Utafiti uliofanywa katika sekta ya madini unaonyesha Tanzania
ina aina 30 za madini. Ramani mpya ya madini kutoka wizara ya nishati na
madini inaonyesha kuwa kila wilaya hapa nchini inakadiriwa kuwa na aina
30 za madini.
Hata hivyo, hali ya uchumi wa Tanzania na hali
halisi ya maisha haifanani na watu wanaoishi katika nchi yenye madini na
raslimali nyingi adimu kama vile madini ya dhahabu, almasi na
tanzanite.
Aidha, miaka ya karibuni imegundulika uwepo mafuta
na gesi, sekta ambazo zinaweza kuleta mapinduzi ya uchumi kwa
Watanzania endapo viongozi watasimamia rasilimali hizo kwa uzalendo.
Maliasili tulizonazo za madini, gesi na mafuta
iwapo hazitasaidia kutatua matatizo mbalimbali ya huduma za kijamii kama
afya, elimu umeme na barabara bora ni sawa na nchi kuwa na laana kwa
kuwa rasilimali zilizopo zikisimamiwa kikamilifu zinaweza kuleta
maendeleo endelevu kwa Watanzania.
Bila kuwepo usimamizi madhubuti katika sekta ya
madini, gesi na mafuta, wawekezaji wanaweza kumaliza madini yote na nchi
itaendelea kubakia katika umasikini na kwamba madini yanaweza kubakia
historia kwa vizazi vijavyo kwamba Tanzania ilikuwa na madini,
yamekwisha bila kuwa na manufaa kwa nchi.
Ukiachia madini hayo, gesi asilia iligundulika kwa
mara ya kwanza hapa nchini mwaka 1974 katika kisiwa cha Songosongo
mkoani Lindi.
Ugunduzi wa gesi asilia umekuwa unaendelea katika
eneo la bahari na inafikia takriban futi za ujazo trilioni 51. Pia kwa
mujibu taarifa ya Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kuna
uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa mafuta katika maeneo mbalimbali
nchini yakiwemo baharini na nchi kavu kwenye bonde ufa kama vile Ziwa
Rukwa, Kyela na Bonde la Ruhuhu pamoja na maeneo mengine.
Tanzania inaweza kujifunza kutoka nchi jirani ya
Uganda ambayo iligundua mafuta mwaka 2006 katika eneo la nchi kavu la
Ziwa Albert ambalo ni mpakani mwa nchi hiyo na Kongo DRC .
Tangu kugundulika kwa mafuta hayo, Serikali ya
Uganda imekuwa inafanya maandalizi ya kutosha na mwaka 2008 iliandaa
sera, kanuni na kutunga sheria ya mafuta. Huduma za kijamii katika
maeneo yaliyogundulika mafuta zimeanza kuboreshwa, hivi sasa kiwanda cha
kusafishia mafuta kinajengwa katika wilaya ya Hoima ambayo mafuta
yamegundilika.
Sekta binafsi katika nchi hiyo zimeshirikishwa na
tayari wakulima 6,000 katika vijiji vilivyogundulika mafuta wamepata
mafunzo maalum ya kuzalisha mboga na mifugo ya kisasa, ufundi na mafunzo
ya ujasiriamali hata kabla ya uzalishaji wa mafuta safi kuanza.
Dennis Kamurasi, makamu mwenyekiti wa huduma ya
jamii ya gesi na mafuta nchini Uganda, anasema sekta ya mafuta
inatarajia kutoa ajira rasmi kwa watu 150,000 na ajira ambazo siyo rasmi
zitakuwa zaidi ya 50,000.
Hapa Tanzania sekta binafsi zimechelewa kushiriki
kuwaandaa wananchi ambao wapo katika maeneo ambayo yamegundulika kuwa na
rasilimali kama mafuta na gesi hali ambayo imechangia kusababisha
mgogoro na wawekezaji kama ilivyotokea mkoani Mtwara, hali
iliyosababisha kutokea uvunjifu wa amani.
Wananchi hawajaandaliwa kupewa mafunzo mbalimbali kama
ilivyofanyika nchini Uganda, ili waweze kutumia fursa hiyo kujipatia
ajira ambayo sio rasmi kwa kuwa ni watu wachache tu ambao wanaweza
kupata ajira rasmi.
Sera na sheria za mafuta pamoja na mikataba katika
sekta ya madini, mafuta na gesi katika nchi ya Uganda ni ya wazi kila
mmoja anaruhusiwa kuona, tofauti na hapa nchini ambako hadi sasa licha
ya mikataba kutowekwa wazi, sheria ya gesi bado haipo licha ya mchakato
wa uzalishaji wa gesi kuendelea.
Pia Tanzania inatumia sheria ya zamani ya
utafutaji na uzalishaji wa mafuta ya mwaka 1980 ambayo iliandaliwa
wakati wa siasa ya ujamaa na sasa haiwezi kukidhi mahitaji ya soko
huria.
Bila kuweka vizuri sera, sheria za madini,
mikataba, kanuni na kodi nchi husika haiwezi kunufaika na sekta hiyo
ndiyo maana katika nchi ya Uganda licha ya mafuta kugundulika mwaka 2006
hadi sasa bado hawajaanza kuzalisha kwa sababu kwanza walimaua kuweka
sera, kanuni na sheria ndipo waanze kuzalisha.
Kuzalisha mafuta na gesi bila kufanya maandalizi
ya kutosha ni sawa na kuingia katika mashindano ya kunyonywa kwenye
sekta ya gesi na mafuta hivyo kupoteza rasilimali ya nchi na kupora
rasilimali za kizazi cha sasa na kijacho.
Albano Midelo ni mwandishi mwandamizi anayeandikia masuala ya maendeleo, madini, gesi na mafuta
Post a Comment