0

Msajili, Jaji Francis Mutungi.PICHA|MAKTABA  


Tumesikitishwa na mgogoro kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kiasi cha viongozi wake kudai ofisi hiyo inatumiwa na wasaliti wa chama hicho kutaka kukivuruga. Kiini cha malalamiko ya viongozi hao ni kauli iliyotolewa juzi na Msaidizi wa Msajili, Sistyl Nyahoza kwamba mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa hawana sifa ya kugombea uongozi kutokana na kuzuiwa na katiba ya chama hicho.
Msaidizi huyo wa Msajili alidai kwamba kipengele cha ukomo wa mgombea katika Katiba ya Chadema ya mwaka 2006 kiliondolewa kinyemela bila idhini ya mkutano mkuu, huku akisisitiza kuwa, Katiba ya Chadema ya mwaka 2004 ilikuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka wa vipindi viwili vya miaka mitano. Kutokana na kauli hiyo, chama hicho kimemtaka Msajili, Jaji Francis Mutungi kujitokeza na kueleza iwapo yeye ndiye alimtuma msaidizi wake kutoa kauli hiyo.
Tunaposema tumesikitishwa na hali hiyo tuna maana kwamba mgogoro huo ni mkubwa, ingawa baadhi ya watu wanaweza kudhani unafaa kupuuzwa. Lakini yeyote ambaye amekuwa akifuatilia mwenendo wa ofisi hiyo ya msajili tangu ilipoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 5 ya mwaka 1992 atagundua kwamba, migogoro mingi iliyotokea katika baadhi ya vyama vya upinzani na kuvivuruga, kwa kiasi kikubwa ilitokana na ofisi hiyo kuwa sehemu ya migogoro kwa kuendesha shughuli zake kisiasa.
Sisi tulidhani kwamba uzoefu wa miaka 22 ya kuwapo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ungetosha kwa mamlaka husika kuhakikisha ofisi hiyo inakuwa mlezi wa kweli wa vyama vya siasa nchini. Tofauti na mazingira ya kazi ya msajili aliyepo hivi sasa, mazingira ya kazi ya wenzake waliomtangulia yalikuwa magumu mno kiasi cha wananchi wengi kujenga dhana kwamba walikuwa mawakala wa chama tawala. Hivi sasa dhana ya demokrasia na utawala bora imekubalika kwa kiasi kikubwa.
Hivyo, hatuoni kikwazo kinachoweza kumzuia msajili wa vyama hivi sasa asifanye kazi kwa kujiamini na kutenda haki, kwa maana ya kusimama kama mlezi na kutumia busara kufanya uamuzi kama kiongozi wa vyama vyote vya siasa. Unahitajika umakini mkubwa kwa upande wa msajili kutatua migogoro ndani ya vyama pasipo kuvuka mipaka yake, kwani kinyume chake ni kuichochea. Hata hivyo, hatuna maana kwamba msajili asihusike katika utatuzi wa migogoro. Tunachosema ni kwamba ni muhimu kwake kwanza kufanya uchunguzi jadidi ili kufahamu ukweli kuhusu pande zote zinazokinzana. Kukurupuka na kutoa hukumu kwa kusimamia hoja za upande mmoja, tena kupitia kwenye vyombo vya habari ni kukuza tatizo.
Katika hili la Chadema, Msajili pia alipaswa kusikiliza hoja za chama hicho kinachosema mwaka 2006 Katiba ya chama hicho haikurekebishwa, bali iliundwa upya. Hoja ya Chadema kwamba mabadiliko hayo siyo tu yaliridhiwa na mkutano mkuu Agosti 13, 2006 bali pia yalipewa baraka na msajili aliyemtangulia, John Tendwa ni hoja nzito ambayo ilipaswa kufanyiwa kazi ipasavyo. Pamoja na kwamba sisi hatuna masilahi yoyote na upande wowote katika sakata hili, tungependa kuweka wazi kwamba matamanio yetu pekee ni kuona mfumo wa vyama vingi ukifanikiwa badala ya kuwa kiinimacho.

Post a Comment

 
Top