0










KUIMARIKA kwa kiungo, Salum Telela kumeifanya safu ya kiungo ya Yanga kuwa na ushindani kutokana na idadi ya mafundi kuwa wengi.
Telela ameanza kupiga hodi kikosi cha kwanza na upo uwezekano wa kuipangua ‘first 11’ hiyo ya Mholanzi Ernie Brandts.
Kulingana na fomesheni ya 4-3-3 aliyokuwa akiitumia, Brandts na kumpa ubingwa msimu uliopita kiungo ilichezwa na Athuman Idd ‘Chuji’, Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na Frank Domayo.
Telela alipata nafasi hiyo katika mechi za kirafiki pamoja na Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumamosi iliyopita na kufunga bao la ushindi matokeo yakawa 1-0 baada ya Domayo kupata majeraha ya paja kwenye mechi ya Taifa Stars na Uganda.
Telela alionyesha kiwango cha juu katika mechi hizo, anashambulia na anakaba lakini kitendawili kilichopo ni kama atafanikiwa kupangua safu hiyo, lakini pia ni changamoto kwa Niyonzima, Chuji na Domayo kwani atakayelala atajikuta akisugua benchi.
Pia, nje ya uwanja kuna mafundi wengine wapya, wanaocheza nafasi hiyo, Hamis Thabit kutoka African Lyon na Bakari Masoud ambaye amepandishwa kutoka timu B ya vijana U-20 na msimu uliopita aliichezea Coastal Union ya Tanga.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Minziro aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Hiyo ni changamoto kwa wachezaji wote wajitambue, kwani ushindani utakuwa mkubwa.”
Telela alikuwa kwenye kikosi hicho kwa misimu minne lakini hakuwa na wakati mzuri.

Post a Comment

 
Top