Dar es Salaam. Idadi ya wagonjwa wanaohitaji
huduma ya upasuaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huenda
ikapungua baada ya hospitali hiyo kupewa vifaa tiba kutoka Serikali ya
Misri vitakavyotumika kutoa matibabu kwa wingi na haraka.
Zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaohitaji
huduma ya upasuaji katika Hospitali ya Muhimbili ni wenye matatizo ya
urolojia hali inayoonyesha kuwa mashine hizo zitahudumia wagonjwa wengi
zaidi.
Akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo kutoka kwa
Balozi wa Misri nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Dk. Marina Njelekela alisema huduma ambazo hutolewa na
kitengo cha urolojia ni pamoja na uvimbe wa tezi dume, kuziba kwa njia
ya mkojo, saratani ya kibofu na saratani ya tezi la kiume.
Dk. Njelekela alisema vifaa hivyo vimekuja wakati
muafaka ambapo vitasaidia kufikia azma ya Serikali ya kutoa huduma bora
ya afya kwa wakati, kwa wingi na kwa viwango vinavyokubalika.
Akitoa vifaa hivyo, Balozi wa Misri nchini, Hossam
Moharam alisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia hospitali hiyo
kwa kuipatia vifaa tiba zaidi ili kuboresha huduma ya afya.
Post a Comment