Msemo usemao ‘Wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho atakuwa
wa kwanza’ unatosha kuelezea shule maarufu ambazo zimeporomoka kielimu
kwa miaka ya hivi karibuni.
Miaka ya nyuma shule za ufundi na za vipaji
maalumu zilisifika kwa kutoa elimu bora na wanafunzi wake kufanya vizuri
katika mitihani yao lakini leo hii imekuwa kinyume.
Kwa mfano shule kama Ilboru, Mzumbe, Jangwani,
Pugu, Uru Seminary, Tabora Boys, Iyunga, Azania, Zanaki, Kilakala,
Ifunda Girls, Consolata Seminary, Kifungilo Girls na Tambaza zimefanya
vibaya katika Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika Mei
mwaka 2014.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Shule ya
Sekondari ya Tambaza iliyopo Ilala, Dar es Salaam ni ya tatu kati ya
shule 10 za mwisho katika matokeo ya mtihani huo.
Historia ya shule hii kuanzia miaka ya 1990 hadi
2000 inaonyesha kwamba Tambaza ilikuwa miongoni mwa shule zilizokuwa
ziking’ara kwa kushika nafasi za juu katika matokeo ya mitihani ya
kidato cha nne na sita.
Aibu hii imeikuta shule ambayo iko katikati ya
Jiji kilomita chache kutoka yalipo makao makuu ya wizara yenye dhamana
ya kusimamia elimu nchini pamoja na taasisi zake.
Tambaza ni kati ya shule zilizosifika kielimu
katika Jiji la Dar es Salaam hasa miaka 1990. Baada ya hapo, vurugu za
wanafunzi zilisababisha kufutwa kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na
kubakiza kitado cha tano ba sita tu.
Mkuu wa Shule
Mkuu Shule hiyo, Hussein Mavumba anasema taarifa za kufanya vibaya kwenye matokeo hayo ni za kushtusha ambazo hawakuzitarajia.
“Ni mapema sana kusema chochote.Bado siamini na
imetuchanganya sana, tunafanya uchunguzi kubaini hasa tatizo ni nini ,”
anasema na kuongeza:
“Nitatakaa na walimu wangu na tutafanya uchunguzi
wa kisayansi kuchunguza nini kilikosewa hadi kusababisha matokeo haya
lakini siyo rahisi kuamini hiki kilichotokea”.
Kwa upande wake, mtangulizi wa Mavumba aliyekuwa
mkuu wa shule hiyo kuanzia 2004 mwishoni hadi 2009, Nicolas Buretta
anasema utandawazi umechangia wanafunzi kufanya vibaya.
Buretta ambaye sasa ni Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya
Morogoro anasema Tambaza ni shule ya kutwa hivyo wazazi na walezi
wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuwasimamia ipasavyo.
“Shule hii ni ya kutwa na mzazi au mlezi anatakiwa
kuwa karibu na mwanaye kwani wanaporudi nyumbani unakuta anatumia simu
kuchati na rafiki zake hadi usiku wa manane badala ya kusoma na kufanya
mazoezi ya nyumbani na mwisho wa siku ndiyo hayo yaliyotokea,” anasema
Buretta.
Anaongeza: “Nikiwa mkuu pale nilitengeneza kitu
kama mafiga matatu yaani walimu, wazazi na wanafunzi lakini nilisisitiza
nidhamu ya hali ya juu kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake na hiyo
ndiyo ilikuwa siri ya mafanikio yangu.”
Buretta anasema wanafunzi wa sasa ni tofauti na wa
miaka ya nyuma wengi hawataki kutimiza wajibu wao na mzazi asipokuwa
makini matokeo ya wanafunzi yataendelea kuporomoka.
“Mzazi, mwanafunzi, mwalimu na Bodi ya shule ambao
ndiyo wasimamizi wa shule watimize wajibu wao kila mmoja na wakifanya
hivyo Tambaza itarudi sehemu yake kama ilivyokuwa nyuma,” anasema
Buretta.
Ilianza kuporomoka 2010
Takwimu zinaonyesha kuwa Tambaza ilianza
kuporomoka 2010 na imeendelea hivyo kwa miaka mitatu mfululizo, hadi
ilipojikuta katika kundi la shule kumi za mwisho kwenye matokeo ya mwaka
huu.
Matokeo ya 2010 ni daraja la I-19, II-66, III-215,
IV- 91 na waliofeli walikuwa 89. Kimkoa ilikuwa ya 40 kati ya shule 50
huku kitaifa ilishika nafasi ya 290 kati ya 337.
Mwaka 2011 matokeo yalikuwa daraja la I-15, II-51,
III-189, IV-84 na waliofeli walikuwa 88. Kimkoa ilishika nafasi ya 28
kati ya shule 41 na kitaifa ilikuwa ya 282 kati ya shule 334.
Matokeo ya 2012 yanaonyesha kuwa daraja la I-12, II-71, III-235, IV-89 huku waliofeli wakiwa 91.
Kimkoa ilishika nafasi ya 30 kati ya 35 na kitaifa ilishika nafasi ya 270 kati ya shule 326
Mwaka huu 2014 daraja la I-4, II-28 , III-130 ,
IV-109 , waliofeli walikuwa 44. Kitaifa ilikuwa ya 266 kati ya 328
akimaanisha ilikuwa ya tatu kati ya shule 10 za mwisho.
Hali hii inaonyesha kwamba Tambaza haikufanya vibaya mwaka huu pekee bali ni mwendelezo wa matokeo kushuka tangu mwaka 2010.
Wanafunzi wasikitika
Wanafunzi wa shule hiyo ambao hawakupenda kutajwa majina yao wanasema, ni taarifa zilizowasikitisha na kutokujua hatima yao.
“Shule hii inafundisha masomo ya sayansi lakini
walimu wenyewe hawapo na hata vifaa vya maabara hakuna, tatizo hili
najua litakuwa limechangia kwa kiasi fulani,”alisema mmoja wa wanafunzi
hao na kuongeza:
“Serikali inatakiwa kuangalia na kuchunguza nini
tatizo kwani ikiachwa hivi hivi inaweza kuifanya Tambaza ikawa shule
itakayoshika mkia 2015 kwani walimu nao kufundisha kwao ni tatizo.”
Kauli za wadau
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Hakielimu,
Godfrey Bonaventure anasema ni jambo la kushangaza kwa shule iliyokuwa
ikisifika kuwa ya vipaji leo inafanya vibaya.
Shule hiyo kufanya vibaya inawezeka ni masuala ya
utawala kutokuwa karibu na wanafunzi na kutokutekeleza majukumu yake
ipasavyo hasa suala la nidhamu kwa kila mmoja.
“Nina hakika Tambaza ina walimu wengi lakini je,
wanafundisha, maabara iliyokuwapo je, inajitosheleza na vifaa vyake. Ina
vitendea kazi na mwisho usimamizi unatekelezeka ipasavyo? Haya ni mambo
ambayo nina hakika yanahitaji kupatiwa ufumbuzi,” anasema Bonaventure.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu
Tanzania (CWT), Ezekiel Olouch anasema tatizo linaweza kuwa katika
vitendea kazi na kushuka kwa morali ya walimu kufundisha.
“Tambaza ina wanafunzi wengi lakini je, walimu
wanatosha? Vitendea kazi vipo inahitaji kuangaliwa nini kimeifanya
kuporomoka na siyo kuinyooshea tu kidole,” anasema Olouch aliyefundisha
shule hiyo miaka ya 1990.
Mkazi wa Jijini Dar es Salaam, Alex Msafiri
anasema kinachoitokea Tambaza ni mwendelezo wa shule maarufu kufanya
vibaya na serikali inatakiwa kuzitupia macho kwa kutatua changamoto
inazozikabili.
“Ukiangalia hata Mzumbe, Ilboru, Kifungilo, Azania, Jangwani,
Makongo ni shule ambazo zilikuwa zinawika lakini leo hii zinafanya
vibaya, hivyo kunahitajika uchunguzi kubaini tatizo ni nini. Madeni ya
walimu nayo yanapaswa kutazamwa kwani inawezekana ni chanzo cha walimu
kutotekelea majukumu yao, hivyo kuwaumiza wanafunzi,” anasema Msafiri.
Kwa umaarufu na ukongwe wake, ni dhahiri wapo watu
wenye nafasi nzuri katika jamii ambao ni mazao ya Tambaza. Hawa
wanaweza kutafutwa na kushirikishwa katika mikakati ya kuepusha shule
hii dhid ya aibu kubwa zaidi.
Post a Comment