Mkuu
wa wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali akiwa kwenye mazungumzo na
wadau wa maendeleo waliofika wilayani humo kukagua miradi ya maendeleo
inayofadhiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Afisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph
(kushoto) ambaye pia ndio mkuu wa msafara huo akifafanua jambo mbele ya
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali wakati wa mazungumzo hayo.
Kulia ni Meneja Mauzo wa Kampuni ya Samsung tawi la Tanzania, Bw.
Slyvester Nteere.
Diwani
wa kata ya Ololosokwani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika lisiolo la
kiserikali la RAMAT, Bw. Yannick Ndoinyo akitoa maelezo juu mradi
waliobuni wa kituo cha utamaduni wa Kimasai ambao uko mbioni kuanza
ujenzi wake wakati wa ziara ya UNESCO kukagua miradi mbalimbali
inayofadhiliwa na shirika hilo.
Afisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph
(wa pili kulia) akitoa ushauri kuhusu kituo hicho kuwa kitakuwa na
manufaa ya kiuchumi kwa jamii hiyo ya kifugaji pindi kitakapokamilika
huku akisisitiza kuwa mipango iliyopangwa kama walivyopewa maelezo
iendane na wakati.
Mmoja
wa wadau wa maendeleo kutoka Ubalozi wa Uswiss nchini, Bw. Erick
Kalunga akisoma moja ya vitabu ndani ya maktaba hiyo inayofadhiliwa na
UNESCO, Maktaba hiyo inayotumiwa na wanafunzi wa shule ya sekondari
Ololosokwani na vijana wa kata hiyo.
Afisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph
(kulia) ambaye pia ni mkuu wa msafara huo wa kukagua miradi
inayofadhiliwa na UNESCO akiteta jambo na Meneja Mauzo wa Samsung tawi
la Tanzania, Bw. Sylvester Nteere ndani ya maktaba hiyo. Anayefuatilia
mazungumzo hayo kwa karibu ni Afisa Mradi wa uchumi wa kijani ndani ya
hifadhi hai (GEBR) Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa
KOICA, Myoung Su Ko (katikati).
Afisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph
(wa pili kulia) akitoa maelezo baada ya kutembelea Maktaba
inayofadhiliwa na UNESCO nje ya maktaba hiyo.
Kikundi
cha ngoma ya Kimasai kilichowatumbuiza wageni waliotembelea mradi wa
redio ya Loliondo FM inayofadhiliwa na UNESCO wakitumbuiza wakati wa
ziara hiyo.
Afisa
Miradi wa kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO, Myoung Su Ko, akijumuika
na kinamama wa kikundi cha ngoma za kimasai kutoka kata ya Ololosokwani
wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
Diwani
wa kata ya Ololosokwani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la
kiserikali la RAMAT inayomiliki Redio Loliondo FM, Bw. Yannick Ndoinyo
akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya miradi mbalimbali ikiwemo maktaba,
redio na ugawaji wa vitabu vya masomo ya Sayansi na hesabu
vinavyofadhiliwa na UNESCO kwenye kata hiyo.
Meneja
Mauzo wa Samsung tawi la Tanzania, Bw. Sylvester Nteere akitoa pongezi
kwa redio Loliondo FM kwa kuweza kuihamasisha jamii inayoizunguka kwa
kuburudisha, kutoa elimu na habari kwa ujumla hiyo sio kazi nyepesi
kutokana na uchanga wenu wa redio yenu.
Meneja
Mauzo wa Samsung tawi la Tanzania, Bw. Sylvester Nteere akikabidhi
zawadi kwa kikundi cha ngoma cha kinamama wakati wa ziara hiyo ya
ukaguzi wa miradi inayofadhiliwa na UNESCO kwenye kata ya Ololosokwani.
Wanakikundi
cha ngoma na wakazi wa kata ya Ololosokwani wakiangalia taarifa
mbalimbali za mitandao kwenye “Tablet” inayotengenezwa na kampuni ya
Samsung wakati wa ziara hiyo.
Mmoja wa wanakikundi akitumia Tablet kupiga picha wanakikundi wenzake pamoja na wadau wa maendeleo (hawapo pichani).
Wanakikundi
cha ngoma za kimasai wakiwa kwenye picha ya pamoja na ugeni huo huku
wakionyesha furaha baada ya kupokea zawadi ya fulana kutoka kampuni ya
Samsung.
Meneja
mauzo wa Samsung tawi la Tanzania, Bw. Sylvester Nteere (aliyeketi)
akiwa na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al
Amin Yusuph ndani ya studio za kurushia matangazo za redio ya Loliondo
FM inayorusha matangazo yake kwenye mnara wa Kampuni ya simu za mkononi
ya Airtel na kuifikia jamii kubwa kwenye maeneo hayo.
Serikali na
halmashauri wilayani Ngorongoro zimetakiwa kutoa ushirikiano kwa redio
za kijamii wilayani humo kwa lengo la kuwaletea maendeleo ya haraka
wananchi wao.
Hayo
yameelezwa na Meneja wa redio ya kijamii ya Loliondo FM, Joseph Munga,
wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendeshwa na Shirika la Elimu,
Sayansi na Utamaduni (UNESCO) redio hiyo ikiwa miongoni mwa miradi
inayofadhiliwa na UNESCO wilayani hapa wakiambatana na wadau wa
maendeleo kutoka kampuni ya Samsung na Ubalozi wa Uswiss hapa nchini.
‘Redio za
Jamii ndio chombo pekee kinachoziunganisha serikali na jamii katika
suala zima la kujiletea maendeleo’ alisema Joseph Munga.
Munga
aliongeza kwa kusema kuwa redio hiyo iliyoanza kurusha matangazo mwezi
Oktoba 2013 imekuwa ni kichocheo cha kutoa taarifa mbali mbali kwa jamii
wilayani Loliondo na kuibua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii
huku akiitaka serikali na halmashauri wilayani humo kuisaidia katika
kufikia malengo ya kuitumikia jamii na kuwashukuru wadau mbali mbali
wanaoiwezesha redio hiyo ikiwemo kampuni ya simu za mkononi ya Airtel
ambayo imetoa mnara wao kurushia Matangazo ya redio Loliondo.
“Suala hapa
ni ushirikiano hasa kwa halmashauri kuelewa na kuona umuhimu wa kutumia
redio hii katika matukio mbali mbali yanayofanyika kwenye halmshauri
vikiwemo vikao vya baraza la madiwani ili wananchi walioshindwa kufika
waweze kujua baraza lao limepitisha nini sanjari na huduma kwenye sekta
za afya na elimu”, alisema Munga.
Redio
Loliondo ni miongoni mwa miradi inayofadhiliwa na UNESCO wilayani humo
kupitia asasi isiyokuwa ya kiserikali ya RAMAT kwa kufadhili miradi ya
Maktaba,kutoa elimu kwa jamii ya kifugaji yenye malengo ya kuinua uelewa
na ufahamu kwa jamii hizo zilizopo pembezoni hasa katika suala zima la
kujiletea maendeleo.
Nae Afisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph,
alisema kuwa misingi ya redio hiyo inalenga kuikomboa jamii ya Loliondo
kwa kutoa elimu ya kifugaji na elimu kwa wananchi wilayani humo ambao
hapo awali hawakupata fursa ya kupata taarifa na matukio mbalimbali
yanayoendelea wilayani humo.
Akifafanua
faida za redio hiyo kwa jamii ni kupata taarifa mbali mbali zinazoendana
na shughuli zao za ufugaji hususan taarifa za chanjo ya mifugo na
madawa na kupata taarifa nyingine kuhusiana na masuala mbali mbali ya
kijamii ndani na nje ya wilaya hiyo ambayo hapo awali yalikuwa vigumu
kupatikana kwa wakati kutokana na jiografia ya wilaya hiyo.
“Pamoja na
kwamba malengo ya mradi huu yameanza kuonekana dhahiri machoni
petu,wafadhili kutoka UNESCO pamoja na kampuni ya simu za mikononi ya
Airtel ambayo mnara wake umekuwa ukitumika kurusha matangazo ya redio
hii, tunataka kuhakikisha kwamba mnaweza kujiendesha wenyewe hapo baadae
ili mradi kama huu uweze kuwanufaisha na wenzenu sehemu zingine”,
alisema Al Amin.
Akizungumzia
miradi inayoletwa na wafadhili wilayani humo Mkuu wa wilaya ya
Ngorongoro, Elias Wawa Lali alisema kuwa imechangia kwa kiasi kikubwa
kuwahamasisha vijana ambao wana shauku ya kuishi mijini kurudi nyumbani
na kuendeleza jamii hali ambayo imetafsiriwa kutoa uelewa kwa wanajamii
na hivyo ni faraja kubwa kwa wananchi wilayani Loliondo.
Ameyataka
mashirika na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuingalia
Ngorongoro kwa ukaribu na kuwa wadau wazuri wa kuiletea maendeleo wilaya
hiyo kwani miradi iliyopo itachochea ukuaji wa uchumi na kusaidia
uelewa wa wakazi wilayani Loliondo katika dhana nzima ya kujileta
maendeleo na kukuza uelewa wa wananchi wa kupata taarifa mbalimbali kwa
wakati.
Post a Comment