Wachezaji wakiwa katika mechi ya mpira wa kengele katika mashindano ya
Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (Umisseta)
iliyofanyika Kibaha, Pwani hivi karibuni. Picha na Imani Makongoro.
“Kabla ya kuanza mechi, kocha unatakiwa kumchukua mchezaji mmoja
mmoja na kumzungusha eneo zima la uwanja kwa dakika 30, tunafanya hivyo
ili kumjengea mchezaji hali ya kuzoea mazingira ya uwanja kabla ya
kucheza,” anasema kocha wa mpira wa kengele, Hashiru Tembo
Anasema wachezaji hupelekwa kila sehemu ya uwanja
utakaotumika kwenye mechi hiyo, ambazo ni kwenye goli wanalotakiwa
kufunga na kwenye goli lao kwa ajili ya kuzuia na mwisho wa uwanja, pia
katikati ili kung’amua urefu na ukubwa wa uwanja watakaoutumia.
Mpira wa kengele au ‘Goal ball’ ni mchezo
ulioanzishwa na raia wa Australia, Hanzi Lorenzen na raia wa Ujerumani,
Sepp Reindle mwaka 1946 kwa ajili ya kuwasaidia askari waliopigana vita
ya pili ya dunia na kupata matatizo ya macho.
Kwa mara ya kwanza nchini mchezo huu umechezwa
kwenye mashindano ya 20 ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za
Msingi Tanzania (Umitashumta) ya msimu huu kwenye viwanja vya Shirika la
Elimu Kibaha, Pwani.
Mpira wa kengele unavyochezwa
Hashiru Tembo ambaye ni kocha wa mchezo huo
anasema mpira wa kengele unachezwa na wachezaji wasioona (vipofu) na
wenye uoni hafifu ambao kabla ya kuanza kwa mechi wote huvaa vitambaa
vyeusi kuziba macho kwa ajili ya kuzuia wale wenye uoni hafifu kutoona
kabisa ili kuendana na wenzao (vipofu).
Timu nzima ina wachezaji wangapi?
Tembo anasema kila timu inasajili wachezaji wanne,
ambao kati yao watatu wanakuwa kwenye kikosi cha kwanza na mmoja
anakuwa mchezaji wa akiba, wanaoanza mmoja anakuwa mchezaji wa kati na
wachezaji wawili wa pembeni.
“Mchezaji wa kati mara nyingi anakuwa yule mwenye
hisia za haraka za kubaini mpira pale unapokuwa umerushwa golini kwao na
anapoudaka hatakiwi kuugusa zaidi ya mara mbili, akishagusa mara mbili
anapaswa kumpa mchezaji wa pembeni akigusa mara ya tatu hiyo ni faulo,”
anasema Tembo.
Anasema mchezaji wa kati ambaye ni muhimu kwa
ulinzi anapougusa mpira kwa kuwa ni mchezo wa wasioona, anapaswa kufanya
ishara ya kugusa mpira kwa nguvu kidogo ili kengele itoe sauti
kumwashiria yule wa pembeni kuwa anampa pasi.
“Akiugusa mara ya tatu hiyo ni faulo, na faulo za
mpira wa kengele ni kupigwa kwa penati, wakati wa upigaji wa penati
wachezaji wa pembeni wanapaswa kutolewa na kubaki yule wa kati peke
yake,” anasema Tembo.
Anasema mpira wa kengele hauna kona wala mpira wa
kurusha, goli linapofungwa timu iliyofungwa ndiyo inaanzisha mpira
kutoka pembeni mwa goli lao na mchezaji atakayetoa nje mpira unapelekwa
kuanzwa kwenye lango la timu pinzani.
Washangiliaji wanaruhusiwa
Washangiliaji wanaruhusiwa
“Ndiyo washangiliaji wanaruhusiwa kwa sharti la
kuwa watazamaji tu bila kushangilia hadi pale goli litakapoingia ndipo
wanaruhusiwa kupiga makofi tena kwa sekunde chache tu na kukaa,” anasema
Tembo.
Anasema mpira wa kengele hautaki kelele kwani wachezaji wanapaswa wasikie sauti ya kengele wakati mpira unaporushwa.
“Tofauti na michezo mingine timu zinaweza
kushangilia kwa mavuvuzela, ngoma, sauti kali muda wote, lakini kwenye
mpira wa kengele ni kinyume, hakutakiwi kabisa kelele ili kuwapa fursa
wachezaji kusikia kengele ya mpira,” anasema Tembo.
Kwa nini wanachezea kwenye zulia?
Tembo anasema uwanja wa mpira wa kengele unapaswa
kuwa na zulia kwenye magoli ya pande zote mbili ili kuwasaidia wachezaji
kutopata michubuko au majeraha wakati wa mechi.
“Mpira wa kengele unachezwa wakati wachezaji
wakiwa wamepiga magoti ili kuweza kuusikia vizuri mpira unapokuja
langoni kwao, na kawaida uwanja wa mpira wa kengele umesakafiwa kama
vilivyo viwanja vya kikapu na netiboli.
“Tofauti yake ni kwamba uwanja wa mpira wa kengele
unakuwa na magoli kama ya soka, lakini mafupi na mapana, hivyo kapeti
linawasaidia kutoumia kwani mbali ya kupiga magoti, mchezaji anaweza
kujirusha kuelekea anaposikia mlio wa kengele ili kuufuata mpira,”
anasema Tembo.
Anasema mbali na uwanja kuwekewa zulia, pia
wachezaji wote wanapaswa kuvaa vitu vitakavyowasaidia kutopata michubuko
sehemu za magoti na kwenye viwiko vya mikono wakati wa mechi.
Kocha anaruhusiwa kusimamisha mechi?
“Ni kweli kocha anaruhusiwa kusimamisha mpira
(mapumziko mafupi) mara tatu katika dakika zote 24 za mechi kwani mechi
huchezwa kwa dakika 12 kipindi cha kwanza na dakika 12 kipindi cha pili,
akizimaliza haruhusiwi kuomba tena,” anasema Tembo.
Anasema mara nyingi huwa wanaomba mapumziko mafupi
ili kuwaweka vizuri wachezaji wao uwanjani ambapo kuna wakati mchezaji
anaweza kuwa amegeukia pembeni ya uwanja bila kujua wakati mechi
inaendelea.
“Mchezaji anaweza kuwa amegeukia pembeni au anaangalia nyuma ya
uwanja kwa kuwa anakuwa haoni, hivyo kocha anaweza kuomba mapumziko
mafupi na kwenda kumrekebisha na kumuweka vizuri japo mwisho wa kuomba
ni mara tatu,” anasema Tembo.
Mazoezi yao yanafanyikaje?
“Mpira wa kengele ni mzito hivyo wachezaji
wanapaswa kutumia nguvu kidogo katika kuurusha, ili kuendana na mpira
wachezaji huwa wanafanya mazoezi makali ikiwamo ya gym, na kukimbia kwa
ajili ya pumzi,” anasema Tembo.
Anasema, wanapofanya zoezi la kukimbia, yule
mwenye uoni hafifu humshika mkono yule asiyeona kabisa na kuanza
kukimbia naye kwa kuzunguka uwanja wa mpira wa miguu raundi kadhaa au
eneo lolote ambalo kocha anaona linastahili.
Changamoto wanazokutana nazo wachezaji
Aman Fungo ni mchezaji wa mkoa wa Iringa, yeye anasema changamoto kubwa ni ukosefu wa viwanja vya mchezo huo hapa nchini.
“Mara nyingi tunatumia viwanja vya michezo
mingine, kama kwenye Umitashumta tulikuwa tunatumia uwanja wa mpira wa
kikapu ambao upo jirani na ule wa netiboli na wavu hivyo tunapokuwa
tunacheza sisi michezo mingine inasimamishwa au tunatakiwa tucheze
asubuhi sana kabla michezo mingine haijaanza,” anasema Fungo.
Wakati Seleman Omary wa Dodoma anasema, uhaba wa
viwanja na vifaa ni changamoto kwao kwani vinavyotumika viko katika
mazingira ya kelele ingawa mchezo huo hautaki kelele.
“Uwanja wa mpira wa kengele unapaswa kuzungushiwa
uzio ili kuzuia mpira usitoke nje ya eneo la uwanja, lakini viwanja
tunavyovitumia havina uzio na mara nyingi tunatumia vile ambavyo ni
maalumu kwa michezo mingine kwa ujumla sisi hatuna viwanja,” anasema
Omary.
Mchezo huo unavyowasaidia walemavu
Kocha Tembo anasema tangu ulipoanzishwa mpira wa
kengele, walemavu wa macho mkoani Dodoma wamehamasika mno kucheza na
umewajengea kujiamini na kujiona hawana tofauti na jamii ya kawaida.
“Kwanza wamejiona sio tofauti na watu wengine,
wamejenga mahusiano mazuri na wachezaji wengine, lakini pia umewasaidia
kuwa wadadisi na hata maarifa kwao yameongezeka mara dufu kulinganisha
na walivyokuwa awali,” anasema kocha huyo.
« Pr
Post a Comment