Kikosi cha Taifa Stars kikiwa nchini Gambia
Leo timu yetu ya Taifa (Taifa Stars) itakuwa ugenini nchini
Gambia kucheza na wenyeji wao katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza
fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
Stars tayari imeishapoteza matumaini ya kufuzu
kushiriki fainali hizo, lakini inatakiwa kucheza mechi hii dhidi ya
Gambia kwa ajili ya kumalizia ratiba ya kundi C.
Katika kundi C timu ya Ivory Coast ndiyo
inayoongoza ikiwa na pointi 13 ikifuatiwa na Morocco yenye pointi nane,
halafu Taifa Stars ina pointi sita na Gambia inashika mkia ikiwa na
pointi moja.
Tayari Ivory Coast imejihakikishia nafasi ya
kusonga mbele kutoka kundi C kati ya makundi 10, ambapo kila kundi
litatoa mshindi kucheza raundi ya tatu ambayo itatoa timu tano
zitakazofuzu Kombe la Dunia 2014. Taifa Stars imeshindwa kupata nafasi
ya kuongoza kundi C kwa kuwa haikufanya vizuri katika mechi zake.
Ilichapwa 2-0 na Ivory Coast ugenini, mechi ya
pili iliichapa Gambia 2-1 nyumbani, ikaifunga Morocco 3-1 nyumbani Ikaja
kupoteza kwa kipigo cha mabao 2-1 na Morocco ugenini na katika mechi ya
tano, ilifungwa 4-2 na Ivory Coast.
Lakini pamoja na kushindwa kupata tiketi ya kufuzu
kushiriki fainali hizo, bado tunaamini Taifa Stars wana jukumu la
kuiwakilisha Tanzania na kucheza mechi hiyo dhidi ya Gambia kwa
kujituma, uzalendo, umoja na na lengo moja ili kuipatia Taifa Stars
ushindi.
Tunaamini wachezaji wamejiandaa vizuri na
wataendelea kutekeleza wajibu wao wa kuliwakilisha taifa uwanjani bila
kuidharau Gambia au kudharau mechi kwa kuiona haina umuhimu.
Mechi hii ni muhimu kwa Taifa Stars na Tanzania
kwa jumla kwani kama tutashinda itatusaidia kumaliza katika kundi letu
katika nafasi ya pili na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kupanda
katika viwango vinavyotolewa na Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) kila
mwezi.
Hivi sasa Tanzania katika viwango hivyo vya Fifa inashika nafasi ya 128, wakati Gambia inashika nafasi ya 163.
Ni wazi Taifa Stars hawatakata tamaa,
wanalipigania taifa letu kwa hali na mali, kujituma, kutengeneza nafasi
nyingi za ushindi na kuzitumia. Watakuwa makini zaidi muda wote wa mechi
huku wakiepuka makosa madogomadogo.
Wachezaji wa Taifa Stars wakiongeza umakini,
wakitumia akili na kuwa watulivu uwanjani tunaamini wana uwezo wa juu wa
kuleta matokeo mazuri uwanjani katika mechi dhidi ya Gambia.
Tunaamini, siku zote mchezaji wa timu ya taifa
anachopigania ni ushindi kwa taifa lake, mchezaji wa timu ya Taifa
anaposhinda huwa analiletea Taifa lake furaha na kujisikia fahari kuishi
katika taifa hilo.
Hatutarajii wachezaji wetu wakate tamaa katika kuliwakilisha
vizuri taifa lao, eti kwa sababu hata wakishinda mechi hiyo
haitawasaidia.
Kwenye mapambano yoyote yale, suala la kukata
tamaa linapaswa kuwa la mwisho mtu kulifikiria. Kukata tamaa mapema,
maana yake ni kujipima haki ya ushindi.
Tunatarajia kuona wachezaji wa Taifa Stars wanaipa
umuhimu mkubwa mechi hiyo kama ilivyokuwa katika mechi nyingine za
hatua hii ya makundi.
Post a Comment