Dar es Salaam. Wakati Mbeya City ikipangwa
kufungua dimba la michuano ya kimataifa ya Bonde la Mto Nile dhidi ya El
Merreikh Al Fasher Mei 23, kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mwambusi
amesema wanakwenda Sudan kufanya kazi.
Mbeya City inaingia kambini leo kujiandaa na
michuano hiyo itakayoanza Mei 22 kwenye viwanja vitatu tofauti nchini
humo na Mbeya City iliyo kundi B itacheza mechi yake ya kwanza na El
Merreikh Al Fasher kwenye Uwanja wa Khartoum.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwambusi alisema
nafasi waliyoipata walikuwa ‘wakiililia’ tangu walipopanda daraja
kucheza Ligi Kuu hivyo hawatafanya mzaha na kuwaomba Watanzania kuwa
pamoja nao.
“Tulitamani kumaliza ligi katika nafasi ya kwanza
au ya pili ili tushiriki mashindano ya kimataifa ingawa tulimaliza
kwenye nafasi ya tatu na sasa tumepata nafasi ya kushiriki mashindano
mengine ya kimataifa huko tunakwenda kupambana,” alisema Mwambusi.
Kwa mujibu wa Mwambusi timu hiyo iliyokuwa ikijifua kwenye Uwanja wa Coca-cola na ule wa Shule ya Sekondari Iyunga mjini Mbeya.
Ofisa Habari wa Chama cha Soka Afrika Mashariki na
Kati (Cecafa), Rogers Mulindwa alisema jana kuwa michuano hiyo
itashirikisha timu 16 ambazo zitacheza katika hatua ya makundi na timu
mbili katika kila kundi zitafuzu kucheza hatua ya robo fainali
itakayoanza Mei 29 kabla ya fainali itakayochezwa Juni 4.
Post a Comment