Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Balozi wa Libya nchini Tanzania,
Ismail Nwairat, amejiua kwa risasi jana ofisini kwake, katika tukio la
kwanza la aina yake nchini kwa kigogo wa ubalozi kuondoa uhai wake.
Hadi sasa haijafahamika sababu za kujiua kwa
balozi huyo ambaye alikuwa akipingana waziwazi na sera za utawala
ulioondolewa madarakani wa Kanali Muhamar Gaddafi, aliyeuawa wakati wa
mapinduzi Oktoba 2011.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zilisema kuwa Nwairat
alijifungia kwenye ofisi yake iliyopo Mtaa wa Mtitu, Barabara ya Umoja
wa Mataifa na kujifyatulia risasi upande wa kushoto wa kifuani.
Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally alisema baada
kusikia mlio wa bunduki majira ya saa 7:00 mchana, maofisa ubalozi
walivunja mlango wa ofisi hiyo na kumkuta Nwairat ameanguka chini.
“Tumepata taarifa hizo na kubaini kuwa lilikuwa ni tukio la kujiua, marehemu alikutwa na risasi moja kifuani,” alisema Ally.
Alisema baadaye walimpeleka balozi huyo Hospitali
ya AMI, Oysterbay ambako ilielezwa kuwa alikuwa ameshafariki dunia. Kwa
sasa mwili wa balozi huyo umehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) kuhifadhiwa kabla ya kusafirishwa kwenda kwao Libya.
Ally alisema hadi sasa hawajafahamu sababu za balozi huyo kujiua kwa kuwa hakuacha ujumbe wowote.
Nwairat anajulikana kwa kuwa mpinzani wa wazi wa
utawala wa Gaddafi, ambaye alikuwa kiongozi wa kijeshi wa Libya tangu
alipoingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1969.
Katika hafla ya kuadhimisha miaka mitatu ya
mapinduzi ya Libya iliyofanyika Machi 9 jijini Dar es Salaam, Balozi
Nwairat aliuelezea uongozi wa Gaddafi kuwa wa ukandamizaji, wa kiimla,
usiotumia katiba na ambao uliwanyima wananchi wake haki ya kujieleza
ndani na nje ya nchi hiyo.
Kuhusu taratibu za mazishi, Ally alisema kwa sasa
Wizara inafanya inafanya jitihada kushirikiana na wafanyakazi wa ubalozi
huo pamoja na ubalozi wa Tanzania Libya kuangalia taratibu za
kusafirisha mwili huo.
“Serikali itawapa ushirikiano wote watakaohitaji
ili kufanikisha mwili wake kusafirishwa na atapewa heshima zote za
kidiplomasia kama inavyotakiwa na kama wafanyiwavyo mabalozi wote,”
alisema.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, pamoja na kueleza kufahamu tukio hilo, alisema angetoa
maelezo ya kina leo katika mkutano maalumu na wanahabari.
“Tunazo hizo taarifa, lakini nenda kwanza kazungumze na Wizara
ya Mambo ya Nje wakueleze kinagaubaga kisha uniambie, lakini kesho (leo)
tutafanya mkutano kueleza kilichotokea,” alisema Kova.
Wafanyakazi wa ubalozi huo ambao hata hivyo
hawakutaka kujitambulisha kwa majina, walisema hawawezi kuzungumza
lolote kwa sasa hadi watakapokamilisha uchunguzi na watatoa taarifa
rasmi muda mwafaka utakapofika.
“Hatutaki kunukuliwa wala hatutazungumza chochote
hadi tutakapoamua kutoa taarifa kamili kuhusu kilichotokea,” alisema
mfanyakazi mmoja wa ubalozi bila kutaja jina lake.
Msemaji wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema mwili wa
balozi huyo ulipokelewa jana saa 5:00 usiku na kuwa maelezo ya awali
yanaonyesha kuwa alijipiga risasi.
“Tumepokea mwili huo. Upo katika chumba chetu cha
kuhifadhia maiti na bila shaka kesho (leo) atafanyiwa uchunguzi kujua
kipi kilichosababisha kifo hicho,” alisema.
Post a Comment