LONDON, ENGLAND
ARSENE Wenger amegeukwa. Kwa sasa anatembea peke
yake. Mashabiki wa Arsenal wameamua kumchachamalia kutokana na tabia
yake ya ubahili huku ikiwa ni saa chache baada ya timu hiyo kupokea
kipigo katika mechi ya kwanza dhidi ya Aston Villa uwanjani kwao
Emirates.
Kundi la mashabiki wa timu hiyo juzi Jumapili
walimwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Arsenal, Ivan Gazidis, wakimtaka
amwambie Wenger abadili sera zake kuhusu masuala ya uhamisho wa
wachezaji klabuni hapo.
Wenger amepewa kiasi cha Pauni 70 milioni kwa
ajili ya kununua wachezaji mastaa kukiimarisha kikosi hicho ambacho
kimecheza misimu minane bila ya taji lolote.
Hata hivyo mpaka sasa hajamnunua mchezaji yeyote staa zaidi ya kumchukua bure kinda, Yaya Sanogo, kutoka Auxerre ya Ufaransa.
Mabosi wa timu hiyo pamoja na Wenger mwenyewe
wamekuwa wakisisitiza kwamba wahukumiwe Septemba 2 ambayo ni siku ya
mwisho ya usajili, lakini mabao mawili ya Christian Benteke na la
Antonio Luna yamewachanganya mashabiki wa Arsenal baada ya kipigo cha
mabao 3-1 kutoka kwa Villa Jumamosi.
Wenger alizomewa na mashabiki wa timu hiyo,
lakini kama vile haitoshi, mashabiki hao wameandika katika barua yao
kwamba hasira zao zitaendelea kama hatabadilika katika sera zake za
uhamisho wa wachezaji.
“Msifanye makosa, kama timu yetu haitaimarika
katika namna inavyocheza kwa wiki kadhaa zijazo, kutaongezeka hasira
katika majukwaa na itakuwa vigumu hali kurudi kuwa ya kawaida,” inasema
sehemu ya barua ya hiyo.
“Haijawahi kutokea hali mbaya ya hewa Arsenal kwa
zaidi ya miaka 30 na Bodi inaonekana kuzubaa tu wakati mambo yametoka
kuwa mabaya hadi mabaya zaidi. Tuna uhakika jambo hili halitatokea
tena.”
Licha ya ahadi nene za kusajili wachezaji mastaa
huku akisema anafanya jitihada, tayari Wenger amepoteza fursa za
kusajili mastaa kama Gonzalo Higuain, Luiz Gustavo, Marouane Fellaini,
Wayne Rooney na Luis Suarez wote wameota mbawa katika orodha yake.
Kesho Jumatano, Arsenal itakuwa ugenini kucheza na
Fenerbahce katika pambano la kufuzu hatua za makundi ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya na endapo mambo yakiwa mabaya, Wenger atajikuta katika
wakati mgumu zaidi.
Post a Comment