0

 
Na Zitto Kabwe, Mwananchi

Kwa mara nyingine Serikali kupitia viongozi na watendaji wake, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola 250 milioni za Kimarekani zilizopaswa kuendelea kuwapo kwenye ‘Tegeta Escrow Account’ si mali ya Serikali na hivyo si mali ya umma.
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited (IPTL).
Kwa bahati mbaya sana viongozi wa Serikali wamekuwa wakiendelea kurudia kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya umma.
Inasikitisha pia kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza huo uongo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia asasi za kiraia nazo zimekaa kimya. Inatisha na kushangaza kuona wapinzani wakimwachia suala hili mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, pekee wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya wapinzani.
Kafulila amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke yake bila kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka kwa wenzake wa kambi ya upinzani bungeni.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi maalumu kwenye akaunti hiyo ya escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma.
PAC haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka 2009 iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.
Akaunti ya ‘Tegeta Escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa Tanesco.
Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.
Kwa uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo maalumu zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2012 za Tanesco, zinaonyesha wazi kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
Fedha za kampuni ni suala la kisheria kama inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa maelezo hayo na hoja hizo, inakuwaje Serikali ianze kudai kwamba fedha hizo siyo mali ya umma?
Hivi inawezekanaje fedha za mtu binafsi zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma?
Serikali inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo siyo mali ya umma. Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa sasa wa ‘Tegeta Escrow Account’.
Fedha zinazohusiana na akaunti ya escrow ni Dola 250 milioni za Kimarekani, kati ya hizo Dola 122 milioni zilizokuwa BoT zimeshatolewa na kiasi kilichosalia Dola 128 milioni zitalipwa na Tanesco kutokana na fedha zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati.
Zitto Kabwe ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Post a Comment

 
Top