0

Timu ya Taifa Stars ikiwa nchini Gambia  
Banjul, Gambia. Safari ya Timu ya Taifa (Taifa Stars), juzi usiku ilikumbana na misukosuko ya aina yake baada ya kukwama majini ndani ya kivuko kwa zaidi ya saa tano wakati ikielekea Mji Mkuu wa Gambia, Banjul.
Stars inayodhaminiwa na TBL, ilikwama majini baada ya kivuko walichokuwa wakitumia kutoka kwenye mpaka wa nchi hiyo na Senegal, kushindwa kuendelea na safari kutokana na kuzidiwa na mkondo wa maji.
Kutokana na hali hiyo, kivuko hicho kinachofanana na kile cha Mv Kigamboni, kililazimika kukwepa mkondo huo wa maji kwa kupitia njia nyingine, lakini nako kilishindwa kuendelea na safari na kusimama majini mpaka mpaka kilipokuja kuvutwa na chombo kingine mpaka kwenye bandari.
Mbali na hali hiyo, Stars, leo inahitimisha dakika tisini za safari iliyokosa tija kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani, kwa kupambana na Gambia katika mchezo wenye taswira ya kukamilisha ratiba.
Siyo Tanzania wala Gambia itakayofaidika na ushindi kwenye mchezo huo, kwani zote zimeshaondoka kwenye vita ya kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo mwakani nchini Brazil.
Kikubwa kwa timu hizo leo ni kulinda heshima, lakini zaidi Gambia wakitaka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-1 na Tanzania katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabla ya mchezo wa leo, Stars ilishinda mechi mbili tu, dhidi ya Morocco (3-1), na kisha dhidi ya Gambia (2-1). Mechi zote imeshinda kwenye uwanja wa nyumbani.
Taifa Stars ilipoteza mechi zake dhidi ya Ivory Coast nyumbani na ugenini (2-0 ugenini) na (4-2 nyumbani), kisha ikakubali kipigo cha mabao 2-1 ugenini nchini Morocco.
Kwenye msimamo, Stars iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita, wakati wapinzani wao, Gambia wanaburuta mkia Kundi C wakiwa na pointi moja. Ivory Coast tayari imefuzu hatua ya mtoano.
Mshindi kutoka kila kundi kati ya matano hatua ya mtoano, atafuzu kucheza fainali hizo, ambazo kwa mara ya kwanza zitachezwa nchini Brazil.
Stars ilitua mjini Banjul katikati ya wiki hii, huku Kocha Kim Poulsen akisema wazi kuwa anaupa uzito wa kutosha mchezo dhidi ya Gambia hata kama wakishinda hawatakwenda popote.
Kocha wa Stars, Kim Poulsen alisema pamoja na kushindwa kufuzu kwa fainali hizo mchezo huo ni muhimu kushinda kwa vile kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi kutaisaidia kupanda viwango.
Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Independence mjini Bakau, unatarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi wa kati kutoka nchini Rwanda, Hudu Munyemana.
“Tukishinda na kupanda viwango vya ubora, kutatupa fursa ya kupangwa kwenye kundi zuri kwenye hatua ya kufuzu kwa fainali zijazo za Afrika,” alisema Kocha Poulsen.
Stars itawategemea Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, David Luhende, Henry Joseph, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Frank Domayo na Erasto Nyoni kutengeneza matokeo mazuri ugenini.
Kwenye kikosi hicho, hawatakuwemo washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu baada ya kuzuiwa na klabu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa upande wa Gambia, imewaita wanasoka wake saba wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, ambapo kufikia juzi nusu walishawasili na kujiunga na wenzao tayari kwa mchezo huo.
Kocha wa Gambia, Peter Bonu Johnson alisema amefurahishwa kuwasili kwa wachezaji, Omar Colley, Ken Mansally na Demba Savage kutoka Ubelgiji, na kwamba alikuwa akiwategemea Momodou Ceesay na Tijan Jaiteh jana.

Post a Comment

 
Top