Dar es Salaam. Ziara ya Naibu Waziri wa Maji,
Amos Makalla jana iliingia dosari baada ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Kinondoni, Salum Madenge na Diwani wa Kata ya Kimara, Paschal Manota
(Chadema), kurushiana matusi mbele ya wananchi na nusura wakunjane
mashati.
Tukio hilo lilitokea jana wakati wa mkutano wa
wananchi wa Kata ya Saranga, Kimara uliofanyika Uwanja wa Shule ya
Sekondari ya Mavurunza ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Makalla katika
ukaguzi wa miradi maji ya Dawasco.
Vurugu hizo zilitokea baada ya Makalla kuagiza
polisi kuwakamata wafuasi wa Chadema kwa madai kuwa walitaka kuvuruga
mkutano huo. Baada ya Makalla kutoa agizo hilo, Diwani Manota na Mbunge
wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika walisimama na kupinga uamuzi huo na
walirushiana maneno na Mwenyekiti Madenge aliyesema wawili hao waache
upumbavu.
“Unatetea nini? Acha upumbavu... Hatuwezi
kuendesha mkutano na watu wanaofanya vurugu,” alitusi Madenge huku
Manota akiwa na jazba kabla ya viongozi wengine wa kisiasa kuwatuliza.
Hata hivyo, kabla ya Makala kuzungumza, Mnyika
aliyekuwa ameongozana naye katika ziara hiyo alikuwa na wakati mgumu wa
kuzungumza kutokana na zomeazomea kutoka kwa wafuasi wa CCM.
Makalla alisema kosa kubwa lililosababisha kutokea kwa vurugu hizo ni maandalizi mabovu ya wafuasi wa vyama vyote.
“Wafuasi walikuwa na itikadi zao zaidi kuliko kuja
kusikiliza hoja za serikali kupitia ziara. Pia labda waliwakosa
uvumilivu kutokana na ahadi ya maji kuwapo kwa muda mrefu, lakini
kuvurugana wanasiasa ni kukosa uvumilivu,” alisema.
Kwa upande wake, Mnyika alipendekeza ziara zote za kiserikali zisiwe na uhusiano na vyama vya kisiasa.
“Kama ingekuwa ni mambo ya kuzungumzia ilani ya
chama, tangu mwaka 2005/10 ahadi ya maji ya asilimia 90 kwa Jiji la Dar
es Salaam haijatekelezwa,” alisema Mnyika.
Post a Comment