London, England. Kiungo nyota wa klabu ya Manchester City, Yaya
Toure amekataa ofa ya kujiunga na mahasimu wao wa mji mmoja, Manchester
United.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, Toure
anadaiwa kutokuwa na furaha katika mji wa Manchester kutokana na sababu
mbalimbali, ikiwamo klabu kushindwa kumtakia siku njema ya kuzaliwa na
pia kushindwa kumpa ruhusa wakati mdogo wao alipokuwa hospitali kabla ya
kufariki.
Inaonekana dhahiri kuwa nyota huyo wa zamani wa
Barcelona ataondoka City, lakini kujiunga na miamba ya Old Trafford si
chaguo lake.
Taarifa zinadai kwamba mabosi wa United wamekuwa
wakifuatilia kwa ukaribu suala la kuondoka kwa Toure, ambapo wameweka
mezani pauni 40 milioni kwa ajili hiyo, lakini Toure inadaiwa
ameshawaambia kuwa hatarajii kujiunga nao.
Mchezaji huyo anadaiwa kuwa ana mpango wa kuondoka
kabisa katika Ligi Kuu England, na huku mabingwa wa Ufaransa, Paris
Saint Germain, wakipewa nafasi kubwa ya kumsajili.
Toure amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha
City na kukiimarisha katika Ligi Kuu, ambapo pia alimaliza msimu
uliopita kwa kuipa City ubingwa wa ligi hiyo.
Toure ametwaa mara mbili tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kutokana na kiwango chake kizuri uwanjani.
Post a Comment