Dar es Salaam. Nyota wa Yanga, Kelvin Yondan na Athuman Iddi
‘Chuji’ wameungana na wachezaji wenzao jana asubuhi kuanza mazoezi
magumu huku Salum Telela na Abdallah Mguhi wakianza kufanya mepesi.
Daktari wa Yanga, Nassoro Matuzya aliliambia
gazeti hili jana baada ya kumalizika kwa mazoezi Uwanja wa shule ya
Sekondari, Loyola Mabibo jijini Dar es Salaam.
“Yondan na Chuji wako fiti kwa asilimia 100, ndio maana leo (jana) wamejiunga na wenzao kuanza kufanya mazoezi magumu.
Telela yeye ameanza mazoezi mepesi rasmi leo (jana) wakati Mguhi ana siku ya tatu sasa.” alisema Matuzya.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts alisema
amefurahishwa na kurejea kwa wachezaji hao na kusema ni dalili nzuri
kwake kabla ya kukabiliana na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara
wikiendi ijayo.
“Nimefuraha kurejea kwao, nafikiri ni dalili nzuri
za ushindi kwenye mchezo wetu dhidi ya Mbeya City. Nafikiri mchezo
utakuwa mgumu na ushindani mkubwa.”
Alifafanua kuwa anaenda kucheza na timu ambayo
haifahamu kwa maana hiyo itakuwa vigumu kwake kujua atumie aina gani ya
mchezo kukabiliana na timu hiyo ngeni kwenye ligi.
Post a Comment