Ngeli ni vikundi vya majina ya Kiswahili. Ngeli za nomino ni
utaratibu unaotumika kuweka nomino katika matabaka au makundi
yanayofanana.
Kufahamu ngeli za Kiswahili kunamwezesha
mwanafunzi kuelewa upatanisho wa kisarufi katika sentensi, kutambulisha
maumbo ya umoja na uwingi pia kufahamu uhusiano wa Kiswahili na lugha
zingine.
Ngeli ya A–WA hutumika kurejelea viumbe vilivyo
hai (wanyama na watu). Majina mengi katika ngeli ya A-WA huanza kwa
sauti M- kwa umoja na sauti WA- kwa wingi. Hata hivyo baadhi ya majina
huchukua miundo tofauti.
Mifano; mgonjwa - wagonjwa, mchungaji - wachungaji, mwizi-wezi, mtu- watu.
Muundo ulio tofauti na maelezo hapo juu ni kama
mbuzi-mbuzi, kwale - kwale, nyati - nyati
kifaru – vifaru.
Ngeli ya LI-YA husimamia nomino zenye miundo
mbalimbali. Licha ya majina ya vitu visivyo hai, ngeli hii pia hutumika
kwa majina yote katika hali ya ukubwa (yakiwamo ya watu au wanyama).
Majina mengi huanza kwa JI- au J- kwa umoja na hubadilishwa kuanza na
MA- au ME- kwa wingi. Majina mengine ambayo huanza kwa sauti nyingine
kama vile /b/, /d/, /g/, /k/, /z/ n.k ambayo huwekwa katika wingi kwa
kuongeza kiungo MA-
Mifano; jimbo - majimbo, jicho - macho, jiko -majiko, jino - meno, maua, umbo - maumbo, bati - mabati.
Ngeli ya KI - VI hurejelea vitu visivyo hai ambavyo majina yao huanza kwa KI- au CH- (umoja) na VI- au VY- (wingi).
Mifano; kijiko - vijiko, kikapu - vikapu, kioo- vioo,
choo - vyoo, chumba - vyumba, chuma - vyuma, chungu - vyungu
Ngeli ya U - I huwakilisha nomino za vitu visivyo hai na ambavyo majina yake huanza kwa sauti M - (umoja).
Mifano; mfupa - mifupa, mtambo - mitambo, mfuko – mifuko.
Ngeli ya U - ZI hurejelea majina ambayo huanza kwa U- (umoja) na huchukua ZI- kama kiambishi kiwakilishi cha ngeli katika wingi.
Mifano; ufunguo - funguo, ukuta – kuta.
Majina ya silabi mbili katika ngeli hii huongezwa NY katika uwingi. Mifano; uzi - nyuzi, uso – nyuso.
Ngeli ya I - ZI hutumiwa kwa majina yasiyobadilika
kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti:
I- (umoja) na ZI- (wingi). Aghalabu haya ni majina ya vitu ambayo
huanza kwa sauti N, NG, NY, MB, n.k
Mifano; nyumba - nyumba, nguo - nguo, mbegu - mbegu, nyasi - nyasi, nyama – nyama.
Ngeli ya U - YA hujumuisha nomino ambazo zina kiambishi awali u-katika umoja na ma- katika uwingi.
Mifano; unyoya - manyoya.
Ngeli ya KU huwakilisha majina yanayotokana na
vitenzi kwa vitenzi vinavyoanza na ku-(huitwa vitenzi jina). Mfano
Kusoma kwetu kumetusaidia, Kusema uongo kumemponza.
Ngeli ya mahali PA - KU – MU. Ngeli ya PA
hurejelea mahali maalumu, padogo au palipo wazi. Ngeli ya KU hurejelea
mahali fulani kwa jumla au eneo fulani. Ngeli ya MU - hutumika kurejelea
mahali ndani ya kitu kingine kama vile ndani ya nyumba, shimo n.k.
Ngeli za mahali hubaki vivyo hivyo katika umoja na wingi
Hivyo, mwanafunzi anaweza kufanya mazoezi kadiri
awezavyo kwa kutunga sentensi umoja na uwingi kwa kutumia neno au
kitenzi jina ili kubaini kundi husika la neno au maneno.Mwandishi ni mtaalamu wa Kiswahili.
Post a Comment