Nature.
Historia yoyote huwa na msingi wake. Uwe wa kitu au mtu,
historia hujengeka kutokana na matukio iwe ya kusikitisha, kusisimua,
kufariji hata kutia moyo.
Inaweza kuishia ikihuzunisha, kufurahisha hata
kuonyesha ushujaa kutokana na mtiririko wa matukio kwa jambo au mtu
husika anayelezea au kusimulia historia yake.
Ndivyo ilivyo pia kwa msanii wa muziki wa kizazi
kipya aliyejizolea umaarufu nchini hata nje ya mipaka ya Tanzania
kutokana na umahiri wake katika muziki.
Hata hivyo, siyo kila mmoja anajua historia ya
nguli huyo katika muziki huo, hata kumfanya apachikwe majina mengi na
mashabiki wake.
Mara zote mashabiki hawakusita kufurika alipofanya
uzinduzi wa albamu zake. Hiyo huwa ndiyo kile kinachoitwa na vijana
kuwa ni habari ya mjini.
Hali hiyo husababisha ulinzi wa ziada kuhitajika
ili kudhibiti msongamano wa mashabiki ambao usalama wao kuwa shakani
kutokana na msongamano.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya
Nature anaanza kwa kueleza kuwa yeye ni mzaliwa wa jijini Dar es Saam
katika Hospitali ya Ocean Road mwaka 1980 na kwamba jina lake halisi ni
Juma Kassim Ally.
Anasema kwamba kabla ya kufikiria kuwa mwanamuziki
alikuwa ni mchezaji mzuri wa soka katika timu za uswahilini maarufu
kwa jina la ‘Cha ndimu’.
Anaeleza kuwa pamoja na kucheza soka katika timu
ndogo wakati huo akisoma Shule ya Msingi Kurasini, alikuwa akiwaza kuwa
kipaji hicho cha soka ndiyo ‘kingemtoa’ na kumsaidia maishani.
Anabainisha kuwa alisoma shule ya msingi kwa shida na baada ya kumaliza hakuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari.
“Elimu ya ‘kibongo’ bila kuwa na mpango mbadala wa
masomo ya ziada, ni vigumu kufaulu. Wenzangu waliokuwa na uwezo
walisonga mbele mimi nikaishia hapo, “anasema Nature.
Anafafanua kuwa kutokana na familia yake kutokuwa
na uwezo wa kumsomesha, binafsi alikuwa na moyo wa kusoma na aliazimia
kufanya analoweza ili ajiunge na sekondari mwaka unaofuata, baada kusota
nyumbani kwa mwaka mmoja baada ya kumaliza elimu ya msingi.
“Nilikuwa nikiishi uswahilini, biashara ya kwanza wakati ule kwa
watoto kama mimi, ilikuwa kuuza vyuma chakavu, hivyo nilikuwa kiguu na
njia kutafuta malighafi hiyo na kuuza, lengo likiwa kutafuta
ada,”anasema Nature.
Msanii huyo nyota anasema kwamba alikuwa akiongeza
kipato chake kwa kazi nyingine ikiwamo kupasua mawe eneo la Kurasini,
kusukuma mikokoteni ya maji na mizigo, pia kuokota mkaa na kusaidia
wazazi kuuza vitumbua.
“Baada ya kukusanya fedha hizo nilipata fedha ya
kianzio za kulipia shule binafsi iliyopo maeneo ya Temeke (hakupenda
kuitaja),”anasema.
Anaeleza kuwa alisoma huku akifanya kazi hizo ili
kujikimu katika mahitaji mbalimbali ya shule, ikiwamo kulipia mitihani
ya kila wiki, kununulia madaftari, vitabu na vifaa vingine vya shule.
Nature anasema kuwa akiwa kidato cha tatu ndipo
alipata hisia za kupenda muziki, ambapo walikuwa wakienda katika kumbi
za starehe na kukutana na vijana waliokuwa wakiimba kutoka shule
mbalimbali.
Anasimulia kuwa wakiwa shuleni, kulikuwa na mpango
maalumu wa kupelekwa katika semina ili kujikinga na maradhi ya Ukimwi,
matumizi ya pombe na dawa za kulevya.
Anafafanua kwamba walikuwa wakifanya uhamasishaji
katika Ukumbi wa Amana Center uliopo Ilala na pamoja na Ukumbi wa Ruaha
Galaxy uliopo Kimara.
Anabainisha kwamba, hapo ndipo alianza kutunga
mashairi akioanisha na kile walichokuwa wakifundishwa na kuimba peke
yake akijikumbusha. “Hapo nilihisi kuna kitu kipo ndani yangu kuhusu
muziki.”
Anasema hisia hizo ndizo zilimfanya awashawishi
vijana wenzake watatu kuanzisha kikundi kilichokuwa likijulikana kwa
jina la For Skills Gangstar (FSG), ambalo kiongozi wake alikuwa yeye
akitumia jina la Nature Man. Anawataja wenzake hao kuwa ni Mark 2 B,
Chriss na Dollo.
“Kama kuna watu nilikuwa nawakwaza wakati huo
basi ni wazazi wangu. Walikuwa wanatiwa ndimu na mjairani kuwa muziki ni
uhuni, hivyo mimi nitapotea. Nyumbani moto ukawa ukiwaka kila
niliporudi, hivyo nikiwa njiani kurudi nilipanga maneno mazuri ya
kumliwaza mama. Yalimtuliza jazba kwa siku husika na kupata chakula,
siku nyingine kilikuwa kinawaka, hata chakula nilinyimwa,”anasema
Nature.
Anaeleza kuwa wakiwa na kundi hilo walipata
changamoto nyingi ikiwamo kutembea kwa miguu kwa umbali mrefu kutafuta
shoo za kuimba ili watambulike.
“Tuliwahi kutembea kutoka Posta hadi Kimara, mara
ya kwanza tulisikia kuna shoo ya jamaa fulani, tukatoka Kurasini hadi
Posta. Kumbe hatukusikia vizuri ilikuwa ni Kimara na tukalazimika
kutembea hadi Kimara kwa miguu, “anasema.
Anasimulia kuwa mwaka 1999, waliingia studio iliyokuwa chini ya
Mtayarishaji Endrico, inayoitwa Sound Craftaz na kurekodi wimbo wa
kwanza alioupa jina la ‘Jambo hili ni Batili’.
Anaeleza kuwa mashairi ya wimbo huo yalikuwa
yakilenga kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya ambayo kwa wakati huo
yalikuwa yameshamiri.
Anabainisha kuwa wimbo huo ulifanikiwa kusikika
katika kituo cha Redio One, akieleza kuwa kabla ya kupeleka studio kwa
kuwa yeye ni kiongozi alilazimika kurudi mtaani kuokota vyuma chakavu
ili kupata fedha za kununulia kanda ya kurekodi wimbo huo na kuzisambaza
studio.
Anafafanua kuwa iliwachukua mwezi mzima kutafuta Sh3,000 za kununulia kanda tupu.
“Sikujali kuwa mimi ni kiongozi kwa kuwa niliokuwa
nao kwenye kundi hawakuwa na uzoefu wa kuokota vyuma chakavu kama mimi.
Nililazimika kuokota kwa kazi mbili, ada na kununulia kanda,”anasema.
Kuibuka kwa Nature
“Mwaka 2000 ni wa historia kwangu kwani nilihitimu
kidato cha nne kwa shida na kufanikiwa kuupeleka redioni wimbo wetu
tuliorekodi,”anasema Nature.
Hata hivyo, anasema kuwa katikati ya mwaka 2000
kundi lao lilivunjika sababu ikiwa kila mmoja alitafuta njia yake
kimaisha baada ya kumaliza shule.
Nature anasema kuwa hali hiyo haikumkatisha tamaa
na kuendelea kutembea kwa miguu hadi Kimara kutafuta shoo za kuimba ili
kujenga urafiki na wanamuziki wakubwa.
“Kipindi hicho nilidhalilishwa sana na makondakta
wa daladala. Kuna wakati nilichoka na kuamua kuvaa nguo za shule,
nikajidai mwanafunzi huku nikionekana baba mzima. Nilishushwa njiani
kwa kukosa nauli au kwa kushindwa kuelewana na konda,”anasema.
Anaeleza kuwa kama ilivyo maisha ya uswahilini,
majirani na watu wanaomfahamu walimuona kama chizi na kumsema kwa maneno
ya kejeli, wakimchukulia kuwa ni mwizi, mtukutu, mvuta bangi na mambo
yanayofanana na hayo ingawa ukweli sikuwa na sifa hata moja kati ya
hizo.
“Kutoka kimuziki kulikula akili yangu yote wakati
huo. Hata nilipoambiwa kuna shoo Kibaha, bila kualikwa na kuhisi naweza
kupata nafasi ya kuimba hata wimbo wangu mmoja, ningeenda bila kujali
kama nina nauli au sina. Hakuna mtu hata mmoja wa familia yetu ambaye
ningemwambia anipe nauli niende huko na kukubali, waliona ni uhuni na
upuuzi, “anasema Nature.
Itaendelea wiki ijayo. Usikose kujua Nature ataeleza nini?
Itaendelea wiki ijayo. Usikose kujua Nature ataeleza nini?
Post a Comment