Dar es Salaam. Sakata la Katibu Mkuu wa Yanga limechukua sura
mpya baada ya juzi jioni kuibuka vurugu kubwa Makao Makuu ya klabu hiyo,
Mtaa wa Twiga na Jangwani wakati kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga
kikiendelea.
Vurugu hizo zilizuka baada ya kuibuka makundi
mawili ya vijana, moja likiunga mkono uamuzi wa viongozi kuajiri katibu
kutoka Kenya, na lingine likipinga mpango huo.
Kutokana na hali hiyo, zilizuka ngumi miongoni mwa
makundi hayo, huku wengine wakirushiana mawe ambapo askari wa kutuliza
ghasia (FFU) walilazimika kuitwa kuja kuleta amani.
Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga
Clement Sanga alisema, Patrick Naggi bado hajapewa mkataba, ila ni
miongoni mwa wale walioomba ajira na bado mchakato unaendelea.
“Mwalusako bado ni katibu wa Yanga, taratibu za
kumpata katibu mwingine mchakato unaendelea na yeye ni sehemu ya
mchakato huo. Kuna nafasi pia ya Mkurugenzi wa Fedha na Ufundi,” alisema
Sanga.
Kauli ya Sanga imekuja siku chache baada ya Baraza
la Wazee wa Yanga kuitisha Mkutano na Waandishi wa Habari kupinga
kuajiriwa kwa Naggi, kwa kuwa siyo mwanachama.
“Katiba ya Yanga haitambui Baraza la Wazee,
inajieleza wazi, ila tunawaheshimu waliotoa ni maoni tu kama anavyotoa
mtu mwingine. Utaratibu waliotumia sio sahihi, kama walikuwa na hoja
wangefuata taratibu,” alisema.
“Dhamana ya kuajiri ni ya Kamati ya Utendaji na
siyo mtu mwingine yoyote. Kama kamati ikipitisha Naggi, basi atakuwa
Katibu Mkuu, kwa vile kuna wengine wamewahi kuajiriwa na hawakuwa
wanachama wa Yanga,” alisema zaidi.
Post a Comment