Ibrahim Bakari
Naingia tena kwenye ulingo huu wa hoja kuzungumzia mambo yetu yanayotuhusu ya michezo.
Leo nataka kuizungumzia Azam FC hasa maandalizi
yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ACL, ambayo inafikia ukingoni kabla ya
kuanza mwanzoni mwa mwaka ujao.
Itakumbukwa, kwa mara ya kwanza, walimaliza nafasi
ya nne, mwaka uliofuata walikuwa watatu, wakashika nafasi ya pili na
leo hii ni nafasi ya kwanza, kwa kweli hongereni sana.
Niliwahi kuwapongeza na leo nawapongeza tena Azam
FC, ukweli wanastahili pongezi kwa kuwa waliingia kwenye Ligi Kuu wakiwa
na malengo ya kweli katika kuendeleza soka Tanzania.
Wanajipanga kuanzia nyenzo za uwanjani, wamejipanga hata katika rasilimali ya wachezaji kwa kuwekeza katika soka ya vijana.
Azam walionyesha kweli wana nia ya ushindi tangu kuanza kwa ligi na ndiyo maana walimaliza ligi bila hata kupoteza mechi.
Lakini kikubwa ninachotaka kuwakumbusha viongozi
na benchi la ufundi, ni kwamba wakati unayoyoma kutengeneza timu
madhubuti kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani. Wakati ndiyo huu
badala ya kusubiri mchakamchaka wa mwisho wa mwaka.
Ninachokiona kwa upande wangu japo ni utashi wa
kocha, kuwa ni wakati wa kusajili wachezaji wenye sifa za kucheza Ligi
ya Mabingwa Afrika msimu ujao na zaidi ni wachezaji walio na tija.
Kama alivyosema awali kocha wa timu hiyo kuwa
wachezaji wengi waliopo hawana uwezo wa mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa
Afrika hivyo kuna kila sababu ya kupata wachezaji wenye uwezo mapema
zaidi.
Imekuwa kawaida kwa klabu za Simba na Yanga,
kusajili wachezaji kwa ajili ya mechi za watani, ama Simba au Yanga kitu
ambacho kinawafanya washindwe kufurukuta mashindano ya kimataifa.
Ukiangalia timu ya TP Mazembe ya DRC, huwa
inasajili wachezaji kwa kuangalia majukumu yaliyo mbele yao. Hutumia
fedha nyingi kupata nyota wakali kwa ajili ya ligi na michuano ya
kimataifa.
Sasa, ikiwa kocha wa Azam na benchi zima la
ufundi, watataka kusajili kwa kuangalia wachezaji gani wa kuifunga Simba
au Yanga ni kwamba watapoteza mwelekeo.
Wachezaji wasajiliwe kulingana na uwezo kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
Vilevile kingine ninachotaka kusema ni kwamba
benchi la ufundi liachwe lifanye kazi yake pasi na kuingiliwa na watu
ambao mwisho wa siku lawama zote zinaelekezwa kwa kocha.
Kocha afanye kazi yake, kocha asajili wachezaji
anaodhani na anaowaamini kuwa ndiyo watakaomsaidia katika kazi yake
baadaye, ndani na nje.
Kwa sasa, ni wazi wapo wachezaji ambao, kimsingi
hawastahili tena kuwepo Azam, na kilichobakia ni kupewa kiinua mgongo
chao na watakaokuwepo wawe chachu ya mafanikio zaidi.
Nimeirejea Azam kwa kuwa ndiyo wawakilishi wetu
Afrika na ndiyo klabu naweza kusema inaweza kusajili kutokana na nafasi
yake ikilinganishwa na klabu nyingine.
Ukweli kinachotakiwa ni maandalizi ya mapema na kucheza mechi nyingi za kirafiki ili kuipa timu uzoefu.
Post a Comment