Dar es Salaam. Sekta ya kilimo nchini itakua
kwa kasi endapo msaada wa magari kwa taasisi zinazosimamia sekta hiyo
utatumika ipasavyo kuwawezesha watendaji kuzungukia maeneo mbalimbali
kufanya utafiti.
Umoja wa Ulaya (EU) umetoa magari 21 ili kusaidia sekta ya kilimo nchini, ambayo hutegemewa na Watanzani wengi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo,
kiongozi wa ujumbe wa EU, Tom Vens alisema wanafanya jitihada za
kubadilisha sekta ya kilimo barani Afrika ili ibadilishe maisha ya watu
wake.
Vens alisema mabadiliko yatafanyika kama taasisi
za kitafiti zitawezeshwa vitendea kazi muhimu, baadaye taasisi hizo
kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwapa ushauri wa kitaalam.
Alisema ushirikiano kati ya EU na Tanzania
umebainisha usalama wa chakula kama kipaumbele katika uhusiano wao.
Mazao yanayolengwa zaidi ni kahawa, pamba, chai, uvuvi na mazao ya
mbogamboga.
“Taarifa sahihi, mtaji na ujuzi ndiyo vitu muhimu
katika kukuza kilimo. Pato la taifa litokanalo na kilimo litaongezeka na
kulinufaisha taifa,” alisema Vens.
Baada ya kupokea msaada huo, katibu mkuu wa Wizara
ya Fedha, Dk Servacius Likwelile alisema magari hayo yatagawiwa kwa
taasisi za kitafiti zilizo chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula.
Taasisi hizo ni ya Utafiti wa Kahawa (TCRI), Bodi
ya Pamba (TCB), Maabara ya Mazao ya Uvuvi (NFCL), Shirika la Viwango
(TBS) na Taasisi ya Chai (TIT). Magari hayo yana thamani ya Sh8 bilioni.
Post a Comment