Mathalan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa kikishika nafasi
ya nne kwa ubora wa elimu kwa miaka kadhaa sasa miongoni mwa vyuo vikuu
bora 100 barani Afrika. Je, nafasi hii itaendelea kutetewa na chuo
kinachoiwakilisha nchi kwa miaka michache ijayo?
Kubwa zaidi ya yote, taaluma ya ualimu ni taaluma
ya ajabu yenye sifa bainifu miongoni mwa taaluma nyingine, achilia mbali
suala la kutokuwa na mipaka inayoweza kuonyeshwa kwa urahisi kwa
taaluma.
Ninavyofikiri mimi, asili ya ualimu ni suala la
kiroho. Kufundisha ni zaidi ya kile kinachofikiriwa na watu wengi;
kitendo cha mwalimu kusimama mbele ya wanafunzi darasani na kuwafunza
yale masomo yaliyopangwa. Hata hivyo ili hilo lifanyike kwa ufanisi
linawezeshwa na uwepo wa hali fulani ndani ya mwalimu.
Hali hii ndiyo humwezesha mwalimu kuwa tayari,
huru na aminifu (genuine) kutoa kile kinachotakikana kwa maendeleo ya
ubongo wa mwanafunzi. Kwa kuwa kazi kuu ya mwalimu ni kumsaidia
mwanafunzi na kumpa mwelekeo fulani, kunahitajika umakini wa hali ya juu
sana ambao utategemea hali aliyo nayo mwalimu.
Huu ndiyo uamilifu mkuu wa mwalimu kwa jamii
kwamba ni kulea na kumpa mwelekeo ubongo au tunu za asili za mwanafunzi
(mwanadamu). Hivyo kama mchakato na kanuni hii vikikosewa tayari mtoto /
mwanafunzi atafuba.
Ndiyo maana utasikia watu wengi wakilalamika kuwa
siku hizi watoto hawafundishwi sawasawa, walimu hawatekelezi wajibu wao
sawasawa. Anayeijua siri ya urembo ni mwalimu. Mhadhiri wangu mmoja siku
moja alionyesha hisia zake juu ya mwenendo wa elimu nchini wakati
alipokuwa anatoa somo alisema kuwa ana uhakika miaka 50 ijayo hatokuwa
hai ili ashuhudie taifa la ajabu ambalo watu wote hawatakuwa tena na
uwezo wa kiakili tangu viongozi wao hadi watoto wadogo. Kwa sababu
kanuni za elimu zimekiukwa.
Madhara mabaya ya elimu ( walimu) hayaonekani
kirahisi kwani yanafanya kwa mbinu za hali ya juu sana. Ni mchakato
unaofurukuta chinichini. Ukifikia hali ya kuonekana waziwazi haiwezekani
kirahisi kuzuilika ambapo vizazi kadhaa itakuwa vimekwisha haribikiwa
tayari. Ni suala la ndani la kisaikolojia. Tiba yake ni kutibu
saikolojia ya mwalimu na wala sio kumtishia au kugombana naye.
Na mara nyingi mtu anayejiamini kuwa na madhara
makubwa si mpigaji wa kelele sana. Akisema ukweli atapingwa
anachokifanya anakaa kimya na kutekeleza uaminifu wake. Jambo hili pia
linakwenda nje ya uwezo wa uzalendo alionao. Ni nguvu ya ndani mwake.
“Unafikiri ni nani kati ya daktari na mwalimu ana
madhara makubwa na mabaya zaidi akitoweka katika jamii?” elimu ni uwanja
mpana sana ambao si rahisi kuuzungumzia kwa wakati mmoja.
Kwa dhana hiyo utakubaliana na mimi kuwa ‘UHAI WA
TAIFA LOLOTE UMO MIONGONI MWA MWALIMU’. Mwalimu ni kundi la watu ambaolo
ndilo huamua tabia na mwelekeo wa Taifa lolote”.
Hivyo ningeshauri kuwa suala zima la elimu ndani
liachiwe kwa wadau husika, walimu wakiwa ndio kiini cha suala hili.
Serikali na vyombo au wadau wengine wabaki kuwa wawezeshaji wa wataalamu
hawa, ili watekeleze wajibu wao kwa furaha na waaminiwe kwani ndio
waliopewa wito huu muhimu wa kuandaa taifa.
Walimu nao kwa upande wao wautafakari wito wao vema.
Ninalopenda kusisitiza ni kwamba; ualimu usitafsiriwe kama kazi yakuhamisha ujuzi alionao wa masomo kama Hisabati, Kiswahili nk.
Mwandishi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu 0752 – 480824
Post a Comment