Masasi. Rais Jakaya Kikwete amezindua mradi wa
maji wa Mbwinji unaotoa huduma kwa wakazi wilayani hapa na Nachingwea
mkoani Lindi na kulifanya tatizo hilo sugu la ukosefu wa maji lililokuwa
linawakabili wakazi wa wilaya hizo kuwa historia.
Akizindua mradi huo juzi, Rais Kikwete alisema ni
faraja kwake kuweka historia katika tatizo la maji kwenye wilaya hizo
kutokana na yeye mwenyewe kuwa miongoni mwa wananchi walioonja adha
hiyo. “Niliwahi kuishi Nachingwea wakati huo nilikuwa katibu wa CCM wa
wilaya kabla sijahamia Masasi. Mimi ni miongoni mwa walionja adha hii ya
kukosa maji, hivyo niliahidi wakati wa kampeni zangu kuwa nitahakikisha
tatizo la maji Masasi na Nachingwea linakuwa historia na sasa
imewezekana,” alisema Kikwete akionekana mwenye furaha
Aliongeza kusema: “Kazi kubwa iliyopo ni kuilinda
miundombinu hii isihujumiwe, itunzeni ili nanyi iwatunze. Hakikisheni
maeneo ya vyanzo vya maji kule Mbwinji hayaharibiwi, sheria zipo na
ikibidi basi tangazeni kwenye gazeti la Serikali kuwa ni eneo la
hifadhi.”
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa
Mazingira wa Masasi-Nachingwea (Manawasa), Nuntufye Mwamsojo alimwambia
Rais katika taarifa yake kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza Februari 2011
na kuligharimu taifa Sh31 bilioni.
Alibainisha kuwa mradi huo utanufaisha wakazi
102,696 wa Mji wa Masasi na kwa sasa wakazi 83,128 (sawa ana asilimia
81) wamefikiwa na huduma hiyo, wakati katika Mji wa Nachingwea wakazi
77,207 (sawa na asilimia 64) wamefikiwa na huduma hiyo.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe
alimpongeza Rais kwa kuwekeza nguvu zake katika mradi huo na kumwomba
jitihada kama hizo zifanywe katika miradi mingine pia. “Mheshimiwa Rais
katika bajeti ya mwaka jana nilipangiwa Sh600 bilioni hadi mwaka unaisha
nilipewa Sh140 bilioni tu. Hii ndiyo sababu miradi mingi ya maji
imekwama,” alisema Maghembe.
Post a Comment