Kwa siku kadhaa sasa, gazeti hili
limekuwa likichapisha makala kuhusiana na madhila yaliyompata msichana
mmoja mkazi wa Dar es Salaam, aliyepelekwa nchini China na mtandao wa
watu wanaofanya biashara ya kusafirisha binadamu, lakini akaishia
kutumikishwa katika madanguro mbalimbali badala ya kupewa ajira katika
hoteli kubwa kama alivyokuwa ameahidiwa. Msichana huyo ambaye
hatutamtaja jina kwa sababu za kimaadili sasa amerudi nchini akiwa
ameathirika kimwili na kisaikolojia, baada ya kuwatoroka watu waliokuwa
wamemrubuni na kumuweka utumwani kwa miezi mitatu hivi.
Msichana huyo ambaye kabla hajapelekwa utumwani
nchini China alikuwa na matumaini ya mafanikio katika maisha yake.
Hivyo, alipokutana na wanawake hao hapa jijini Dar es Salaam, ambao
hakujua walikuwa sehemu ya mtandao wa wafanyabiashara ya kusafirisha
binadamu hakuwatilia shaka hata kidogo, kwani aliamini walikuwa na nia
ya kumsaidia kutimiza ndoto yake ya kupata ajira nzuri za kimataifa nje
ya nchi. Hakuwahi kufikiria kwamba wanawake hao walikuwa wakimpeleka
kudhalilishwa utumwani, bali pia kufanya kazi ambazo malipo yake
yalikuwa yanakwenda moja kwa moja kutunisha mifuko ya wanawake hao na
mawakala wao nchini China.
Ni simulizi zinazotia uchungu mkubwa ambazo
zinathibitisha kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu imeshamiri
hapa nchini, huku Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama
vikionekana kutojua ukubwa wa tatizo wala wapi pa kuanzia. Pamoja na
maumivu aliyonayo, msichana huyo anasema ameamua kujitokeza na
kuzungumzia mkasa huo ili mamlaka husika za hapa nchini na za kimataifa
ziingilie kati na kukomesha biashara hiyo ambayo anasema imewakumba
wasichana wengi kutoka Tanzania ambao wengi wameshindwa kujikwamua.
Ni simulizi pia zinazoonyesha kwamba mifumo ya
kiserikali na kiutawala hapa nchini haifanyi kazi kama ilivyotarajiwa
kutokana na kuwapo janga la rushwa na ufisadi miongoni mwa watendaji
wengi serikalini na taasisi zake. Tunajiuliza jinsi mitandao ya biashara
hiyo inavyoweza kuwaweka watendaji hao mifukoni kiasi cha kutoa viza na
pasi za kusafiria kwa vijana ambao hawana uwezo kifedha wala sifa za
kupata ajira mahali popote. Inashangaza kuona mitandao hiyo ikifanya
biashara hiyo kiulaini pasipo vyombo na mamlaka husika kushtuka.
Makala tulizochapisha kuhusu msichana huyo ndizo
zimevishtua vyombo vya dola. Sasa tunaambiwa kwamba Shirika la Polisi la
Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania limemhoji msichana huyo kwa
zaidi ya saa 11 likitaka kujua jinsi safari yake hiyo ilivyokuwa na
namna wanawake waliowasafirisha kwenda China walivyosuka mipango hiyo.
Ofisi hiyo ya Interpol imekiri kumhoji msichana huyo na kusema lengo ni
kufahamu kwa undani jinsi Watanzania wanavyotumikishwa katika madanguro
hayo, pamoja na kujua jinsi biashara hiyo inavyofanyika kati ya China na
Tanzania.
Angalizo letu kwa Serikali ni kwamba iamke na
kuchukua hatua, kwani biashara hiyo haiko tu kati ya Tanzania na China,
bali kati yake na nchi nyingi za Kiarabu, Ulaya, Asia, Amerika na hata
Afrika. Ni biashara kubwa inayoendeshwa na mtandao mpana wa genge la
wahalifu wa kimataifa. Msichana huyo sasa anaishi kwa woga baada ya
kutishiwa kifo na wanawake waliompeleka China na baadaye kutoroka na
kurudi hapa nchini. Tumetiwa moyo na Tamwa pamoja na kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), ambavyo vimeanza kuchukua hatua za kumsaidia.
Post a Comment