao wa Polisi Dodoma kwa magoli 20-17, Jeshi Stars
ikaichabanga 37-21 Polisi Arusha na CIDT ikashinda kwa 18-29 dhidi ya
CMTU.
JKT Ruvu walifanikiwa kuibuka na ushindi mbele ya
Polisi Dar es Salaam wa magoli 37-21, JKT Mbweni ikawachapa tena Mbeya
City 40-23, ambapo Polisi Mwanza ikawanyukwa na Polisi Dar es Salaam kwa
magoli 23-18, huku JKT Ruvu wakiwagaragaza Polisi Shinyanga 47-3.
Hadi sasa michuano hiyo inaonekana kuwa mizuri kwa
timu za Uhamiaji na JKT Mbweni, ambao wameonyesha kiwango kikubwa
katika ligi hiyo, ambapo timu hizo zimepewa nafasi ya mmoja wapo
kunyakua ubingwa wa mashindano hayo.
Kocha wa Uhamiaji, Winfrida Emmanuel alisema kasi
waliyoianza haitaisha hadi mechi ya mwisho na hakuna timu ambayo inaweza
kukwamisha, na kwa sasa mipango yake ya kunyakuwa ubingwa wa netiboli
nchini inatimia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli
Tanzania (Chaneta), Anna Kibira alisema michuano ya mwaka huu imekuwa na
ushindani mkubwa kutokana na viwango vikubwa vilivyoonyeshwa na timu
shiriki haswa kutokana na kuwepo kwa vipaji vingi.
Post a Comment