0
Dar es Salaam. Wakati msafara wa Tanzania ukiwasili kwenye kijiji cha michezo tayari kwa michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Scotland, kocha mkuu wa timu ya taifa ya judo, Zaid Hamis ametoa kali baada ya kueleza kuwa medali ya timu yake imebaki Tanzania.
Zaid aliyeambatana na wanajudo watatu kwenye michezo ya Madola itakayofunguliwa Jumatano ijao kwenye Uwanja wa Celtic Park jijini Glasgow, alisema: “Tegemeo langu kubwa la medali lilikuwa kwa Ahmed Magogo, ambaye ameachwa Tanzania, hivyo medali ya judo imeachwa nyumbani.”
Kocha huyo alisema anaamini Magogo ndiye angeiletea nchi medali ya judo lakini kuondoshwa kwake siku moja kabla ya safari kumemvunja moyo yeye pamoja na wanajudo wengine wanaoshiriki kwenye michezo hiyo.
“Hii itanipa wakati mgumu kuwarudisha kwenye hali ya kawaida wachezaji wengine, Magogo alikuwa bora zaidi,nilitegemea medali ya Madola kutoka kwake, kama ningepata mbili basi moja ingekuwa yake,” alisema kocha huyo.
Magogo alikuwa miongoni mwa wanajudo watatu walioachwa baada ya taarifa zao kutoonekana kwenye Shirikisho la Jumuiya ya Madola (CGF) nchini Scotland saa chache kabla ya ujumbe wa Tanzania kwenye michezo hiyo kuondoka nchini, wachezaji wengine waliokumbwa na dhahama hiyo ni Gervas Chilipweli na Amour Kombo.
Wakati huo huo, Katibu mkuu na Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi na Gulam Rashid wanaondoka mchana huu kwenda Scotland kwenye mkutano mkuu wa CGF.
Kwa mujibu wa Bayi, mkutano huo utafanyika Jumatatu na Jumamnne kabla ya kushiriki sherehe za ufunguzi wa michezo ya Madola, ambapo Tanzania inawakilishwa na wanamichezo 44 wa judo, riadha, ngumi, kuogelea, mpira wa meza, kunyanyua vitu vizito na baiskeli, huku Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Michezo, Juma Nkamia wakitarajiwa kujumuika nao nchini humo.

Post a Comment

 
Top