Dar es Salaam. Serikali
imesema imefanikiwa kudhibiti matumizi yasiyofaa ya tindikali baada ya
kuweka utaratibu unaowaruhusu watu walioorodheshwa tu kununua kemikali
hiyo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkemia Mkuu
wa Serikali, Profesa Samwel Mnyele alisema utaratibu mpya wa kuzuia
kila mtu kuuziwa tindikali umesaidia kupunguza matumizi mabaya ya
kemikali hiyo.
Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) uliandaa
utaratibu wa kuhakikisha watu wote wanaotumia tindikali kwa ajili ya
shughuli mbalimbali wanaorodheshwa.
“Tulihakikisha watu mbalimbali, wakiwamo wanaotoa
elimu ya ujasiriamali wa kutengeneza sabuni na bidhaa nyingine,
wanajiorodhesha,” alisema.
Alisema wakufunzi ndio wanaouziwa tindikali hiyo na wao wanaigawa kwa walengwa.
Alisema mamlaka inatambua umuhimu wa tindikali kwa
ajili ya wajasiriamali na marufuku pekee yake isingekuwa na maana,
badala yake imeweka utaratibu utakaowezesha udhibiti.
“Pia elimu juu ya matumizi ya tindikali imesaidia.
Mpango huu ni endelevu. Sheria inakuja itakayosaidia kuwepo kwa
matumizi sahihi ya kemikali na ukaguzi wa vyakula na dawa,” alisema.
Post a Comment