0
an Jose, Costa Rica. Kutoka ufukweni hadi katikati ya mji mkuu, mashabiki na raia wa Costa Rica walimiminika barabarani juzi kushangilia ushindi wa kihistoria wa timu yao iliyofanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya kuitoa Ugiriki.
Mashabiki katika mji mkuu wa Costa Rica, San Jose, walikusanyika katika eneo la Fuente de la Hispanidad, eneo ambalo hutumika kwa ajili ya sherehe za kitamaduni, wakiwa na bendera za taifa lao, nywele bandia na jezi zao wakiishangilia timu yao kwa ushindi wa mikwaju ya penalti.
‘”Taifa limeanguka. Kunaweza kuwa na tetemeko la ardhi,” alinukuliwa akisema mhudumu wa mgahawa, Teo Prestinary (43), katika fukwe za Nosara, ambapo kulikuwa na watu wengi wakishangilia kwa kuimba wimbo wa ‘Vamos Ticos’ (Go, Costa Ricans).
Maria Mendoza, mwenye miaka 33, alishuhudia shamrashamra hizo kupitia runinga akiwa mjini Santa Ana, alisema: “Ni furaha, furaha, furaha iliyopitiliza.”
Costa Rica ilifikia hatua ya kuitoa Ugiriki baada ya kuzichapa  Uruguay na Italia na kulazimisha sare na England, wakati ilitabiriwa kuwa ndiyo timu dhaifu katika kundi lao.
Na walishinda kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya mchezo wao kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 120. Na sasa Costa Rica wanasema kufika mbali zaidi.
“Siku zote huwa tuna matumaini,” alisema Luis Diego Escorriola, shabiki mwenye miaka 42, ambaye alikuwa akifuatilia mchezo huo kwenye runinga kabla ya kujiunga na wenzake mitaani kushangilia.

Post a Comment

 
Top