Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Ofisi ya Rais imesema kuwa wanaomkosoa Rais
Jakaya Kikwete kuhusu msimamo wake katika mchakato wa Katiba Mpya hawako
sahihi kwa kuwa ni mlezi na ana haki ya kutoa maoni yake kama mkuu wa
nchi na kama mwanasiasa.
Pia, imewataka wasiokuwa wajumbe wa Bunge la
Katiba waiache kazi hiyo mikononi mwa Bunge hilo kwa sasa hadi hapo
rasimu itakapowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya
kuikubali au kuikataa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu ikiwa ni siku moja baada ya Jumuiya ya
Kikristo Tanzania (CCT), kutoa tamko zito kwa Rais Jakaya Kikwete
ikiishangaa kauli yake ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba iliyotokana na maoni ya Watanzania.
Rais Kikwete amekuwa akilaumiwa na taasisi na watu
binafsi baada ya kulieleza Bunge la Katiba kuwa kuna baadhi ya mambo
kwenye Rasimu ya Katiba ambayo hayawezekani kutekelezeka, akitoa mfano
wa muundo wa Muungano wa serikali tatu, jambo ambalo CCT ilisema jana
kuwa alitakiwa alifanye wakati Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa
ikimfuata kumweleza maendeleo ya kazi yao.
Hata hivyo jana, Rweyemamu aliliambia gazeti hili
kuwa: “Kinachoendelea kwa sasa kwa baadhi ya makundi ya kidini kutoa
matamko dhidi ya Rais si sahihi, kwa kuwa Rais ni mlezi na ana haki ya
kutoa mtazamo wake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa.”
Alisema kimsingi mchakato huo ni wa kisiasa na
Rais ni mwanasiasa, pia ni mkuu wa nchi hivyo ndiye mwenye uwezo wa
kutoa ushauri na kutoa angalizo pale inapohitajika, hasa anapoona kuna
jambo lisilokuwa sawa, hivyo hakuna haja ya kuendelea kusimama kupinga
kile alichokielekeza nje ya Bunge.
“Tulioko nje ya Bunge la Katiba hebu tuwaachie
wajumbe. Rais kama msimamizi mkuu atakoseaje kwa kutoa ushauri?
Alichokifanya ni sahihi na kama kuna tatizo, walioko nje ya Bunge warudi
ndani ili wajadiliane kwa kina na kumaliza tatizo,” alisema.
Kauli ya CCM
Wakati Rweyemamu akisema kazi hiyo ya mjadala wa
katiba iachwe kwa wajumbe wa chombo hicho cha kuandika Katiba, CCM
ilisema jana kuwa kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake kuhusu mchakato
huo na akaisifu CCT kwa kutumia haki hiyo ya kikatiba.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema katika mchakato wa kupatikana kwa katiba iliyo bora, kila mtu na
kila kundi lina fursa ya kutumia uhuru wa kikatiba kueleza na kutoa
maoni yao, hivyo viongozi hao wa CCT wametumia vyema uhuru huo.
Alisema kwamba anaamini CCT haikufanya hivyo
kimakosa kama ambavyo makundi mengine, wakiwamo majaji, chama chake na
hata watu binafsi wamekuwa wakifanya, kwa kutoa mitazamo yao kuhusu aina
ya muundo wa Serikali wanayohitaji.
“Siyo hao tu, tunatarajia na wengine zaidi
watatoa. Hiyo ni haki ya kimsingi iliyowekwa na Katiba. Hatupo hapa kwa
ajili ya kushindanishwa, tunaamini Bunge lipo kwa mujibu wa sheria nalo
litaendelea kusimamia taratibu zake, hatuna sababu ya kumziba mtu
mdomo.”
Post a Comment