Ni jambo la kawaida kwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi au
sekondari kutokuwa na ustadi wa maisha hasa wa kujitegemea na kuepuka
kuwa tegemezi kwa wazazi au walezi wao.
Hali hii inasababisha ongezeko la vijana wengi
mitaani wasio na kazi na kubaki wakirandaranda mitaani wasijue la
kufanya. Miongoni mwao, wamo wahitimu wa elimu mpaka vyuo vikuu.
Elimu isiyowezesha mhitimu kuwa na uwezo wa
kujitegemea, wengi wanasema ni matokeo mabadiliko ya mara kwa mara
katika mfumo wake ambao hivi sasa unaweka mkazo zaidi katika nadharia
badala ya vitendo. Elimu ya nadharia haimwezezi muhitimu kuweza
kujitegemea kwa kufanya shughuli kama kuwa mkulima, fundi nguo, viatu au
mfanyabiashara.
Baadhi ya wadau wa elimu walioshiriki kwenye
kongamano lililiofanyika Dar es Salaam kujadili mada isemayo ‘Elimu ya
Tanzania, wanasema mfumo wa elimu unahitaji kuboreshwa ili uweze
kuendana na matakwa ya jamii na taifa kwa jumla. Profesa wa Chuo Kikuu
cha Ardhi, Alphonce Kessy anasema kitendo cha wanafunzi kuhitimu elimu
ya msingi au sekondari wakiwa hawezi kujitegemea ni jambo la hatari.
Anasema elimu inayotolewa kwa wanafunzi kuanzia
darasa la kwanza anafundishwa jinsi ya kulima mbogamboga au useremala
kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Anasema shule zimeongezeka lakini vitendea kazi
vya kufundishia na kujifunza bado ni vichache jambo linalorudisha nyuma
ufanisi wa utoaji wa elimu kwa walimu.
“Mfumo wetu wa elimu unahitaji kuangaliwa ili
mwanafunzi anapohitimu aweze kujiajiri, haina maana kuongeza shule na
wanafunzi wanaojiandikisha huku ubora wa elimu ukiwa bado upo nyuma,”
anasema Profesa Kessy.
Anaongeza: “Mwalimu wa zamani alikuwa mwalimu
kweli, lakini leo hii amekuwa hathaminiki hivyo ni wakati wa Serikali
kuhakikisha inarudisha hadhi ya mwalimu kwa kumboreshea masilahi na
mazingira mazuri ya kuishi hasa mikoani.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Kitila Mkumbo anasema ili kuzalisha wasomi wenye weledi na wenye
kushindana katika soko la ajira ni lazima kuwe na walimu makini na
wanaoipenda kazi yao.
Anasema Serikali lazima iwekeze katika elimu kwani
mwalimu akiwa mzuri hata mwanafunzi atamwelewa lakini ukiwa na walimu
ambao siyo makini ni ngumu kupata jamii iliyoelimika.
Dk Mkumbo anasema kuna ulazima mfumo wa elimu
ukatazamwa upya ili kuepuka tabaka la wanafunzi wanaoendelea kuhitimu
wakiwa hawana ujuzi.
Aidha, Dk Mkumbo anawaomba Watanzania kutumia
uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 kuchagua kiongozi ambaye atakuwa na
agenda ya elimu na walioelimika.
Anasema tunahitaji kuchagua viongozi ambao watakuwa na agenda ya
elimu kwani bila kuboresha sekta ya elimu nchi haitapiga hatua kutokana
na kutokuwa na wataalamu wa kutosha wa kada mbalimbali.
Kauli ya washiriki
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Catherine Sirikwa
anasema serikali inatakiwa kuweka mazingira bora ya walimu hasa
wanaofundisha katika mazingira magumu.
Anasema mazingira ya vijijini bado siyo rafiki kwa
walimu kutimiza majukumu yao ipasavyo, hivyo kunahitajika jitihada za
makusudi kuwezesha maeneo hayo kuwa rafiki.
“Mishahara ikiboreshwa na mazingira ya kufundishia
hasa ya vijijini yakiimarishwa, nina hakika kwamba walimu wataipenda
kazi yao na kutekeleza kwa weledi mkubwa,” anasema Sirikwa.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee ya
jijini Dar es Salaam, Dominick Elias anasema shule za umma mara nyingi
zinakosa uangalizi wa karibu ukilinganisha na shule binafsi.
Anasema katika mchakato huu wa Katiba kunahitajika
kuwapo kwa kipengele kitakachowabana viongozi wa umma kupeleka nje
watoto wao kusoma.
“Shule hizi za Serikali hazitaimarika endapo
viongozi wataendelea kupeleka watoto wao nje ya nchi hivyo Katiba ijayo
inatakiwa kuwabana watoto wao wakasoma katika shule hizi ili wawe na
uchungu wa kuziboresha,” anasema Elias
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, tawi la
Dar es Salaam, Godfrey Kisemba anasema elimu inayotolewa inatakiwa
kuwajengea uwezo wa kuwawezesha kujenga viwanda vidogovidogo.
Anasema mitalaa ya elimu bado haina mbinu
zinazomwezesha mwanafunzi anapohitimu anakuwa na uwezo mara baada ya
kuhitimu masomo yake.
“Elimu yetu kweli bado haina mfumo thabiti kwani
unaweza kuwakuta wanafunzi wamehitimu vyuo vikuu lakini hawana lolote la
kufanya zaidi ya kusubiri kuajiriwa,” anasema Kisemba
Anaongeza: “Tunatakiwa kuwa na elimu ambao
utabadili fikra za watu kwa kuwaandaa wanafunzi siyo waishi mijini bali
vijijini ambako wataweza kuanzisha miradi kadhaa mfano ya kilimo, uvuvi
au ufugaji.”
Mwanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya
Jitegemee, Sylvia Mkomwa anasema baadhi ya wanafunzi wanashindwa kufikia
malengo yao kwa kuendekeza anasa kabla ya wakati.
Anasema kunahitajika kuwapo na semina mbalimbali
hasa kwa wanafunzi wa kike kuelezea madhara yanayotokana na kuanza anasa
mapema.
“Wazazi wanatakiwa kushirikiana na watoto wao kwa
ukaribu katika kuelekeza na kutokuacha jukumu hilo kwa walimu pekee
kwani mwisho wa siku anayebeba mzigo ni mzazi mwenyewe,” anasema Mkomwa
Anaongeza: “ Serikali iendelee kutoa elimu kwa
usawa hasa vijijini ambako bado baadhi ya wazazi hawawapeleki watoto
shuleni na kuwaacha nyumbani wakitekeleza majukumu ambayo si ya kwao.”
Post a Comment