Mkate
Chakula anachokula mtu lazima kiwe na muda wa matumizi. Kutokuwa
na tarehe ya ukomo wa kutumika ni kukiuka haki ya mlaji. Kama hiyo
haitoshi ni lazima kiandaliwe katika mazingira mazuri na kukidhi viwango
vya matumizi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Ikumbukwe kwamba asilimia 60 ya Watanzania hasa
waishio mijini wamekuwa wakitumia mkate kama kifungua kinywa, hata hivyo
chakula hiki kimekuwa kikitengenezwa na watu wengi bila kufuata sheria,
lakini vyombo vya sheria vimekaa kimya.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa
licha ya uwepo wa matanuru ya kuoka mikate sehemu tofauti za nchi,
wafanyabiashara wengi hasa jijini Dar es Salaam wamekuwa wakizalisha
bidhaa hiyo uchochoroni na kwenye makazi ya watu, kisha kusambaza katika
maduka bila kuthibitishwa ubora wake na taasisi husika za Serikali.
Maduka yakiwamo yale makubwa (supermarkets),
baadhi yake yamekuwa yakitengeneza mikate inayolalamikiwa kuwa mibovu.
Baadhi yake hulalamikiwa kuwa haina ubora, mingine huwa na ukungu na
mingine kuwa migumu kutokana na kukaa kwa muda mrefu dukani.
Mfanyabiashara mmoja anayezalisha mikate na
kuisambaza katika mitaa mbalimbali maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam
anasema tatizo ni Serikali akidai imeshindwa kuwaongoza.
“Nilikuwa na wazo la kuanzisha kiwanda cha
kawaida kwa kutumia jiko la mkaa kwa ajili ya kutengeneza mikate na
kuuza katika eneo ninaloishi. Jiko langu nilinunua kwa Sh350,000, pia
ukijumlisha na vifaa vingine ambavyo nilivinunua sambamba na jiko hili
ni Sh450,000, nilifanya hivi kwani sikuwa na kazi ya kufanya. Nikaona
nijiajiri,” alisema mfanyabishara huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Kuhusu bidhaa zake kukaguliwa na kupitishwa na
Shirika la Viwango (TBS), pamoja na kibali cha Mamlaka ya Chakula na
Lishe (TFDA), mfanyabiashara huyo anasema: “Sina kibali kwa kuwa niliona
utakuwa mzunguko mrefu. Pili sikuwa na kiwanda maalumu, nisingefanya
biashara,” anasema mama huyo anayeuza mikate yake kwa gharama ya Sh800
kwa mkate mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa za TBS ya wiki iliyopita ni kwamba asilimia 96 ya mikate inayouzwa nchini haijathibitishwa ubora wake.
Baadhi ya wananchi wanahofia utendaji wa taasisi
za TBS na TFDA kama kweli zinafaa kuendelea kuwepo ikiwa zinashindwa
kudhibiti biashara hiyo, kiasi cha kuachia zaidi ya asilimia 96 ya
mikate kuuzwa bila kuthibitishwa ubora wake.
Muda wa kuharibika
Hili limekuwa tatizo kubwa, mara nyingi katika
maduka haya wauzaji huwabambika mikate iliyoharibika watoto na wasaidizi
wa ndani.
Adamu Shayo mkazi wa jijini Dar es Salaam anahoji:
“Kwanini mikate haina muhuri unaoonyesha muda uliotengenezwa, pamoja na
muda wa kuharibika? Binafsi nimeshanunua sana mikate kwenye maduka
makubwa (supermarkets), baadhi yake hadi huwa imeota ukungu, ila kwa
sababu ya haraka unajikuta umechukua kitu kibovu,” anasema.
Shayo anasema alishawahi kurudisha bidhaa ya aina hiyo katika
duka mojawapo jijini na kuambiwa na muuzaji kwamba hakuona wakati
anamkabidhi iwapo mkate huo ulikuwa umeshaharibika. “Ukirudisha ndiyo
mwenye duka naye anajifanya kushangaa kuwa hakuona pia. Naona ifikie
hatua sasa mikate nayo iwe na tarehe ya kutengenezwa na ile ya
kuharibika kama ilivyo kwa bidhaa nyingine, la sivyo tutakuwa
tunalishana sumu”.
Shayo anaiomba Serikali kuboresha sheria ya
chakula na kuongezewa makali, ili kuweza kuwabana wale wote wanaokwenda
kinyume na sheria hiyo ili kunusuru afya za walaji na kuondoa kabisa
bidhaa zisizokidhi vigezo.
Sheria ya Chakula inasema nini kuhusu suala hili
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilianzishwa
chini ya kifungu 4 (1) cha sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Na. 1 ya
mwaka 2003 na iliundwa baada ya Bunge kufuta sheria ya Dawa na Sumu na
sheria ya Kudhibiti Ubora wa Vyakula zote za mwaka 1978.
Moja ya majukumu ya TFDA ni kukagua viwanda vya
utengenezaji na maeneo ya kuuzia bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka ili
kuhahikisha kuwa viwango vilivyowekwa, vinafikiwa.
Kauli ya TBS na TFDA
Ofisa uhusiano wa Shirika la Viwango (TBS), Rhoida
Andusamile anasema ni jukumu la wakazi wa karibu na viwanda hivyo bubu
kutoa taarifa kwa shirika hilo ili kulinda usalama wa afya zao, akieleza
kuwa bidhaa zote zina sheria iliyowekwa kabla ya kutengenezwa na kisha
kumfikia mlaji.
“Ubora wa bidhaa yoyote ile una utaratibu wake,
mtu haruhusiwi kutengeneza bidhaa hasa vyakula kama mikate na vinginevyo
bila kuwa na kibali kutoka TBS na pia awe amesajili bidhaa yake hiyo
TFDA ambao na wao watajiridhisha kuhusu bidhaa yake kama inafaa
kupelekwa kwa walaji au la,” anasema Rhoida.
Anasema wamekuwa wakilazimika kutoa elimu kwa
umma, akitoa mfano wa kipindi cha mwezi Agosti hadi Desemba mwaka jana
walipotoa elimu na kukamata waliokaidi agizo la kuzalisha mikate kwa
kufuata sheria.
Anasema mikate yoyote inayotengenezwa, ni lazima ifikie kiwango ambacho kitakuwa kimekubaliwa na Tbs.
“Iwapo tutagundua uwapo wa bidhaa zisizo na ubora,
tutachukua jukumu la kuondoa bidhaa hizo sokoni, kufuta leseni ya
mhusika, kuweka utaratibu wa marejesho au fidia, kuweka taratibu za
kuharibu bidhaa duni au kuzirudisha zilikoagizwa na kutoza faini.
“Sheria hii imeambatana na kanuni nne za
utekelezaji ambazo ni kanuni za usimamizi wa alama ya ubora, ithibati ya
ubora, upimaji wa bidhaa, ithibati ya ubora wa shehena na kanuni za
usalama wa chakula,” alisema Rhoida
Ofisa uhusiano wa Mamalaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia
Simwanza anasema mara nyingi inakuwa vigumu kudhibiti mikate hasa kwa
wale wanaotengeneza kiholela mitaani.
“Februari mwaka huu kuna maduka ya kuoka mikate
tuliyafungia. Hiyo ilitokana na wao kutokidhi vigezo vile vilivyowekwa.
Wapo ambao hawakuwa wamesajili na wengine tulibaini kwamba wameanza
kutengeneza mikate isiyokidhi viwango. Wapo tuliowapa muda wa
kurekebisha hilo na wengine tuliwafungia kwa miezi mitatu ili
wajirekebishe na kutimiza maagizo tuliyowapa,” anasema Simwanza.
Post a Comment