0
Dar es Salaam. Wasanii wanne wa filamu nchini wameondoka nchini usiku wa kuamkia jana kwenda Uturuki, ambako watajifunza utamaduni wa nchi hiyo pamoja na kukutana na wasanii wakubwa wa filamu wa nchi hiyo.Wasanii walioondoka nchini ni pamoja na Amri Athumani ‘Mzee Majuto’, Vincent Kigosi ‘Ray’, Irine Uwoya na Jacob Steven ‘JB’.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, JB alisema ziara hiyo ya wiki moja itawapa fursa ya kushirikiana na kubadilishana uzoefu wa kikazi na wenzao wa Uturuki.
“Tukiwa Uturuki tutakutana na wataalamu wa mambo ya filamu, hivyo tutajifunza mambo mapya, lakini pia tutabadilishana uzoefu na wenzetu wa Ururuki.
“Ni matumaini yangu kile tutakachojifunza Uturuki kitatusaidia kutengeneza filamu bora zaidi tutakaporudi nchini na kuifanya Tanzania kuwika kimataifa,” alisema JB.
Naye meneja mkuu wa Princess Cassino, Ali Aiden alisema: “Tumeamua kuwafadhili wasanii hawa kama njia mwafaka ya kuonyesha kwamba tunaunga mkono jitihada zao za kukuza tasnia ya filamu nchini.”
Balozi wa Uturuki nchini, Ali Dovutoglu alisema: “Ziara ya wasanii hao ni matunda ya ushirikiano mzuri kati ya Uturuk na Tanzania, ambayo tangu nimekuja hapa nimebaini ni nchi yenye utulivu wa hali ya juu.”

Post a Comment

 
Top