Dar es Salaam. Pambano la bondia Francis Cheka la kuwania
ubingwa wa dunia unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Dunia (WBF),
sasa litafanyika Juni 6 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es
Salaam.
Cheka, ambaye awali alipangwa kuzichapa na Varely
Brudov wa Urusi, amebadilishiwa mpinzani na sasa atazichapa na bondia
kutoka Uingereza.
Akizungumzia pambano hilo, Cheka alisema tayari
ameanza kambi ya wazi jijini Dar es Salaam kujiwinda na pambano hilo na
kusisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha anatwaa tena ubingwa huo
aliovuliwa mwishoni mwa mwaka jana.
“Nategemea wiki ijayo kwenda Morogoro kujifua
milimani kwa ajili ya kujenga pumzi, lakini pia natarajia kuweka kambi
nje ya nchi kujiwinda na pambano hilo,” alisema Cheka.
Wakati huohuo, kocha mkuu wa timu
ya taifa ya judo iliyoweka kambi nchini Uturuki kujiandaa na Michezo ya
Jumuiya ya Madola, Hamis Zaid amesema kikosi chake hivi sasa
kimekubaliwa kujifua na timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kuonekana
kufikia viwango.
Zaid alisema awali walipowasili nchini humo
hawakukubaliwa kuanza mazoezi na timu ya taifa kutokana na kiwango chao
na kukabidhiwa timu ya vijana ya nchi hiyo kabla ya kufuzu hatua ya
awali na kupewa nafasi ya kujifua na timu ya taifa ya nchi hiyo.
“Wenzetu wana programu ya muda mrefu ambayo hivi sasa tunajitahidi kwenda nayo pamoja na mwelekeo wetu hivi sasa ni mzuri.”
Kocha huyo aliyeambatana na wachezaji Andrew
Thomas, Abubakar Nzinge na Mbarouk Selemani alisema programu hiyo
itafanyika hadi Juni 29 ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa michezo
hiyo.
Post a Comment