Dar es Salaam. Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij na wachezaji
wake wameahidi ushindi wa kishindo kesho dhidi ya Msumbiji huku
wakiwataka Watanzania kufika kwa wingi uwanjani kutoa sapoti.
Stars na Msumbiji zitashuka Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam katika mchezo wa kwanza wa kusaka kufuzu kucheza fainali za
Mataifa ya Afrika 2015, Morocco.
Kocha Nooij alisema wachezaji wake wote wako fiti
kwa ajili ya mchezo huo na anatambua ugumu wa mechi hiyo, lakini
amewataka watanzania kutoa sapoti kwani timu hiyo ni ya wote.
“Itakuwa moja ya mechi ngumu, lakini wachezaji
wangu wote wako tayari kwa ajili ya mchezo huo, naijua Msumbiji kwani
nimewahi kufundisha huko hivyo nafahamu mbinu zao na nimeshawaandaa
wachezaji wangu na kuwapa mbinu jinsi ya kuwadhibiti.”
Naye nahodha wa Stars, Nadir Haroub ‘Canavaro’,
alisema wamejiandaa vizuri na wamerekebisha makosa yote yaliyojitokeza
katika michezo iliyopita hasa safu ya ulinzi na kudai watahakikisha
wanalipiza kisasi na kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
“Bado nakumbuka kipigo tulichopata kutoka kwa
Msumbiji mwaka 2007 wakati Nooj akiwa kocha wa timu hiyo na sasa ni muda
wa kulipa kisasi kwa timu hiyo nikiwa chini ya kocha huyo na
nitahakikisha najituma kwa faida ya Watanzania na yangu binafsi na
nitahamasisha wenzangu kujituma zaidi ili tuweze kushinda mchezo huo,”
alisema Canavaro.
Post a Comment