Allan Goshashi
iku zote historia hukumbuka mabingwa. Bingwa ni bora kuliko
aliyeshindwa. Unaweza kusema mambo mengi kuhusu bingwa, lakini bingwa
anapopatikana ni kielelezo cha mafanikio.
Unaweza kusema bingwa siyo kila kitu, sawa, kwa
sababu watu wengine huamini wakishiriki na kumaliza mashindano fulani
bila matatizo wao ni mabingwa.
Wapo wanaosema bingwa siyo kila kitu ila nia au
dhamira ya kutaka kuwa bingwa ndiyo jambo muhimu, wengine husema uzuri
wa mchezo kwanza halafu ndiyo bingwa, kwa hiyo ipo mitazamo mingi kuhusu
bingwa.
Zipo pia tafsiri nyingi za bingwa, lakini mimi
nazungumzia bingwa katika michezo kwa sababu kwa muda mwingi wanamichezo
wa Tanzania wameshindwa kuwa mabingwa katika mashindano ya kimataifa.
Kwa mtazamo wangu bingwa huandaliwa, kipaji peke
yake hakiwezi kumsaidia mwanamichezo au timu kuwa bingwa, lazima kuwe na
maandalizi ya kumuandaa bingwa.
Ninasema hivyo kwa sababu mwanamichezo ili awe
bingwa anatakiwa kuandaliwa zaidi katika maeneo matatu ambayo ni nguvu,
akili na saikolojia.
Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa michezo na
unayefahamu vizuri maeneo hayo matatu ni dhahiri ukiona timu mbili
zinashindana utagundua ni timu gani ina nafasi nzuri ya kushinda kwa
sababu unaweza kuona nguvu, akili (kwa sababu ya mbinu zinazotumiwa) au
utaona umakini unaotokana na mwanamichezo kujengwa kisaikolojia.
Unaweza kujiuliza kwa nini nguvu?, ni kwa sababu
karibu katika kila mchezo mwanamichezo mwenye nguvu inayotakiwa ana
asilimia kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo husika. Mwanamichezo ni
lazima awe na nguvu, kasi na stamina, hivyo vyote hupatikana katika
mwili wa mwanamichezo aliyeandaliwa kuwa na nguvu nzuri jambo ambalo
haliwezi kufanyika kwa muda mfupi.
Pia unaweza kujiuliza kwa nini akili?, ni kwa
sababu mwanamichezo anatakiwa kuwa na maarifa mazuri ya mchezo
anaoucheza na kujua sheria zake.
Akili uhitajika kwa mwanamichezo kwa sababu
michezo mingi inahitaji mbinu, kwa kuwa zipo mbinu za kushambulia na
kuzuia, kwa mfano katika mchezo wa kikapu mchezaji anatakiwa kujua mbinu
za kufunga na kupata pointi, lakini anatakiwa pia kufahamu mbinu za
kuzuia mpira, kutoa pasi sahihi, kuiba mpira au kuingilia pasi za timu
pinzani.
Vilevile akili uhitajika kwa wanamichezo kwa
sababu makocha wanakuwa na mikakati yao ya kutaka kuisaidia timu
kushinda mechi hivyo lazima wachezaji wamuelewe mwalimu, kwa mfano wapo
makocha ambao huwafundisha wachezaji wao kutumia macho kudanganya
wanamichezo wa timu pinzani wanapokuwa uwanjani na mkakati huo
umefanikiwa sana kwa makocha katika mchezo wa soka au kikapu.
Unaweza pia ukajiuliza kwa nini saikolojia?, ni
kwa sababu wanamichezo walioandaliwa vizuri kisaikolojia wana uwezo wa
kuifunga timu nzuri yenye wachezaji wenye vipaji kama hawajaandaliwa
vizuri kisaikolojia.
Makocha nao huwa wanawapa maneno mazuri wachezaji wao ili
kuwafanya wapambane kwa uwezo wao wa juu, ambapo hali hiyo uhitaji
mchezaji aliyeandaliwa kisaikolojia kumuelewa kocha wake akiwa mchezoni.
Ipo mifano mingi katika masuala ya nguvu, akili na
saikolojia kwa wachezaji ambayo wachezaji wanaweza kuipata kama
wakiandaliwa vizuri kwa muda mrefu.
Mambo yote hayo yanataka viongozi wa michezo
wanaofahamu masuala ya michezo na wenye elimu ya biashara, pia michezo
inatakiwa kuongozwa na watu wenye uzoefu wa programu, utawala hasa
katika bajeti, kupanga matukio na masuala ya masoko.
Lazima tuelewe hivi sasa michezo inahitaji wanamichezo weledi kwa hiyo mahitaji ya viongozi weledi pia ni makubwa.
Kinachoonekana nchini ni kwamba hatuna viongozi
weledi wa michezo nchini watakaowezesha kuhakikisha mabingwa
wanaandaliwa nchini ila tunategemea tu vipaji vya wachezaji kutafuta
ubingwa katika mashindano mbalimbali na hata matokeo tunayoyapata
kimataifa yanaonyesha hivyo.
Post a Comment