“Hakuna kifungu cha sheria kinachosema Rais anaweza kulivunja Bunge hilo, bali linaweza kuahirishwa. Nami ningeshauri liahirishwe hadi hapo maridhiano yatakapopatikana.
Dar/Zanzibar. Zikiwa zimebaki wiki mbili kuanza
vikao vyake, baadhi ya wanasheria wamehoji uhalali wa Bunge hilo
kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba bila ya kuwapo kwa wajumbe wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wamesema msimamo wa Ukawa kukataa kurejea katika
vikao vya Bunge hilo na kushikilia msimamo wa kutaka ijadiliwe Rasimu ya
Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, utafanya akidi ya wajumbe kwa
ajili ya kupitisha uamuzi katika Bunge hilo kutotimia.
Wanasheria hao waliohojiwa jana kuhusu msimamo wa
Ukawa kususia Bunge na hatima ya Katiba Mpya wamesema hakuna uwezekano
wa kisheria kuipitisha wala kufanya mabadiliko ya vifungu ili kupata
uhalali wa kufanya hivyo.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Julai 8
mwaka huu, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alisema
iwapo Ukawa watarudi bungeni lakini wakasusa tena kadri mjadala
utakavyoendelea, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.
Hata hivyo, wanasheria hao walisema kwamba bila
kuwapo maridhiano, Bunge hilo haliwezi kufikia tamati na si rahisi
kupata akidi ambayo si tu inatakiwa na Kanuni za Bunge na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, bali pia Katiba ya sasa.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Kifungu cha 26(2)
kinaeleza: “Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge
Maalumu, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya
wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya
idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Zanzibar.”
Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Jesse James alisema iwapo hakutakuwa na maridhiano hakuna
chochote kinachoweza kufanyika au kupitishwa zaidi ya kuahirisha Bunge
hilo hadi pale watakapokubaliana.
“Hakuna kifungu cha sheria kinachosema Rais
anaweza kulivunja Bunge hilo, bali linaweza kuahirishwa. Nami
ningeshauri liahirishwe hadi hapo maridhiano yatakapopatikana,” alisema
James.
Kuhusu kubadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ili kubadili akidi ya wajumbe wa pande zote mbili, James alisema
hilo litasababisha vurugu zaidi.
Alisema hilo linaweza kufanyika kwa kuitishwa kwa
Bunge la Muungano, lakini kwa maoni yake itakuwa ni uhuni kwa kuwa
haiwezekani kubadilisha kanuni wakati mchezo umeshaanza.
“Wakifanya hivyo itakuwa ni vurugu tupu, watakuwa
wanapitisha kwa matakwa yao kitu ambacho kitaleta shida wakati
itakapowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya upigaji kura,” alisema James
na kuongeza:
“Wakati wa upigaji kura italeta shida kwani hawa
ambao hawakubali watapiga kampeni kuwaeleza wananchi wasiikubali kwa
kuwa si matakwa yao na hapo itakuwa vurugu zaidi.”
Akizungumzia suala la Sitta kuitisha kikao cha maridhiano James
alisema Mwenyekiti huyo wa Bunge la Katiba amefanya hivyo kutokana na
mambo kuwa magumu lakini hana mamlaka ya kufanya hivyo kisheria.
Haya hivyo, wakili na kiongozi mwandamizi wa Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema kitendo
cha kutaka kubadilisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kitapoteza uhalali
wa kisheria wa kuwapo kwa Bunge hilo na ni kinyume na Katiba ya nchi
Ibara ya 98 inayoeleza kuwa, ili Bunge liweze kufuta mambo fulani ni
lazima likubalike katika pande zote za Muungano (Bara na Zanzibar).
Sungusia alisema ili kubadilishwa kwa sheria hiyo,
ni lazima Bunge la Muungano likutane na kuongeza kuwa, kwa muda
uliobaki jambo hilo ni gumu, labda kiitishwe kikao cha dharura cha
Bunge.
“Haya yote yametokana na Bunge la Jamhuri kuwa
sehemu ya Bunge la Katiba. Ilitakiwa mabunge haya yajitegemee na
kutoingiliana katika utendaji wake wa kazi. Ndiyo maana wapo
wanaolalamikia tafsiri ya Kifungu cha 25 ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba,” alisema.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS),
Charles Rwechungura alisema: “Endapo Ukawa hawatarudi bungeni hakuna
uamuzi utakaopitishwa na hata ikibadilishwa sheria ni wazi kuwa itakuwa
kwa manufaa ya watu fulani.”
Alisema Bunge linaweza kubadili sheria lakini
ubadilishwaji huo usiwe kwa sababu ya kukwepa upungufu wa akidi na
kusisitiza kuwa ni lazima zitafutwe njia za kuwarejesha wajumbe wa Ukawa
bungeni na kila upande uwe na utashi.
“Kama kuna sheria ifuatwe na kama kuna tatizo
litatuliwe na siyo kubadili sheria husika. Kama yote hayatawezekana ni
vyema mchakato ukaanza upya,” alisema.
CCM, Ukawa wazungumza
Mjumbe wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema wapo katika mazungumzo na CCM kutafuta mwafaka.
“Tupo katika mazungumzo ila kwa sasa hatuwezi
kusema kama tutashiriki au hatutashiriki vikao vingine. Tukiridhiana
kisiasa tunaweza kwenda katika kikao cha Sitta (cha maridhiano),”
alisema Mbatia.
Hata hivyo, Mbatia alisema ni vigumu Bunge la
Katiba kupitisha jambo lolote bila akidi kutimia na kusisitiza kuwa kama
sheria itabadilishwa, ni wazi haitakuwa sheria nzuri.
“Uandikaji wa Katiba ni tendo la maridhiano na
siasa inafuata baadaye, ili kubadili sheria ni lazima Bunge la Jamhuri
likutane wakati ratiba zinaonyesha kuwa litaketi Novemba,” alisema.
Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisisitiza msimamo
wa Ukawa na chama chake kuwa wajumbe wake hawatarejea bungeni iwapo
itajadiliwa rasimu nyingine tofauti na ile ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Mbowe alitaja mambo mengine ambayo yatawafanya
warejee katika Bunge hilo kuwa ni kuendeleza mazungumzo na Rais Jakaya
Kikwete kwa sababu ndiye msimamizi mkuu wa mchakato huo.
Nape alia na Ukawa
Wakati Ukawa wakiwa katika mazungumzo na CCM,
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye amewataka Ukawa
kurudi bungeni, akisema suala la kuzunguka kwa wananchi ili wasiipigie
kura Katiba Mpya ni la mwisho ambalo kila mdau atashirikishwa ili
kuipata katiba iliyo bora.
Nape aliyasema hayo akijibu msimamo uliotolewa na
Mbowe wa kutorejea bungeni na kwenda kwa wananchi kuwaambia waikatae
Katiba itakayopendekezwa.
“Nilisikia alichokisema Mbowe jana (juzi). Sisi
(CCM) tunawashauri warudi bungeni ili tuipitishe Katiba na muda
utakapofika wananchi waambiwe ukweli. Wao waipinge na sisi tuitetee ili
tuone wananchi wataamua nini kwa sababu kwa vyovyote itakavyokuwa, wao
ndio wenye uamuzi wa mwisho,” alisema Nnauye.
ZIRPP wamkosoa Sitta
Katibu wa Kamati ya Kuwaunganisha Wazanzibari
katika mjadala wa Katiba Mpya (ZIRPP), Muhammed Yussuf Mshamba amesema
Sitta alianza kazi yake vibaya kwa kuruhusu kanuni kubadilishwa kabla ya
kuanza kutumika kupitisha Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hayo jana wakati wajumbe sita wa kamati
hiyo walipokutana na kumteua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri
Kiongozi Zanzibar, Ali Abdallah Suleiman kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo.
Alisema kwa kuwa kanuni zilitungwa na kupitishwa
na bunge hilo, haikuwa mwafaka kubadilishwa kabla ya kuanza kutumika
katika kupitisha vifungu vya Rasimu.
Imeandikwa na Boniface Meena, Fidelis Butahe, Julius Mathias na Mwinyi Sadallah
Post a Comment