Muziki ni miongoni mwa starehe inayomhusu mtu yeyote ikiweza
kuburudisha, kufariji hata kuliwaza wakati wowote, popote kwa jambo
lolote.
Ndivyo ilivyo kwani muziki huweza kutumika
harusini, kwenye misiba na hafla mbalimbali ukisaidia kusherehesha,
kufurahisha, kuomboleza, kuhuzunisha hata kumsifu na kumtukuza Mungu.
Lakini zaidi katika ulimwengu wa leo muziki ni
zaidi ya hayo hasa kwa vijana kwani umekuwa ni ajira inavyowavuta wengi
kujaribu bahati zao kama watatoka kupitia fani hiyo.
Saidi Sekondo anayejitambulisha kwa jina la
kisanii la ‘Saisalu’ ni mmoja wa vijana waliovutwa na fani ya muziki
akijaribu bahati yake kutafuta riziki na mafanikio katika anayoyalenga.
Kwa malezo yake, Sekondo alianza muziki miaka tisa
iliyopita ambapo ilikuwa mwaka 2005, lakini hadi kufanikiwa kutoa wimbo
uliopigwa katika baadhi ya vituo vya redio, alitumia miaka saba
kufanikisha hilo ambapo mwaka 2012, alitoa wimbo wake wa kwanza alioupa
jina la ‘Kipato Kidogo’.
Saisalu anasema kuwa wimbo huo alimshirikisha
mwimbaji Steve RnB, mtayarishaji akiwa na Man Water kutoka Studio za
Combination Sounds.
Hata hivyo anasema kuwa kwa bahati mbaya video ya wimbo huo haikuchezwa sana kutokana na kuwa na picha isiyovutia.
Anasema kwamba kwa sasa ana wimbo mpya unaokwenda
kwa jina la ‘Madikodiko’, aliourekodi Studio za Mazuu na kwamba umeanza
kuchezwa kwenye baadhi ya vituo vya redio.
Saisalu anaeleza kuwa pamoja na kuvutiwa na
wanamuziki wengi wa miondoko ya Bongo Fleva, hakuwaza kujiingiza huko
kwa ajili ya kufuata wanachokifanya, bali kuja na mitazamo tofauti na
kufanya kitu tofauti.
“Nilikuwa nawasikiliza waimbaji wa Bongo Fleva
walio na mafanikio, pia chipukizi kama mimi nikagundua uwezo wa kufanya
kitu kama wanachofanya wao ninao, hivyo baada ya kumaliza masomo yangu
ya ufundi mwaka 2005 nilianza harakati rasmi, “anasema Saisalu.
Anabainisha kuwa katika sanaa yake nyimbo zote
anatunga mwenyewe na kwamba sasa anahitaji nyimbo mbili ili kukamilisha
albamu yake itakayokuwa na nyimbo saba.
Anataja nyimbo zake kuwa ni pamoja na kwanza wa
‘Kipato Kidogo’, Madikodiko ulio kwenye asili ya mdundiko, Sjachoka
kusubiri, Mgumba, na Mtetea zikiwa katika miondoko ya Bongo Fleva.
Anaeleza kuwa licha ya kuwapo kwa changamoto nyingi ikiwamo
baadhi ya madj kudharau kazi za wasanii chipukizi kwa kuacha kwa
makusudi kuzipiga katika vituo vya redio bado hajakata tamaa.
Saisalu anasema kuwa alichojifunza ni wasanii
wengi walifanikiwa kwa kupata watu wa kuwashika mkono hivyo kupata fedha
za kurekodi kwenye studio bora na kupata matangazo kwenye vyombo vya
habari jambo analolitaja kuwa ni tatizo kubwa kwa wasanii hasa wachanga
akieleza kuwa bila kujulikana hata msanii akiwa na kazi nzuri vipi ni
kazi bure.
“Baadhi ya redio zinarudisha nyuma kutokana na
kupiga nyimbo za wasanii wenye majina. Sisi wachanga, kama unataka
nyimbo yako ipigwe basi uwe na kitu kidogo, ingawa zipo baadhi
zinazotupa sapoti na zibarikiwe sana, “anasema Saisalu.
Anasema pamoja na hayo yote tayari ameshajisajili kwenye Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).
Kuhusu elimu anasema kuwa alisomea ufundi wa
kutengeneza viyoyozi katika Chuo cha Ufundi (VETA) ngazi ya cheti
kutokana na ufundi huo kuhitaji elimu zaidi ameamua kuwekeza nguvu na
akili katika muziki akiamini atapata fedha za kuongeza ujuzi wake.
Anaeleza kuwa elimu aliyonayo haimwezeshi kuingia
kwenye soko la ushindani kwani kila siku vifaa vya umeme vinakuja vipya
na kuhitaji ujuzi zaidi.
“Naamini nikiwa na ujuzi zaidi ni rahisi hata
kufungua kampuni na kupokea zabuni za matengenezo ya vitu mbalimbali.
Kama nitafanikiwa katika muziki, cha kwanza ni kuongeza ujuzi, “anasema
Saisalu.
Post a Comment