Mshambuliaji wa Ujerumani, Andre Schuerrle (kushoto) akifunga bao la
kwanza kwa timu yake huku kipa wa Algeria, Rais Mbohli akiruka bila
mafanikio akitazamwa na beki wake, Faouzi Ghoulam, katika mchezo wa
jana wa hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia uliopigwa kwenye Uwanja wa
Beira-Rio, mjini Porto Alegre, Brazil. Algeria ilichapwa 2-1 na kuwa
timu ya mwisho kutoka Afrika kutolewa katika fainali hizo. Picha na
AFP
Porto Alegre, Brazil. Wawakilishi wa Afrika
katika fainali za Kombe la Dunia waliokuwa wamebaki, Nigeria na Algeria
nao wametolewa katika mashindano hayo.
Katika mchezo wa mapema jana, Nigeria ilikubali
kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Ufaransa, yakifungwa na Paul Pogba na beki
Joseph Yobo akijifunga.
Algeria walifanikiwa kwenda suluhu dakika 90, lakini dakika 30 za nyongeza zilikuwa mbaya kwao baada ya kukubali mabao 2-1.
Andre Schurrle alifunga dakika ya pili ya muda wa
nyongeza kabla ya Metsuit Ozil kufunga la pili, lakini bao la kufutia
machozi la Djabou halikutosha kuwaokoa Algeria katika kipigo.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Waafrika, Uswisi wana
kazi ya ziada kuhakikisha inatinga hatua ya robo fainali ya Kombe la
Dunia, wakati watakapovaana na Argentina leo.
Kikosi cha kocha Alejandro Sabella kilifuzu kwa
hatua ya mtoano kutoka Kundi F wakiwa mabingwa kwa kushinda michezo yote
mitatu, ambapo walizichakaza timu za Bosnia-Herzegovina, Iran na
Nigeria.
Hata hivyo, Uswisi nayo ilifanya vizuri
ilipoishinda Ecuador katika nafasi ya pili ya Kundi E, wakipata nafasi
ya kutinga katika hatua ya timu 16 kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya
Honduras katika mchezo wao wa mwisho wa makundi.
Argentina huenda wakamuanzisha Ezequiel Lavezzi
kama winga na hiyo ni kutokana na kuumia kwa nyota huyo wa Manchester
City, Sergio Aguero.
Wasiwasi mkubwa kwa Uswisi ni jinsi ya kumzuia
Lionel Messi na kazi hiyo inaonekana kukabidhiwa kwa Fabian Schar,
ambaye alijihakikishia nafasi baada ya Philippe Senderos katika mchezo
dhidi ya Honduras.
Post a Comment