Baadhi ya wakulima walipinga wakisema ipo kampuni inayonunua pareto yao
kwa Sh2,200 na kulipa papo kwa papo na kwamba pia wapo watu waliofika
kwenye vijiji kuwataka wakulima wasilime pareto.PICHA|MAKTABA
Mbeya. Wakulima wa
Pareto mkoani hapa wamehoji uwapo wa mkanganyiko wa bei ya zao hilo
msimu huu baada ya kuwapo kwa wanunuzi wanaowalipa Sh2,200 papo kwa papo
huku wengine wakiwalipa Sh1,500 kwanza na nyingine hulipwa baada ya
kupima sumu.
Malalamiko ya mkanganyiko huo waliutoa mbele ya
Ofisa Kilimo wa Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT), Christopher Shimwela
aliyefika katika Kata za Maendeleo na Itala Mbeya Vijijini kwa ajili ya
kuwafafanulia bei ya pareto kwamba ni kati ya Sh1,500 na Sh2,5000
kutegemeana na ubora na uwingi wa sumu.
Shimwela alisema bei ya pareto kwa kawaida ni kati
ya Sh1,500 hadi 2,500 kwa kilo moja lakini mkulima alipwe kwanza
Sh1,500 ambazo ni sawa na bei ya pareto yenye sumu chini ya asilimia 0.9
na kwamba fedha nyingine watalipwa ndani ya siku 30.
‘Kwa mfano wakulima wa Vijiji vya Uzaha Muungano
walilipwa Sh1,500 kwa kilo baada ya kuuza pareto yao lakini baada ya
kupima pareto yao imekuwa na sumu ya asilimia 1.4 hivyo wataongezewa
Sh700 kwa kila kilo’’ alisema.
Hata hivyo, baadhi ya wakulima walipinga wakisema
ipo kampuni inayonunua pareto yao kwa Sh2,200 na kulipa papo kwa papo na
kwamba pia wapo watu waliofika kwenye vijiji kuwataka wakulima wasilime
pareto.
Akizungumzia utata huo, Mkurugenzi wa Bodi ya
Pareto Tanzania, Ephraem Mhekwa alisema mnunuzi yeyote atakayenunua
pareto na kuwalipa wakulima zaidi ya Sh1,500, atanyang’anywa leseni.
Mhekwa alisema wanunuzi wote wanatakiwa kuwalipa
wakulima kwanza Sh1,500 na kwamba kiasi kingine wawalipe baada ya kupima
uwingi na ubora wa sumu ndani ya siku 30.
Mhekwa alisema kampuni itakayovunja sheria na
kanuni za ununuzi wa pareto msimu huu itafutiwa leseni mara moja na
kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo ,
Chakula na Ushirika ilishaagiza kila mununuzi awalipe kwanza wakulima
Sh1,500 na baada ya kupima ubora wa sumu wawalipe tena malipo ya pili.
Post a Comment