Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Yanga, Marcio Maximo amesema atamka mshahara mchezaji yeyote atakayekwenda kinyume na matakwa ya timu.
Kocha huyo jana alikuwa na kikao kirefu na
wachezaji hao kabla ya kuanza kwa mazoezi ya timu hiyo, leo asubuhi
kwenye ufukwe wa Coco na jioni watafanyia kwenye uwanja wa shule ya
kimataifa ya IST Masaki.
Katika kikao hicho kilichoanza saa 2:30 asubuhi na
kumalizika saa 4 asubuhi, Maximo alisisitiza suala la ushirikiano baina
ya wachezaji na kukazia suala la nidhamu.
Maximo amewapa onyo wachezaji wote wa klabu hiyo
kuwa atakayeonyesha utovu wa nidhamu atakatwa mshahara na hatakuwa na
simile na mchezaji wa namna hiyo kwani anasimamia falsafa yake kubwa ya
kila mchezaji kujitolea kwa ajili ya timu na nidhamu nzuri.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho ambazo
Mwananchi imepata zilidai kuwa Maximo aliwasisitizia wachezaji wake
kushirikiana kwani ushirikiano ndio siri kubwa ya ushindi. “Nitakuwa
nanyi kwa kipindi hiki, lakini kubwa ninalopenda mimi ni nidhamu na
ushirikiano baina yenu, sitakuwa radhi kuona mchezaji anafanya vitu
ambavyo haviendani na matakwa ya timu na yeyote akayefanya hivyo
atakatwa mshahara.
Akimzungumzia kipa Kaseja ambaye walikuwa paka na
Panya baada ya kukorofishana wakati akiinoa Taifa Stars, Maximo alisema
sina tatizo na Kaseja, yaliyopita yamepita isitoshe hatukuwa na ugomvi,
yale yalikuwa makubaliano, bila kuweka wazi alikuwa na makubaliano gani
kati yake na kipa huyo.
“ Pia napenda kusisitiza kwenu kuwa sina ugomvi na
kipa Juma Kaseja, yale yaliyopita yamepita na ilikuwa timu ya Taifa,
lakini sasa tunaanza maisha mapya ili kuifanya timu hii itishe ndani ya
nje na kimataifa”alisema Maximo.Baada ya kumaliza kikao hicho Maximo
alimuita Kaseja na kukaa naye pembeni na kuongea mambo mawili matatu
ili kuwekana sawa.
Wakati huohuo; Kiungo wa Yanga,
Nizar Khalfan ameponea chupuchupu kuondolewa ndani ya timu hiyo, huku
kocha Marcio Maximo akitajwa kuwa ni sababu ya kumbakiza Jangwani.
Awali, Nizar alikuwa ni mmoja wa wachezaji
waliopendekezwa kutemwa na kutolewa kwa mkopo, lakini ujio wa Maximo
ukawafanya baadhi ya viongozi kufuta mawazo hayo na kumbakisha kiungo
huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Vancouver Whitecaps ya Canada.
Post a Comment