Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho
Ngassa amewapiku nyota wa Barcelona, Lionel Messi, Neymar kwa ufungaji
wa mabao kwa mwaka 2014, huku akiachwa na kinara wa ufungaji Cristiano
Ronaldo kwa magoli matatu tu.
Katika orodha iliyochapishwa na mtandao
www.iffhs.de unaojihusisha na masuala ya takwimu za soka unamwonyesha
Ngassa akiwa katika nafasi ya 4 katika orodha ya wafungaji 26 bora kwa
mwaka huu akiwa amezifumania nyavu mara sita akiwa na kikosi cha Yanga.
Ngassa ameingia kwenye orodha hiyo baada ya
kufunga mabao sita katika mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya
Komorozine ya Comoro.
Pamoja na Yanga kuondolewa kwenye michuano hiyo na
Al Ahly mwezi uliopita bado Ngassa anafungana na Haythem Jouini wa
Esperance wakiwa vinara wa ufungaji wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mwanasoka Bora wa Mwaka, Cristiano Ronaldo wa
Ureno anashikilia usukani kwenye orodha hiyo ya ufungaji akiwa amefunga
mabao tisa mwaka huu.
Mreno huyo alifunga mabao mawili dhidi ya Borussia
Dortmund na mawili tena dhidi ya FC Bayern Munich na kuiongoza Real
Madrid kufuzu kwa fainali ya Ligi ya Mabingwa UEFA. Ronaldo anafuatiwa
kwa karibu na Mhispania Juan Belencoso anayecheza Kitchee SC ya Hong
Kong ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Asia akiwa na mabao
manane.
Wachezaji waliofunga mabao saba kila mmoja ni
Waafrika wawili (Mmorocco Mouhcine Iajour wa Raja AC Casablanca na
nahodha wa Ghana, Asamoah Gyan anayechezeza Al Ain FC). Pia Waasia
wawili (raia wa Vietnam, Nguyen Van Quyet wa Ha Noi T&T F.C na
Msyria Omar Al Soma wa Al-Qadsia). Vilevile yupo nyota mmoja wa Amerika
Kusini (Mbrazili Paulo Rangel wa Selangor FA).
Waliofunga mabao sita mwaka huu ni Ngassa (Yanga),
Nasser Al-Shamrani (Al-Hilal FC), Kudakwashe Musharu (How Mine),
Haythem Jouini (Esperance).
Jumla ya wachezaji 26 wamefunga zaidi ya mabao matano, ila jambo la kushangaza Lionel Messi hayupo kati yao.
Tangu mwaka 1991, IFFHS imekuwa ikipiga hesabu na
kutoa orodha ya wafungaji bora wa mwaka wa dunia kwa kuangalia mabao
wanayofunga kuanzia Januari hadi Desemba 31.
Wafungaji hao wanapatikana kwa kuzingatia mabao
waliyofunga kwenye michuano ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la
Dunia, michuano ya mabara kwa timu za taifa, Olimpiki, pamoja na
mashindano ya klabu ya kimataifa.
Post a Comment