0

Diwani wa viti maalumu manispaa ya Songea , Jacline Msongozi kushoto akimuuguza Upendo Malembeka katika wodi namba tano alipolazwa baada ya kupigwa, kubakwa na kung'atwa mdomo na sikio. Picha na Joyce Joliga  

Licha ya Serikali, jamii na taasisi mbalimbali zikiwamo Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), kupiga vita ukatili wa kijinsia, baadhi ya watu wamekuwa wakiendeleza vitendo hivyo huku waathirika wakiendelea kuwa wanawake.
Upendo Malembeka ambaye ni mkazi wa Mjimwema, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ni mmoja wa waathirika wa vitendo hivyo kwa kupigwa, kung’atwa mdomo, sikio na kubakwa na mwanaume ambaye hadi sasa hajachukuliwa hatua zozote za kisheria.
“Kila nikikumbuka unyama niliotendewa machozi yananitoka, sijui kwa nini aliamua kunitesa kiasi kile bila sababu. Sijui nilimkosea nini hadi akaamua kunitendea hivi. Siju kwa kuwa ameona mimi sina watu wa kunisaidia kutokana na umaskini wangu?
Naomba wanawake wenzangu na viongozi wa Serikali wanisaidie ili haki itendeke, wanisaidie niweze kuangaliwa kama nimeambukizwa Virusi vya Ukimwi kwa makusudi na kunipatia msaada wa kisheria. Nina uchungu usiokwisha, kamwe sitasahau tukio hilo maishani mwangu,” Upendo anaanza kueleza kwa uchungu akiongeza: Hivyo ndivyo Upendo alivyoanza kusimulia mbele ya mwandishi wa makala haya huku akiwa amenyofolewa kipande cha mdomo wa juu pamoja na sikio lake la upande wa kushoto, kupigwa na kuumizwa vibaya machoni.
Upendo mwenye umri wa miaka 23 anaeleza kuwa aling’atwa meno na mtesi wake na kubamizwa ukutani baada ya kugoma kufanya mapenzi na mfanyabiashara wa maduka ya vifaa vya pikipiki aliyefahamika kwa jina moja la Mwalongo.
Kisa hicho kimesikitisha wakazi wengi wa Songea ambapo Upendo ameuomba uongozi wa juu , wanawake wenzake walio na uwezo wa kumsaidia wafanye hivyo ili haki iweze kutendeka.
Akizungumza na kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, Wodi namba tano ambapo amelazwa, Upendo ambaye bado hali yake ni mbaya kutokana na majeraha na maumivu makali anayopata anaeleza kuwa bado hajafahamu hatima ya maisha yake kwa kuwa yeye hana uwezo wowote zaidi ya kumtegemea Mungu pamoja na Diwani wa Viti Maalumu Jacline Msongozi wa Manispaa ya Songea,ili amlipie matibabu yake na kumsaidia fedha ya chakula na vitu vingine.
Akizungumzia tukio hilo Upendo anasema kuwa alifika Songea mwaka 2007 akitokea Kahama mkoani Shinyanga katika Kijiji cha Nyalwelwe kwa nia ya kufanya kazi za ndani kwa mwanamke aliyemtaja kwa jina la Mama Komeka, ambapo baadaye aliamua kutafuta kazi ya uhudumu katika baa.
Anasema: “Nakumbuka siku ya Agosti 25 mwaka huu nikiwa nimemaliza muda wangu wa kazi ya uhudumu katika Pab ya Friends iliyopo Songea, rafiki yangu ambaye pia ni mfanyakazi mwenzangu( Zai) alipitiwa na mpenzi wake kazini hapo na kuniomba tuende wote disco, lakini mimi nilikuwa sijisikii kwenda huko kwa siku hiyo nikamwomba Zai aende mwenyewe.
Anasema kwa kuwa Zai alimwomba sana kwa madai kuwa hawatachelewa kurudi alikubaliana naye bila kujua yanayokwenda kumpata mbele.
Anasimulia kuwa wakiwa disko, shemeji yake aliwanunulia vinywaji na kila walipomaliza aliwaongezea vingine, lakini baadaye rafiki yake huyo akabadilika ghafla na kuanza kumnunia.
Anasema kuwa, wakati akiendelea kuwaomba wamrudishe nyumbani alitokea rafiki wa shemeji yake, ambaye alikuwa akizungumza na Zai mara kwa mara na kwa kuwa sauti ya muziki ilikuwa kubwa, hakuweza kusikia walichokuwa wakizungumza.
Baadaye rafiki huyo wa shemeji yake alimfuata na kumweleza kuwa asiwe na wasiwasi, watamrudisha au kumchukulia usafiri wa kurudi nyumbani.
Upendo anaongeza kuwa kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda, alikwenda tena kuwaomba wamrudishe nyumbani na kuwakuta tayari wameondoka, akawafuata nje ya ukumbi, ambapo baada ya muda Mwalongo alimfuata akiwa ameshika Sh15,000 akimweleza kuwa wamekubaliana wamchukulie chumba karibu na kazini kwake ili asubuhi ajihimu kazini kwani muda ulikuwa umekwenda na ni hatari mtoto wa kike kutembea peke yake usiku.
Anasema kuwa aliporudi ukumbini alikaa na kubaini rafiki yake Zai na mpenzi wake wameshaondoka na rafiki wa shemeji yake ambaye ndiye Mwalongo alimwomba amwamini na walikubaliana ampeleke akalale.
Anaeleza kuwa alimpeleka nyumba ya wageni Mambo Leo iliyopo Majengo na alipoulizia chumba na kukabidhiwa funguo alishangaa Mwalongo akimwagizia pombe kwa mlinzi, lakini yeye alikataa na kumweleza kuwa hahitaji pombe muda huo zaidi ya kutaka kupumzika.
“Wakati mlinzi akienda kumfuatia kinywaji, nilishangaa kukabwa koo na kusukumiwa ndani, kisha kuzibwa mdomo na kufungiwa ndani, huku nikitishwa kuwa iwapo nitapiga kelele atamuua,” anasimulia kwa uchungu.
Anaongeza: “Nilipigwa na butwaa kuona nikishushiwa kipigo na kuvuliwa nguo kwa nguvu, huku nikiingizwa vidole machoni kwa lengo la kungolewa macho. Kipigo kilikuwa kikubwa na mfanyabiashara huyo akaendelea kuning’ang’aniza tufanye mapenzi.
Sikuwa tayari, lakini Mwalongo aliniingiza bafuni na kunigongesha kwenye ukuta wa choo, kisha kunimwagia maji mwilini, kunisukumia kitandani na kuanza kunibaka bila ya kuvaa mpira wa kiume.”
Anasema kuwa Mwalongo hakuishia hapo, bali aliendelea kumkaba na kumwambia kuwa akipiga kelele atamuua, ambapo alishitukia ameng’atwa mikononi, kisha mdomoni na kutoa kipande cha nyama ya mdomo wa juu.
Akieleza zaidi anasema kuwa ilipofika saa 11 alfajiri alimwomba Mwalongo amuruhusu aende kutibiwa hospitali kwani maumivu yalikuwa makali, lakini aligoma na kumtaka amsubiri afuate pesa, huku akiendelea kumtisha kuwa asipige kelele wala kumwambia mtu yeyote kilichotokea.
“Nilikubali, lakini alipofungua mlango na kutoka alinifungia chumbani, ndipo nikapiga kelele za kuomba msaada, ambapo mmoja wa wahudumu aliwaeleza walinzi wamkamate mfanyabiashara huyo kwani alikuwa amemjeruhi mtu vibaya. Walimkamata na kumpeleka polisi na mimi kunipeleka hospitalini kupata matibabu, kwani nilikuwa na hali mbaya,” anasema.
Kwa upande wa Diwani Viti Maalumu, Jacline Msongozi amelaani tukio hilo na kusema kuwa ukatili aliofanyiwa binti huyo ni wa kutisha na haupaswi kufumbiwa macho.
Ameviomba vyombo vya dola kumsaidia binti huyo ili haki itendeke kwani tayari Upendo ameathirika kisaikolojia na amekata tamaa ya maisha.
Msongozi anasema kuwa tabia ya wanaume kulazimisha mapenzi na kubaka wanawake, imeshamiri mkoani humo huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto.
Diwani huyo amewataka wanawake kumsaidia binti huyo ili kuvitokomeza vitendo hivyo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa katika vyombo vya sheria.
Aliongeza: Binafsi nimesikitishwa sana, nimelifuatilia kwa kina tukio hili, nimekwenda polisi, naomba wampime binti kujua kama ameambukizwa magonjwa, pia aliyefanya unyama huo anafahamika ashtakiwe, Tuache kubebana na kuendelea kuumiza wanawake kutokana na unyonge walio nao kwani hii siyo haki kabisa.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ameeleza kusikitishwa na kitendo hicho, ambapo ameagiza mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho achukuliwe hatua za kisheria ili kukomesha matukio ya aina hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza amekiri kumpokea Upendo hospitalini hapo akieleza kuwa amepatiwa matibabu, hali yake inaendelea vizuri na kwamba wanatarajia kumfanyia vipimo mbalimbali ili kubaini iwapo ameambukizwa magonjwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Revocatus Malimi amesema kuwa upelelezi kuhusu tukio hilo unaendelea ambapo mtuhumiwa wa ukatili huo tayari amekamatwa na polisi.

Post a Comment

 
Top