Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa amemtaka Rais Jakaya Kikwete kujitokeza hadharani
kutafuta suluhu ya kupata mwafaka wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa
hakuna mamlaka nyingine zaidi inayoweza kuunusuru.
Pia, amewatahadharisha viongozi wa dini kuwa
makini na kauli zao wanazozitoa za kuwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) kurejea bungeni Agosti 5.
Dk Slaa aliyasema hayo juzi katika mahojiano
maalumu na gazeti hili, makao makuu ya Chadema Mtaa wa Ufipa, Kinondoni
jijini Dar es Salaam.
“Mwenye rungu la kuweza kutengua kitendawili hiki
ili turudi bungeni ni Rais (Kikwete) mwenyewe, hakuna mwingine,”alisema
Dk Slaa.
“Tatizo aliyesaini waraka uliowasilishwa na
Warioba ni Rais mwenyewe, alisaini ukurasa wa kwanza na wa mwisho, kwa
taarifa rasmi za kina Warioba, Rais alishirikishwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba hatua kwa hatua na kwa kila hatua alisema sawa mchakato
uendelee,”alisema Dk Slaa.
Alikumbusha kuwa wakati akipokea Rasimu ya Pili ya
Katiba, Rais Kikwete alisema: “Mtapata rasimu, ijadilini na itapitishwa
na Bunge. Kwa mwanasheria yeyote, lugha kujadiliwa na kupitishwa haitoi
ruhusa ya kubadilishwa, inatoa ruhusa kuboreshwa. Ndiyo utaratibu wa
sheria zote duniani.”
“Sasa anapofika mahali anayeleta wazo ni Rais,
lakini kwa bahati mbaya anayekwenda kupindua pia ni Rais na amekwenda
mbali zaidi kiasi cha kusema kwamba kama Serikali tatu ile ile ambayo
yeye ameisaini itapatikana, jeshi litapindua nchi.
“Anayezungumza ni Rais, hakuna mamlaka nyingine
inayoweza kutengua kitendawili hiki. Wanaweza kuja maaskofu,
...masheikh, asasi mbalimbali... hatimaye hakuna anayeweza kutengua kwa
sababu aliyeufanya ni mwenye mamlaka ya juu,”alisema.
Dk Slaa aliyewahi kuwa Mbunge wa Karatu kwa
vipindi tofauti alitaja mambo matano anayopaswa kuyafanya Rais Kikwete
ili wajunge wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Ukawa waweze kurejea
bungeni.Aliainisha la kwanza ni majadiliano kuwa na misingi iliyo wazi
akisema Ukawa haipo tayari kufanya mambo na kuishia kupewa pipi na
kwamba Katiba Mpya lazima ipatikane kwa maridhiano.
Alitaja jambo la pili kuwa ni lazima wao , Ukawa
wahakikishiwe kuwa kanuni hazichezewi baada ya kupitishwa na siyo kama
ilivyofanya CCM, baada ya Ukawa kutoka bungeni akisema hatua hiyo ni
sawa na uhuni. Lingine ni kuhakikishiwa kitakachojadiliwa ni rasimu
iliyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba si kingine.
Huku akitoa mfano wa hotuba ya Mwalimu Julius
Nyerere ya Juni, 1965 akisema ndiyo iliyowajibu CCM kuhusu msimamo wa
Serikali mbili waliodai ni kuenzi aliyoanzisha Nyerere, Dk Slaa alisema;
“Itakuwa upumbavu kama watu wataamini kwamba
katiba haibadiliki, hata kama imedhihirika kuwa haitoshelezi tena haja
ya wananchi kwa wakati ule.”
Alihoji kwamba ikiwa Mwalimu Nyerere alitoa kauli hiyo kipindi
hicho ni nini msingi wa CCM kuendelea kung’ang’ania hoja zao wakidai
kudumisha misingi yake (Nyerere). Alifafanua kuwa kimsingi katiba
hubadilishwa kwa haja mbalimbali za wananchi akitaja baadhi yake kuwa ni
za kijamii, kiuchumi, kifedha.
“Kikwete ndiye mwenye rungu la Katiba Mpya,
achukue nafasi yake kama mkuu wa nchi na siyo kama mwenyekiti wa
CCM...Rais wa nchi hapaswi kuwagawa Watanzania na wala hatakiwi
kuonyesha tofauti kama alivyofanya yeye alipozindua Bunge,” alisema.
Aliongeza: “Arudishe mchakato katika reli, aite
wadau wakiwamo Ukawa na asipofanya hivyo msimamo wetu ni ule ule wa
kusimamia na kutetea maoni ya wananchi waliyoyatoa.”
Hakuna haraka ya Katiba
Hata hivyo, Dk Slaa alisema kuwa hakuna haja ya
kukimbizana kupata Katiba Mpya kwa kutaka kulazimisha iweze kutumika
katika uchaguzi mkuu ujao mwakani, akihadharisha kuwa hilo likifanyika
haitapatikana katiba bora.
Alisema kuwa awali, Rais Kikwete aliwatangazia
Watanzania kwamba Katiba Mpya ingepatikana Aprili 26 mwaka huu katika
maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, lakini ameshindwa kutimiza ahadi
hiyo.
“Hata kama ikipatikana (Katiba) Machi au Aprili
mwakani, bado haiwezi kutumika katika uchaguzi huo kwani kutakuwa na
utaratibu wa kufumua sheria zote hizo ili zifanye kazi kama Katiba
inavyoelekeza, jambo ambalo haliwezi kutekelezwa kwa kipindi kifupi,”
alisema.
Alisema kuwa kinachotakiwa sasa ni Bunge kufanya
marekebisho ya katiba iliyopo ya mwaka 1977 katika vipengele viwili ili
kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika ukiwa huru na haki.
Alivitaja vipengele hivyo kuwa ni suala la kuwapo
kwa Tume Huru ya Uchaguzi na rais kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 52
ya idadi ya wapigakura.
“Huwezi kuongoza taifa ambalo hukuvuka asilimia 50
ya kura zote, mfano mwaka 2010 Kikwete waliomchagua hawafiki robo ya
waliopiga kura, sasa, jambo hili linahitaji kufanyiwa marekebisho,”
alisema.
Aliongeza: “Rais anaweza kuwa na dhamira nzuri,
lakini kuna wanachama ndani ya CCM ambao hawapendi katiba ipatikane
katika kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete na yeye hafanyi uamuzi wake
bali husukumwa na wanaomzunguka, wanaotamani utawala.”
Atahadharisha viongozi wa dini
Kuhusu viongozi wa dini kuwataka Ukawa unaoundwa na vyama vya
Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kurejea bungeni, katibu mkuu huyo wa
Chadema alisema, maaskofu wanatakiwa kuwa makini kabla ya kutoa kauli
hizo.
Alisema kilichowatoa Ukawa bungeni ni kutokufuatwa
kwa misingi ya mjadala wa katiba na maoni ya wananchi kudharaulika na
kuanza kujadiliwa kwa Rasimu ya CCM.
“Maaskofu wangu hawajui kilichomo bungeni, hoja
yetu ni je, tunarudi tutajadili rasimu iliyopo mezani? Hatuwezi kukubali
kuona rasimu ikichakachuliwa.
“Viongozi wangu wa dini nawapenda sana, ila
nawasihi wasiingie katika hili kwani litakuja kuwahukumu siku ya mwisho
kwa kutoa kauli ambazo hawajafanyia utafiti,”alisema.
Aliongeza: “Wakumbuke, katika Biblia kuna maandiko
yanasema; yeyote anayewapotosha wadogo, anastahili kufungiwa jiwe
shingoni. Wabunge wanapotoka bungeni wanajali wakitaka sauti ya wanyonge
isikike, waliotutuma wanataka haki itendeke.
“Ukawa inapinga ‘dictatorship of the
majority’(Udikteta wa wengi). Tunachofanya ni njia halali ya mapambano
inayoweza kutumika dunia nzima, pale wengi wanapogeuka madikteta.”
Julai Mosi, Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki
Tanzania (TEC), liliwataka Ukawa kurudi bungeni bila masharti na
kuendelea na mjadala wa Katiba Mpya kwa manufaa ya taifa.
Pia, Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of
God (TAG), Jimbo la Mashariki Kaskazini, Geoffrey Massawe aliomba
wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuungana na kuwa kitu kimoja katika
mchakato huo wa Katiba.
Askofu Massawe alitoa ombi hilo wakati wa ibada
maalumu ya sherehe ya maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa
kanisa hilo nchini iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kinondoni, Dar es
Salaam.
Akitoa salamu za TEC wakati wa kuadhimisha miaka
25 ya uaskofu wa Tarcisius Ngalalekumtwa kwenye Uwanja wa Kichangani,
Iringa, Makamu Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi alisema ni vyema
wajumbe hao wakarudi kwenye bunge hilo linalotarajia kuanza Agosti 5,
mwaka huu.
“Ninatumia neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee
bungeni mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au kufanya mizengwe mingine na
kutupatia Katiba Mpya isiyotufaa, nitawaomba Watanzania wote tuweke
uzalendo mbele na kuikataa rasimu ya Katiba itakayoletwa pia tuwanyime
uongozi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Nguvu ya Chadema
Katibu Mkuu huyo alisema chama hicho hivi sasa kina nguvu nchi
nzima kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu hivyo kinaweza kupambana vyema
na CCM.
Alisema wamekuwa wakitumia ruzuku wanayoipata
kutoka serikalini ya Sh233 milioni kila mwezi kupeleka vitendea kazi
katika majimbo na kanda.
“Tuliamua kufanya hivyo kwani tulivyokuwa
tukipeleka fedha walikuwa wakizigombania na mpaka sasa kanda kumi zina
gari moja moja na wilayani kuna pikipiki moja pamoja na kompyuta.
“Yaani, sasa hivi kama CCM ina wachezaji 11
uwanjani nasi (Chadema) tunao wachezaji 11 ni tofauti na ilivyokuwa
mwanzo hivyo mpira unachezeka sawasawa,” alisema.
Aliongeza kuwa kanda na majimbo yanajiendesha
kwani wamepeleka zaidi ya kadi milioni 75 ambazo kila kadi ni Sh1500 na
ada ni Sh1,000 hivyo fedha hizo zinaweza kuendesha ofisi hizo bila
kutegemea fedha kutoka makao makuu.
Ofisi ya Zitto
Akizungumzia kubadilishwa kwa matumizi kwa ofisi
ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Dk Slaa alisema amefanya
hivyo kutokana na mhusika kutoitumia kwa muda mrefu.
“Nimefanya hivyo kwani siwezi kuiacha ofisi ikakaa
bila mtu wakati kuna watu wangu hapa wanabanana na hata mkipita mtaona
nimebadili matumizi ya ofisi,” alisema Dk Slaa.
Post a Comment