HOJA yangu kuu tangu wiki iliyopita ni hitaji la muhamo wa
liwazo kwenye mfumo wa ufundishaji na elimu kwa jumla kama kweli
tunataka kusonga mbele.
Ni dhahiri shahiri kuwa tunahitaji sasa kuachana
na kuwafundisha watoto wetu masomo na nadharia na kujikita kufundisha
ujuzi, maarifa na utambuzi.
Nadharia na masomo haviwezi kutuvusha kwenye
umaskini wa akili na umaskini wa kipato. Tukiwajaza wananchi majuzuu ya
nadharia na masomo ambayo hayawapi maarifa wala kuwafanya wawe wavumbuzi
wa majibu ya matatizo yetu ni kutwanga maji kwenye kitu. Wenzetu
walioendelea waligundua hilo mapema wakaachana na masomo sasa
wanafundisha ujuzi, maarifa, uvumbuzi, utambuzi na ung’amuzi wa fursa za
kimaendeleo na kuitafiti dunia.
Nimewahi kuandika kuwa wapo watu ambao hawajaingia
darasani kabisa lakini wanaishi maisha mazuri kimifumo ya jamii zao
bila kuwa na uhaba au upungufu wa mahitaji ya msingi kama maji, chakula
na malazi. Wako babu zetu vijijini wana ujuzi na maarifa ya kutosha hata
kutabiri hali ya hewa na majira ya misimu na wakachukua tahadhari
lakini hawajui kusoma na kuandika.
Kiasili binadamu ni viumbe ambao Mungu ameweka
ufahamu na weledi mkubwa bila kujali umezaliwa na nani. Ndiyo maana
mtoto wa miezi minne hawezi kupeleka chakula sikioni; analenga ulipo
mdomo bila kufundishwa. Kama Mungu hakuuweka weledi/umaizi hakuna mtu
anayeweza kuuweka weledi huo.
Weledi asilia na umaizi ambao Mungu amempatia
mwanadamu ndiyo kiungo kikuu cha mafanikio yake. Anachotakiwa kufanya ni
kukuza vipawa hivyo, kuvipalilia vipawa hivyo ili vichanue na
vitamalaki. Shule ziko kwa ajili ya kukuza na kuchagiza ujuzi, weledi,
umaizi na vipaji vya binadamu ili vikue na vichanue siyo kukaririsha
watu masomo au nadharia.
Wavumbuzi na wagunduzi wote hawakufundishwa
darasani kuvumbua wala kugundua, ni akili yao ya kuzaliwa iliyosaidiwa
na mazingira ya kutafakari na furaha ya ndani ya moyo.
Sasa, iweze leo tudharau asili ya akili na weledi
wetu eti kwa sababu tu tuliachiwa masomo na wakoloni? Hata kama mtoto
ana kipaji cha kuimba unalazimisha tena kwa kumchapa viboko ajue kanuni
za pembe mraba? Unamlazimisha akariri tarehe ya kugunduliwa fuvu la mtu
wa kale. Unamlazimisha akumbuke tarehe aliyofika Vasco da Gama ghuba ya
uajemi na Rasi ya Tumaini jema, ili iweje? Jiulize wanaojua kuimba
hawaishi? Wanaojua kucheza mpira hawaishi? Wanaojua kuchonga hawaishi?
Wanaojua kujenga hawaishi? Wanaojua kuhubiri hawaishi? Wanaojua kufuma
hawaishi? Wanaojua kutibu watu hawaishi?
Ujuzi, maarifa, utambuzi na ung’amuzi ndiyo kitovu
cha mtalaa makini siyo nadharia. Jiulize kipi chenye manufaa kupata
ujuzi kuhusu ufugaji bora na uvunaji wa gesi ama kujua idadi ya marais
duniani? Kipi kina manufaa, kupata ujuzi wa kilimo bora au kujua vita
vya kwanza vya dunia viliaza lini? Kipi kina manufaa kujua kanuni za
ujenzi au kujenga? Kujua mbinu za ujasiriamali au kujua miyeyuko ya
barafu huko Ulaya?
Elimu asilia ndiyo imefanya nchi zilizoendelea
kutafakari aina ya maarifa wanayotakiwa kuwapa watoto wao ili waitawale
dunia. Siyo kwetu maarifa hayatolewi kabisa, na msisitizo uko kwenye
kukalili mada za masomo, ili kesho watukiwe shahada. Vyuo vikuu
wanafanya bidii kukalili maandiko na nadharia za wanafalsafa wa
kale-kisha wanatunukiwa digrii nyingi. Wanaitwa wasomi madaktari-pasipo
ujuzi wala maarifa. Wakirudi kwenye jamii wanajikuta walichosoma
hakifanani na hakiwasaidii kuyakabili maisha. Wanabaki kulalamika na
kudai posho tu. Haya ndiyo malengo ya elimu?
Maarifa asilia waliwafanya babu zetu wasiojua
kusoma na kuandika waweze kufanya biashara hadi nchi za jirani
wakitembea kwa mguu bila kuwa na gari wala nyenzo-vivyo hivyo wamachinga
wa leo. Lakini profesa wa biashara hawezi hata kuuza karanga.
Maarifa asilia ndiyo yaliyowafanya nchi za Ulaya
watafsiri elimu sahihi iliyokuwa kwenye falsafa na teolojia zaa kale.
Kuweka maarifa na ujuzi huo kwa lugha za jamii zao ili wayafahamu na
kuyafanyia kazi kujiletea maendeleo. Kweli maendeleo yakafanyika!
Hata wanasayansi wengi waliogundua kanuni na fomula nyingi
zilizotumika kutengenezea vitu kama magari, ndege hawakuwa na vyeti
vingi. Wengine hakuwa na vyeti kabisa, bali walitumia muda wao mwingi
kufikiri na kubuni kikamilifu hadi wakaibuka na manufaa hayo makubwa
yaliyoibadili dunia hii.
Nadharia na masomo havitusaidii. Elimu ya asilia
na maarifa tumizi ndivyo vitatusaidia kuondokana na umaskini wetu.
Kubadili mitaala hukutusaidii, kurahisisha vigezo vya watu kupata digrii
hakutusaidii, kuongeza idadi ya wasomi wa vyeti hakutusaidii na hata
kujenga vyuo vikuu lukuki hakusaidii.
Kitakachotusaidia kama nchi ni kuachana na masomo
tuliyoachiwa na wakoloni na kuanza sasa kuelimisha watoto wetu kwa elimu
asilia na maarifa tumizi ili wawe wavumbuzi, wagunduzi, wabunifu na
wenye maadili ya kuitafsiri dunia. Elimu asilia inawapa maadili ya
rohoni watu kuwa watendaji siyo wapiga porojo. Elimu asilia inaibua
vipaji na vipawa na kuvichepusha ili vitamalaki na kumsaidia mtu
kuingiza kipato. Elimu asilia itawawezesha Watanzania kujua rasilimali
zao na kuzitumia kupata nafuu ya maisha na utajiri. Ndiko kwenye siri ya
mafanikio. Mungu atusaidie kung’amua hili.
Post a Comment